Mchungaji mbaroni kwa madai ya kumkashifu Museveni

Rais Museveni

Muktasari:

Taarifa ya Jeshi la Polisi inasema kuwa Mchungaji Kabuleta alikua akiendesha kampeini kali katika mitandao ya kijamii akikosoa utawala wa Rais Museveni na familia yake.

Kampala, Uganda. Jeshi la Polisi nchini Uganda linamshikilia Mchungaji, Joseph Kabuleta kwa tuhumaza za kumkashifu na kumasirisha Rais Yoweri Museveni.

Mchungaji Kabuleta, alikamatwa siku ya Ijumaa na makachero wa jeshi hilo akiwa jijini Kampala, Uganda.

Taarifa ya jeshi hilo inasema kuwa Mchungaji Kabuleta alikua akiendesha kampeini kali katika mitandao ya kijamii akikosoa utawala wa Rais Museveni na familia yake.

Shirika la habari la BBC lilisema kuwa kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mchungaji Kabuleta aliandika kuwa mpango mzuri ni kuhakikisha Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa kiongozi huyo hamrithi baba yake.

"Tayari Jenerali Muhoozi amekuwa akitumwa kumwakilisha baba yake kwa mikutano ya kimataifa na kukutana na mabalozi na viongozi wengine wa ngazi za juu.

"Huenda baba yake ana mpango wa kustaafu kimpango baada ya kuchakachua uchaguzi wa mwaka 2021 na kuchukua jukumu la kumshauri mwanawe huku akiendelea kundesha biashara ya kampuni ya familia inayofahamika kama Uganda,” ilisema sehemu ya ujumbe wa mchungaji huyo.

Ujumbe huo pia ulisema “mpango wowote walionayo, nahisi mambo huenda yakabadilika. Himaya ya mafia imeanza kuporomoko na Uganda itarejea mikononi mwa Waganda."