Baba aeleza alivyoshuhudia mwanaye akipigwa risasi kanisani

Muktasari:

Mkurugenzi huyo wa mji wa Itigi anadaiwa kufanya mauaji hayo na tayari polisi wanamshikilia; waziri Jafo, mkuu wa Mkoa wa Singida wazungumzia tukio hilo

Dar es Salaam. Petro Kulwa, baba mzazi wa kijana anayedaiwa kupigwa risasi na mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Pius Luhende na kupoteza maisha, amesimulia alivyoshuhudia kifo cha mwanaye.

Mwanaye huyo, Isaka Petro anadaiwa kuuawa kwa risasi akiwa kanisani.

“Nilishuhudia mwanzo hadi mwisho mama yangu, siyo picha mbaya tu ni ya kuogofya mno,” alisema Chambalo.

“Walivyoingia walifanya fujo, waliwakata watu ngwala, nilikuwa nasisimka mwili na kujiuliza kimoyomoyo kuna nini, mbona nyumba ya ibada haina amani, lakini walipompiga risasi kijana wangu mwili ulikufa ganzi na hadi sasa ni kama nimepigwa na butwaa.”

Chambalo alifafanua kuwa alikuwa kanisani pamoja na familia yake, lakini ghafla magari mawili yalisimama nje ya kanisa na waumini wote walishtuka akiwamo yeye.

Alisema baada ya dakika chache watu waliokuja na magari hayo waliingia kanisani na miongoni mwao alikuwamo Luhende wakawa kama wanamtafuta mtu, mara wakatoka nje kabla ya kurudi na kumuua kwa kumpiga risasi kijana wake.

“Sikuwahi kusikia wala kushuhudia Isaka akiwa na ugomvi au visa na mtu, tukio lililotokea kanisani linanishangaza sana, kuna wakati nawaza labda walikosea hawakuwa wakimtafuta yeye na kuna kipindi nawaza hajakufa, ila kwa sababu tupo hapa kwenye mazishi naamini sasa mwanangu ameuawa,” alisema mzazi huyo.

“Nilimshuhudia kwa macho yangu mkurugenzi akimpiga mwanangu risasi na kuondoka wakikimbilia kwenye magari waliyokuja nayo kisha kuondoka kwa kasi.” Alisema ameachiwa familia ya mke na watoto watatu ambao hajui atawafanya nini kuwalea.

“Najua amekamatwa na amewekwa ndani, yote hayo yafanyike lakini mwanangu ndiyo ameshafariki na ameacha hii familia, nitaifanya nini na mimi ni mkulima wa kilimo cha kizamani, natamani Serikali iangalie namna ya kuwasaidia hawa watoto na mama yao,” alisema mzazi huyo.

Chambalo alisema miongoni mwa watu waliohudhuria mazishi ya mwanaye jana jioni ni Pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tamisemi, Selemani Jafo.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Jafo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mkurugenzi huyo na askari wawili wa wanyamapori wanashikiliwa na polisi kutokana na tuhuma hizo za mauaji.

Mchungaji wa Kanisa la Adventista Sabato yalikotokea mauaji hayo, Manyigina Manyigina alisema alipata taarifa hizo akiwa Manyoni alikokuwa akiendesha ibada nyingine.