CAG ataja benki 4 za Serikali zinazojiendesha kwa hasara

Thursday April 11 2019
CAG BENK PIC

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amebaini benki nne za Serikali kati ya sita (asilimia 67) zilikuwa zikifanya biashara kwa hasara kwa miaka mitatu mfululizo wakati benki nyingine zikiwekwa chini ya uangalizi wa BoT.

Ameeleza kuwa mapungufu hayo ameyabaini kwenye ukaguzi alioufanya Benki ya Wanawake Tanzania(TWB), Benki ya Biashara ya TIB, Benki ya Maendeleo TIB na Benki ya Twiga.

"Nilibaini kuwa benki nne(asilimia 67) kati ya benki sita zinazomilikiwa na Serikali zilipata hasara kwa miaka miwili mfululizo,"ameeleza CAG katika ripoti yake.

Ameeleza kati ya benki hizo, benki mbili(Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Benki ya Twiga zilipata hasara kwa miaka mitatu mfululizo).

Pia amesema alibaini kuwa Benki ya Maendeleo ya TIB ilifuta mikopo yenye thamani ya Sh3.69 bilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2017.

"Hasara hizo zinasababishwa zaidi na na mapungufu katika kufanya upembuzi wa maombi ya mikopo, dhamana zisizotosheleza kudhamini mikopo na mapungufu ya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo kwa wateja waliopitisha muda wa kurejesha mikopo na mapungufu katika maamuzi ya mchakato wa kutoa mikopo,"ameeleza CAG katika ripoti yake.

Advertisement

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mashirika ya umma ya mwaka 2017/18, CAG pia amebaini kwamba uwiano wa mikopo chechefu ya benki tatu dhidi ya mikopo yote ya benki hizo umekuwa ukiongezeka zaidi ya kiwango kilichowekwa cha asilimia 11.7 pamoja na lengo la BoT la asilimia 5.

“Nilibaini Benki tano za Serikali zilikuwa na uwiano wa chini wa mtaji wa msingi na mtaji wa jumla ikilinganishwa na mali zinazoambatana na vihatarishi na mali zilizo katika hali hatarishi zilizo nje ya urari wa kimahesabu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2014 na mwongozo wa BoT wa Agosti 5, 2015,” amebainisha CAG kwenye ripoti hiyo.

NBS tegemezi

Pia, CAG amebaini kwamba kiwango kikubwa cha shughuli kuu zinazofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinafadhiliwa na wahisani, jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji wa shughuli muhimu za ofisi hiyo.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa ukaguzi 2017/18, taasisi hiyo ilikuwa na bajeti ya Sh1.64 bilioni ambazo imewezeshwa na Serikali kwa ajili ya kushughulikia masuala muhimu yahusuyo taasisi isipokuwa mishahara.

“Kiasi cha Sh. bilioni 13.84 kilifadhiliwa na Mradi wa Mpango Mkuu wa Kitakwimu Tanzania (TSMP) kwa ajili ya kutimiza majukumu muhimu ya NBS, ambapo pesa zinatoka kwa wabia wa maendeleo,” amesema na kupendekeza Serikali iongeze ruzuku ili taasisi hiyo  iweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.

Advertisement