Dawa za kupambana na ebola zaonyesha matumaini

Muktasari:

  • Wizara ya Afya ya Congo imesema kuwa dawa aina nne zilijaribiwa kwa wagonjwa wa ebola na mbili zimeonyesha uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Congo. Majaribio ya dawa mbili za ugonjwa wa ebola yameonyesha mafanikio makubwa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Wizara ya Afya ya Congo ilisema kuwa dawa aina nne zilijaribiwa kwa wagonjwa wa ebola na mbili zimeonyesha uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, utafiti huo ulianza Novemba mwaka jana na kudhaminiwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti kuhusu uzio na maradhi ya kuambukiza ya nchini Marekani (NIAID) na kuratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

 “Dawa hizo sasa zitatumika kutibu wagonjwa wote wa ebola ambao wapo katika vituo mbalimbali,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la habari BBC, taarifa ya NIAID imesema kuwa “matokeo hayo ni habari njema katika mapambano dhidi ya ebola.”

Mkurugenzi wa NIAID, Dk Anthony Fauci alisema kuwa dawa hizo kisayansi zimeonesha kuwa muhimu kwa kupunguza vifo vya wagonjwa wa ebola.

Dk Fauci alizitaja dawa hizo kuwa ni REGN-EB3 na mAb114, ambazo zinafanya kazi ya kuvishambulia virusi vya ebola kwa kuzipa nguvu chembe chembe za kinga za mwili zinazopambana na maradhi.

Hata hivyo, Dk Fauci alisema dawa nyingine mbili aina ya ZMapp na Remdesivir zimeshindwa kufanya vizuri kwenye majaribio hayo.

Dk Fauci alisema utafiti huo ulihusisha wagonjwa 700 na matokeo ya awali yameonyesha kuwa 499 kati yao wamepona

Mkurugenzi wa mfuko wa msaada wa masuala ya huduma za kiafya Wellcome Trust, Jeremy Farrar alisema dawa hizo zitaokoa maisha ya wananchi wengi ambao walikuwa wakipotea kutokana na ugonjwa huo.

Farrar alisema matokeo hayo yanaonyesha mwanga na kufanya ugonjwa wa ebola sasa kuzuilika na kutibika.

''Hatuwezi kutokomeza ugonjwa wa ebola kabisa, lakini tuwe na uwezo wa kuzuia ugonjwa huu kuwa mkubwa katika taifa na ukanda,” aliongeza.

Mlipuko wa ugonjwa wa ebola Mashariki mwa Congo ulianza mwezi Agosti, mwaka jana na kusababisha zaidi ya watu 1800 upoteza maisha.

Ugonjwa huo pia uliathiri watu 28,616 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.