Dk Tulia aagiza Lema kuhojiwa na Kamati ya Bunge, wapinzani watoka nje ya ukumbi wa Bunge

Tuesday April 2 2019

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akizungumza bunge kabla ya Naibu Spika, Dk Tulia Acksom kumsimamisha kuendelea kuzungumza na kuagiza mbunge huyo ahojiwe na Kamati ya Bunge ya Haki,  Maadili  na Madaraka ya Bunge kwa kutamka bungeni kuwa Bunge ni dhaifu, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Dodoma. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameagiza Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kutamka bungeni kuwa Bunge ni dhaifu.

Uamuzi huo umesababisha wabunge wa upinzani kunyanyuka walipokuwa wameketi na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge. Waliotoka nje ni wabunge wa Chadema na baadhi ya wabunge wa CUF.

Dk Tulia amechukua uamuzi huo baada ya Lema wakati akichangia hoja ya kamati hiyo kudai Halima Mdee hajatendewa haki kutokana na kamati hiyo kupendekeza Bunge kumsimamisha kuhudhuria vikao viwili vya Bunge kutokana na kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuwa Bunge ni dhaifu

"Alichokisema Mdee naungana naye na nikweli kuwa Bunge ni dhaifu," amesema Lema. Baada ya kauli hiyo Dk Tulia aliagiza Lema kuhojiwa na kamati hiyo kuthibitisha kuwa kweli Bunge ni dhaifu, kauli ambayo iliwanyanyua wabunge hao.

Baada ya wabunge kuchangia mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu mbunge huyo wa Kawe, alilihoji Bunge na kupitisha azimio la Mdee kutoshiriki mikutano miwili ya Bunge.

"Bunge limeazimia kuwa Mdee hatashiriki mkutano huu (wa Bajeti)  wa 15 wa Bunge na mkutano wa 16 utakaofanyika Septemba na Oktoba, 2019," amesema Dk Tulia.

Advertisement


Advertisement