Halima Mdee afanyiwa upasuaji Dar, atoa neno

Saturday June 8 2019

Mbunge wa Kawe Chadema, Halima Mdee,hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam,

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee amelazwa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe tumboni.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Juni 8, 2019 Mdee amemshukuru Mungu kwa kuwa anaendelea vizuri, “Nilikuja hospitali juzi (Alhamisi) saa tisa alasiri kwa ajili ya kuangalia afya yangu.”

“Ila madaktari baada ya kunichunguza na kufanya vipimo wakabaini tumboni kuna tatizo na kunishauri nifanyiwe upasuaji haraka iwezekanavyo.”

Amebainisha kuwa kwa sasa anaendelea vyema na afya yake inazidi kuimarika tofauti na jana, kuwataka wapiga kura wake kutokuwa na wasiwasi.

“Nipo vizuri na kati ya kesho au Jumatatu madaktari wataniruhusu kurudi nyumbani,” amesisitiza Mdee.

Theresia Ngowi, mama mzazi wa Halima amesema jambo analoshukuru ni mwanaye kutoka salama katika chumba cha upasuaji.

Advertisement

“Nilisimama katika neno la Mungu wakati mwanangu akiwa  chumba cha upasuaji. Niliamini atapata ahueni  na kurudi salama kwa sababu nilimwamini Mungu.”

"Unajua ukiwa unauguza mtoto, anayepata shida ni anayemuuguza  kwa kweli kwa hatua hii namshukuru Mungu sana. Hii ndio operesheni ya kwanza kufanyiwa mwanangu," amesema Theresia.

Mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya ameungana na Theresia kumshukuru Mungu kufanikisha upasuaji huo.


Advertisement