Kodi, tozo chanzo biashara kufungwa Mtwara

Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Abdallah Mwinyi amesema sababu ya wafanyabiashara wa Mkoa wa  Mtwara kurudisha leseni zao ni utitiri wa kodi na tozo mbalimbali

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Abdallah Mwinyi amesema sababu ya wafanyabiashara wa Mkoa wa  Mtwara kurudisha leseni zao ni utitiri wa kodi na tozo mbalimbali.

Hivi karibuni, wafanyabiashara zaidi ya 100 wa Mtwara wameripotiwa kufunga biashara na kurudisha leseni zao.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Mei 15, 2019 mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara-Mikindani, Emmanuel Mwaigobeko amekiri kuwepo kwa suala hilo, akisema wafanyabiashara wanalalamikia mzunguko mdogo wa biashara na kushindwa kulipa kodi ya pango.

Katika maelezo yake Mwinyi amesema wafanyabiashara wanalipa kodi na tozo lukuki zikiwemo za taka, zimamoto, leseni ya stoo na duka, leseni ya bidhaa tofauti ushuru wa kuegesha magari.

“Kodi ya pango siyo sababu, mtu akishindwa kulipa kodi anahamia sehemu nyingine. Suala kubwa hapa ni utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara, wanalipa kodi 37, huwezi kufanya biashara hapo,” amesema Mwinyi.

Katibu mkuu huyo wa JWT alitoa ombi kwa Serikali kupunguza kodi na kuondoa tozo nyingine zisizo za lazima ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara yatakayowawezesha wafanyabiashara kufanya kazi zao.

Katika maelezo yake Mwaigobeko amesema wafanyabiashara wanarejesha leseni zao za biashara kwa sababu ya mzunguko mdogo wa biashara unaowafanya washindwe kulipa kodi zao za pango.

Mwaigobeko amesema kodi ya pango kwenye majengo ya halmashauri hiyo yaliyopo soko kuu na stendi ya Mtwara ilipunguzwa mwaka jana kutoka Sh75,000 kwa flemu kubwa na Sh50,000 kwa flemu ndogo.

Alisema baada ya malalamiko ya wafanyabiashara hao, manispaa yake ilipunguza kodi ya pango mpaka Sh40,000 kwa flemu kubwa na Sh20,000 kwa flemu ndogo ili wafanyabiashara hao waendelee kufanya biashara.