Kupanda na kushuka kwa Lowassa katika mapambano ya kisiasa

Kama kuna kitu kilichompaisha Edward Lowassa katika safari yake ya kisiasa ni kambi ya wagombea urais iliyoitwa Boys two Men. Ni kambi iliyowahusisha Jakaya Kikwete na Lowassa ambapo mwaka 1995 walikwenda Dodoma kwa ndege ya kukodi kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM.

Hata hivyo, safari ya Boys two Men iliendelea hata baada ya jina la Lowassa kukatwa mapema na Kikwete jina lake lilifika hadi kwenye mkutano mkuu uliofanyika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.

Matumaini ya Boys two Men yalibaki kwa Kikwete lakini mkutano mkuu wa CCM uliohudhuriwa na Mwalimu Nyerere ulikatisha ndoto ya Kikwete baada ya Benjamin Mkapa kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 1995.

Kukatwa kwa jina la Kikwete kulisababisha taharuki ndani ya CCM, baadhi ya wafusia na wanachama wa chama hicho walianza kuimba; ‘bai bai CCM’ wakimaanisha wana mpango wa kukikimbia chama hicho na kujiunga na upinzani. Wakati huo mpinzani aliyekuwa na nguvu alikuwa Augustine Mrema aliyegombea urais kupitia NCCR-Mageuzi.

Baada ya Mkapa kumaliza kipindi chake cha awamu ya mbili mwaka 2005, CCM ilikuwa na kazi ya kuteua mgombea urais mwingine na safari hii kambi ya Boys two Men ilishinda kwa Kikwete kuteuliwa kuwa mgombea na hatimaye kuwa Rais.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wakati Kikwete akimaliza awamu yake ya pili ya uongozi wa nchi, Lowassa alikuwa bado na matumaini ya mshikamano wa Boys two Men, lakini safari hii haikuwa hivyo, jina lake lilikatwa kwenye Kamati ya Maadili ya CCM na baadaye alilazimika kutimkia Chadema.

Maisha yake kisiasa

Maisha yake ya kisiasa yamepitia vipindi tofauti huku vingi vikiwa ni vile vilivyomwezesha kuwa maarufu na kupata mafanikio makubwa.

Katika wasifu wake, Lowassa aliyezaliwa Agosti 26, 1953 huko Monduli mkoani Arusha, ameshika nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali na kisiasa tangu alipohitimu shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977 na baadae shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Bath nchini.

Mwaka 1989 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na kufuatiwa na nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri. Miongoni mwa wizara alizowahi kuziongoza tangu miaka ya 1990 ni pamoja na maji, mazingira ardhi na nyinginezo.

Ateuliwa kuwa waziri mkuu

Baada Kikwete na Lowassa kushindwa kufikia malengo ya kukalia kiti cha urais 1995, waliendelea kujipanga na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 wawili hao waliamua kuungana mkono.

Inaelezwa kuwa walikubaliana Kikwete atangulie katika urais huku Lowassa akimuunga mkono kwa namna mbalimbali hadi walipofanikisha adhma yao hiyo na JK kuingia Ikulu.

Baadaye Kikwete alimteua Lowassa kuwa waziri mkuu nafasi ambayo ndiyo ya juu zaidi mpaka sasa kufikiwa na mwanasiasa huyo aliyesoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo iliyoko mkoani Tabora.

Alidumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu mpaka mwaka 2008 alipojiuzulu na huenda hapo ndipo zilipoanzia figisu za kisiasa zilizomfanya aandike historia katika Taifa na kushindwa kuingia Ikulu mpaka leo.

Kashfa ya Richmond

Februari 7, 2008 Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu baada ya kushutumiwa kushawishi nchi kuingia mkataba na kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Company LLC, ya Marekani ambayo ilishindwa kutekeleza makubaliano ya kimkataba.

Uamuzi wa kusaka kampuni ulitokana na hali ya ukame ulioikumba nchi mwaka 2006 na kufanya vyanzo vya maji vilivyokuwa vikitegemewa kwa ajili ya uzalishaji umeme kukauka hivyo kuhitajika namna nyingine ya kusaidia upatikanaji umeme.

Sakata hilo lilifikishwa bungeni ambapo Bunge liliunda kamati ya wabunge watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe, kufuatilia mkataba huo uliohusisha Ricmond na Tanesco kwa upande wa Tanzania.

Kamati hiyo ikabaini mkataba huo ambao uliipa kampuni hiyo jukumu la kuzalisha megawati 100 za umeme kila siku kuwa na dosari kwani mitambo ya dharura ya Richmond ilichelewa kufika nchini na hata ilipoletwa haikufanya kazi kwa kiwango kilichotakiwa. Hata hivyo, Serikali iliendelea kulipa zaidi ya Dola 100,000 za Marekani kila siku.

Lowassa alijiuzulu lakini alikanusha kuhusika kushawishi mkataba huo na kusisitiza kuwa kinachomng’oa si suala hilo bali ni ‘uwaziri mkuu’.

Akatwa, ahamia Chadema

Katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM kakatika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ndani ya CCM, jina la Lowassa lilionekana kuwa juu ya wagombea wote 42 waliojitokeza kukiomba chama chao kupeperusha bendera yake kwenye uchaguzi huo.

Katika hatua za awali ambapo CCM ilimtaka kila mgombea kudhamiwa na angalau wanachama 450, Lowassa aliwasilisha majina 700,000 ya waliokubali kumdhamini, hata hivyo, jina lake lilikatwa katika hatua za mwanzo kabisa na kukosekana katika yale yaliyoingia hatua ya tano bora. Uamuzi huo ulimchukiza na kulalamikia kuchezewa rafu.

Chama hicho kilimpitisha John Magufuli aliyekuwa Waziri wa Miundombinu kwa mgombea wake katika uchaguzi huo. Baadae aliamua kutimkia Chadema.

Alivyowagawa vigogo CCM

Lowassa aliyesoma Shule ya Msingi Monduli kuanzia mwaka 1961 hadi 1967 kisha kujiunga na Shule ya Sekondari Arusha mwaka 1968, ndiye mwanasiasa pekee mpaka sasa aliyeweza kuwagawa vigogo wa CCM katika vikao vya juu na kushindwa kumaliza tofauti zao ndani ya vikao. Katika mchakato wa kumpata mgombea wa chama hicho mwaka 2015, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM walitoka hadharani na kutamka mbele ya waandishi wa habari kuwa hawakubaliani na uamuzi wa kumkata Lowassa kuwania urais.

Wajumbe wa CC Adam Kimbisa, Dk Emmanuel Nchimbi na Sophia Simba aliyekuwa mwenyekiti wa UWT (wakati huo), walisema kuna hila zilizofanyika na hivyo hawakubaliani na uamuzi huo.

Mbali na hilo, wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambapo majina yaliyopitishwa na CC yalikuwa yakipelekwa kupigiwa kura, kundi la wajumbe lilisimama na kuimba linaimani na Lowassa wakati mwenyekiti wa chama hicho Kikwete (wakati huo) alipokuwa akiingia katika ukumbi wa mkutano.

Matukio kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa kabla ya hapo tangu kuanzishwa kwa CCM. Katika kile kinachoonekana ni matokeo ya kumuunga mkono Lowassa na matukio yaliyodaiwa kukiuka utaratibu wa chama hicho, baadhi ya wana CCM walivuliwa uanachama akiwamo Sophia Simba ambaye hata hivyo mwaka jana alirudishiwa uanachama baada ya kuomba msamaha kwa kuandika barua.

Lowassa alisababisha kundi kubwa la wana CCM kukihgama chama hicho na wengine kumfuata Chadema wakiwamo waliokuwa na nyadhifa mbalimbali kama wabunge, wenyeviti wa mikoa na makatibu.