Mabadiliko ya sheria ya madini yaongeza ukusanyaji wa mapato

Muktasari:

Katibu mkuu wa wizara ya madini Profesa Simon Msanjila amesema kiwango cha ukusanyaji maduhuli kimeongezeka kati yam waka 2011 hadi 2018.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila amesema kati ya mwaka 2011 hadi 2018, kiwango cha ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya madini mkoani Geita kimeongezeka kutoka Sh24bilioni hadi kufikia Sh114.78bilioni.

Amesema mafanikio hayo yamechagizwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwamo mabadiliko ya kisheria kwa lengo la kuongeza manufaa ya rasilimali hiyo kwa Taifa.

Profesa Msanjila ametoa kauli hiyo leo Jumapili Machi 17, 2019 wakati akihutubia katika tukio la uzinduzi wa soko la kwanza la madini hapa nchini.

Pamoja na mafanikio hayo katika ukusanyaji maduhuli, Profesa Msanjila amesema shughuli ya maandalizi ya upatikanaji wa maeneo ya masoko inaendelea kwenye mikoa mbalimbali.

“Tayari kazi ya kutenga maeneo inaendelea, wanaangalia vigezo vya kiusalama lengo ni kuhakikisha kila mkoa wenye madini unapata soko la madini,” amesema Profesa Msanjila.

Uzinduzi wa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa Januari 22, jijini Dar es Salaam mwaka huu kupitia mkutano wake na wafanyabiashara wa madini. 

Awali, mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema mikoa yenye rasilimali ya madini imekuwa na wananchi maskini lakini jambo hilo halitajitokeza kwa mkoa huo tena.

Amesema Geita inaenda kuandika historia na kujenga matumaini mapya kwa wananchi wake kupitia mapato yatokanayo na madini ya dhahabu.

Awali alisema mkoa huo unaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu kwa zaidi ya asilimia 40 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini.