Magufuli: Saudia itatujengea chuo kikuu cha Kiislamu - VIDEO

Monday May 20 2019

Rais  John  Magufuli akimzawadia  Sumayyah Juma

Rais  John  Magufuli akimzawadia  Sumayyah Juma Abdallah wa Tanzania baada ya kupata alama 98.66 na kuibuka mshindi wa tano wa Washindi wa Kuhifadhi Juzuu 30 katika mashindano maalum ya 20 ya Qur’aan Tukufu yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam jana. Picha na Ikulu 

By Aurea Simtowe na Bakari Kiango [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Saudi Arabia imeonyesha nia ya kujenga chuo kikuu cha Kiislamu nchini siku chache zijazo.

Alisema hayo jana alipohudhuria Mashindano ya 20 ya kusoma na kuhifadhi Qur’aan Afrika, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli alisema waziri wa nchi, na mjumbe wa Baraza la Mawaziri Saudi Arabia, Dk Saleh Alashiek amemhakikishia kuwa atakwenda kumueleza Mfalme wa nchi hiyo juu ya kujenga chuo kikuu cha Kiislamu nchini na kwamba ameonyesha nia ya kukubali.

“Japo hamkunituma ila niliona nimchomekee, kuonyesha utayari wao tu katika hili, ni ishara kuwa chuo hicho kitaanza kujengwa mapema iwezekanavyo na kitafadhiliwa na Saudi Arabia,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wazo hilo ni matokeo ya maagizo yake aliyoyatoa mwaka jana kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kumuagiza afuatilie kuona Saudi Arabia inaweza kuisaidia nini kikubwa katika masuala ya elimu hasa ya Kiislamu na kumtaka alisimamie vizuri suala hilo.

“Namshukuru sana mheshimiwa waziri pamoja na Mfalme wa Saudi Arabia kwa niaba ya Watanzania wote, lakini hii inadhihirisha kwamba Tanzania ina baraka ya pekee. Mwaka jana waziri huyu alipokuja alifika ofisini Ikulu na alishiriki mashindano ya 19, alipotoka tu huku Tanzania alipofika kule kwao alipandishwa cheo. Hii inadhihirisha namna gani sala na dua za Watanzania zilivyo nzuri na nina uhakika kwenye hili la chuo kikuu hutalisahau na inawezekana ukapandishwa tena cheo kingine,” alisema.

Advertisement

Alisema nchi hizo zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya kiuchumi na Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa zake ikiwamo kahawa, chai na tumbaku katika nchi hiyo pamoja na mazao mengine ya chakula.

“Mwaka 2016, mataifa yetu mawili yalisaini mkataba wa makubaliano kwenye masuala ya uchumi, biashara, uwekezaji, vijana na michezo ikiwa ni uthibitisho wa uhusiano mzuri na upo umuhimu wa kumualika mfalme wao,” alisema.

Aliwapongeza marais wastaafu, Jakaya Kikwete na Alhaj Ali Hassan Mwinyi kutokana na kushiriki kwao kikamilifu katika kukuza dini ya Kiislamu nchini.

Aidha, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo kuhakikisha kuwa hadi ya Ijumaa ijayo, taasisi ya Al-Hikma iliyoandaa mashindano hayo inapatiwa umiliki wa eneo la wazi lililopo Temeke kwa ajili ya kujenga hospitali.

Alisema badala ya eneo hilo kutumiwa na watu kupumzika na wengine kutupa taka, ni bora litumike kufanya mambo yenye masilahi kwa jamii.

“Lakini nitoe rai, mkalitumie kwa ajili ya kujenga hospitali kweli kwa sababu nitafuatilia nione ile nia njema ya taasisi hii ya kujenga kituo cha afya kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania inatimia,” alisema Magufuli.

Rais Magufuli aliipongeza taasisi hiyo akisema imeshajenga misikiti 50, visima 110, shule ya msingi moja, sekondari mbili na kusomesha yatima 400. Aliiomba ijenge msikiti wa 51 katika Wilaya ya Chato, Geita.

Alipopatiwa nafasi ya kusalimia, Mzee Mwinyi alisema kila Mtanzania aweke nia ya kumsaidia Rais Magufuli si kwa ajili ya kiongozi huyo binafsi, bali kwa maslahi ya nchi na kila mmoja.

Alisema nchi haikuwa na ndege leo ina ndege, ilikuwa na reli ya kusuasua leo ina reli ya fahari, ya kujivunia ndani ya miaka mitano.

“Ndani ya miaka mitano watu wameshikana wapo wengi hapa kwa nia moja na kitako chake ni juu ya usalama na umeona amani, ameshikilia mwenzetu huyu (Rais Magufuli) amani umoja na mshikamano, tumsaidieni,” alisema Mwinyi.

Awali, Kikwete alisema ujio wa Rais Magufuli katika mashindano hayo ni faraja kubwa hasa maneno aliyosema ya kusisitiza mshikamano baina ya Watanzania wa dini zote.

“Nakushukuru kwa ajili ya ahadi yako kwa Taasisi yetu ya Al-Hikma ambavyo inafanya mambo mazuri sana, wanafanya mambo makubwa sana, wametoa ombi kwako na wewe umeyasikia,” alisema Kikwete.

Uwanja wa Taifa wafurika

Mashindano hayo yaliyoanza saa mbili asubuhi, yalihudhuriwa na idadi kubwa ya waumini ambao walianza kumiminika uwanjani hapo tangu saa 12 asubuhi.

Hadi kufikia saa tatu asubuhi, uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 ulijaa hadi kwenye ngazi hivyo kuulazimu uongozi kuwapeleka waumini wengine katika uwanja wa jirani wa Uhuru kusikiliza matangazo ya mashindano hayo.

Kivutio kikubwa katika mashindano hayo kilikuwa ni mshiriki wa Tanzania, Sumayyah Juma Abdallah (12) ambaye alishika nafasi ya tano akiwa mshiriki pekee wa kike kati ya washiriki 20.

Zamu yake ilipofika, umati huo ulimshangilia kwa nguvu huku baadhi ya waumini wakionekana kumrekodi alipokuwa akisoma.

Alipokuwa akihutubia, Rais Magufuli alisema binti huyo ndiye aliyemvutia zaidi na alimzawadia Sh1 milioni baada ya kutangazwa mshindi wa tano na waandaaji kusema atazawadiwa Sh3 milioni.

Advertisement