Makonda atoa mwezi mmoja kuanza ujenzi Ufukwe Coco

Friday August 09 2019
makonda pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa mwezi mmoja kwa mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Meya, Benjamin Sitta  kuanza kuboresha ufukwe wa Coco Beach.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Agosti 9, 2019 alipotembelea ufukwe huo na kubainisha kuwa kuchelewa kwa ujenzi huo ni uzembe wa manispaa hiyo.

"Eneo hili lilikuwa lichukuliwe na mtu binafsi lakini limerudi kwa wananchi kwa ajili ya kulifanya kuwa eneo zuri la kupumzikia watu wote," amesema Makonda

Amesema Rais John Magufuli ameshatoa Sh14 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika, kudai kuwa kila siku watu wanakaa vikao.

“Awali kulikuwa na changamoto za kesi na kupelekea kutotekelezwa kwa mradi huu lakini zilishamalizika na fedha ipo,” amesema Makonda.

Amesema baada ya kufuatilia walielezwa kuwa mshauri ameacha mchoro ulioombewa fedha, kutengeneza mchoro mwingine wa zaidi  ya Sh40 bilioni.

Advertisement

"Tunatoa mwezi mmoja tutakuja kuangalia kama ujenzi umeanza,  hivyo tutarudisha fedha kwa katibu tawala na kutafuta mkandarasi mwingine,” amesema Makonda.

Alipotafutwa Kagurumjuli amesema hayo ni maelekezo yameshatolewa hawezi kuyapinga.

 


Advertisement