Mhandisi wa meli ajinyonga hadi kufa katikati ya safari

Unguja. Mhandisi msaidizi katika meli ya Mv Mapinduzi, Haji Abdalla Khatib (55) amefariki dunia baada ya kujinyonga wakati meli hiyo ilipokua inatoka Unguja kwenda Pemba.

Tukio hilo limetokea leo Jumatatu Julai 22, 2019, Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mustafa Aboud Jume amesema baada ya kupata taarifa hiyo walilazimika kusitisha safari na kuamuru meli hiyo irudi Unguja.

Amesema Khatib amejinyonga katika chumba cha Injini, sehemu aliyokuwa anafanyia kazi na kwamba, hadi sasa bado hawafahamu sababu za kujinyonga kwake.

“Marehemu alikuwa fundi umeme wa miaka mingi tangu enzi za meli ya ukombozi, hivyo ni mtu muhimu sana,” amesema.

Amesema pamoja na hayo, uchunguzi wa kifo hicho umefanyika na tayari jeshi la polisi linaanza kazi zake mara moja kwa lengo la kubaini sababu zilizomfanya injinia huyo kujitoa uhai wake.