Pochettino akataa kuvaa viatu vya Mourinho

Muktasari:

Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino amesema ana furaha kubaki Makao Makuu White Hart Lane na hana mpango wa kutua Manchester United.


London, England. Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino, amesema hana mpango  kujiunga na Manchester United.

Nyota huyo wa zamani wa Argentina, alisema hataki kuvaa viatu vya kocha wa Man United Jose Mourinho endapi atatimuliwa.

Pochettino alisema akili yake ni kuhakikisha Spurs inamaliza Ligi Kuu England ikiwa ndani ya nafasi nne za juu.

Taarifa zinadai Man United inamtazama Pochettino kama chaguo lao la kwanza endapo Mourinho ambaye amekuwa hana mwenendo mzuri ndani ya kikosi hicho, atafungishiwa virago Old Trafford.

“Tottenham imenipa thamani kama kocha, hiyo ni heshima kwangu. Nina furaha kuwa hapa kwasababu hata viongozi wangu wanathamini sana ninachokifanya.

“Pale ambapo (mwenyekiti) Daniel Levy aliponiongeza mkataba wa miaka mitano imeonyesha aliniamini na kuona tunaweza kufikia malengo ya klabu kwa pamoja, kwa hiyo siko tayari kuwaangusha, masikio yangu nimeziba kusikia nini nje kinaendelea,”alisema Pochettino.

Pochettino, alisema anaendelea kukijenga kikosi ili kuwa na nguvu kubwa kiushindani kulinganisha na Manchester City na Liverpool ambazo zinaonekana tishio katika kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligin Kuu msimu huu.

“Tunajaribu kuimarika, lakini namna yetu siyo sawa na timu nyingine, mpango wetu ni kuwa timu bora ya muda mrefu, tutaona muda tutakochukua,” alisema Muargentina huyo.