Breaking News

Serikali yafunguka utata wa kampuni ya kununua korosho

Monday February 11 2019

Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Nafaka

Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dk Hussein Mansoor(kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power Solutions ya nchini Kenya, Brian Mutembei wakibadilishana nyaraka baada ya kutiliana saini mkataba wa mauziano ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja, katika hafla iliyofanyika jijini Arusha Januari 30, mwaka huu. Picha na Vijimambo Blog 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya kusambaa kwa taarifa za kampuni ya Indo Power ya Kenya kutokuwa na uwezo wa kununua tani 100,000 za korosho nchini, Serikali imejibu na kusema haiangalii mambo mengine, bali uwezo wake wa kutekeleza masharti ya mkataba.

Januari 30, Serikali ilitangaza kumpata mteja atakayenunua tani 100,000 za korosho kwa Dola 180,000 za Marekani (zaidi ya Sh418 bilioni) na wiki mbili tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, gazeti la kila wiki la The East African limechapisha habari kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa mwaka 2016 haina historia ya kufanya miamala mikubwa kiasi hicho.

“Kampuni hii iliyojikita kwenye biashara ya kimataifa haina tovuti. Hata hivyo, taarifa zake za usajili zinaonyesha haina akaunti za benki, wanasheria wala katibu wa kampuni na haina wakaguzi wa hesabu,” limesema gazeti hilo.

Kwenye miamala iliyofanya tangu ianzishwe, The East African linasema Indo Power haijawahi kuwa na mkataba japo wa Dola 10 milioni na kwa maelezo ya kampuni husika, fedha za kufanikisha mkataba wake na Tanzania utafanikishwa na mkopo kutoka benki ya nje ya Kenya.

Hata hivyo, katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Joseph Buchweishaija aliiambia Mwananchi jana kuwa historia sio hoja ya msingi waliyoipa kipaumbele.

“Inayouza korosho ni Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko, jukumu letu lilikuwa kufanikisha biashara tu. Unachoangalia ni uwezo wa mnunuzi kulipa bei anayoitaka muuzaji yanayobaki wanaelewana wao,” alisema katibu mkuu huyo.

Advertisement

Nyaraka za usajili wa kampuni hiyo, The East African linasema zinaonyesha ina makao makuu yake katika Mji wa Thika, nje kidogo ya Jiji la Nairobi katika jengo la Indo House ambalo lilipotafutwa halikupatikana.

Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Indo Power, Brian Mutembei ameliambia gazeti hilo kuwa wamejikita kwenye biashara ya mazao ikijihusisha zaidi na kahawa, kuku, uingizaji wa pombe uuzaji jumla wa bidhaa za mafuta na haijawahi kufanya biashara ya korosho.

Profesa Buchweishaija alisema “inawezekana ikawa haijawahi kufanya biashara hii lakini imeona fursa ikaamua kuitumia. Sote tunafahamu hata matajiri wakubwa hawana fedha, huzitoa benki. Hawa nao wamechukua mkopo benki. Watanzania nasi tunatakiwa kuzitumia fursa zinazojitokeza kila inapobidi.”

Kutokana na uchanga wake kufanikisha mkataba huo, Mutembei ameliambia The East African kuwa hati ya muamana (letter of credit) ya mkataba wa Indo Power na bodi ya mazao mchanganyiko imetolewa na benki ya nje ya Kenya.

“Tumeshapeleka hati ya malipo ya fedha zote zinazohitajika kwa Serikali ya Tanzania. Imetolewa na benki ya nje ambayo siwezi kuitaja kutokana na sababu za kibiashara,” amenukuliwa Mutembei na gazeti hilo.

Kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa mauzo ya korosho uliofanywa kati ya mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dk Hussein Mansour na Mutembei, walikuwapo pia Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga.

Pamoja na hao, alikuwepo Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu ambaye aliliambia gazeti hilo kuwa ni wajibu wake kufanikisha biashara kati ya kampuni za Kenya zinazotaka kuwekeza au kufanya biashara na Tanzania.

Bila kujali uwezo wa kampuni hiyo, malipo ya mkataba uliosainiwa, taarifa zinasema yanatarajiwa kufanywa kwenye akaunti iliyopo BoT ndani ya wiki moja baada ya kuafikiwa kwa makubaliano hayo.

Hata hivyo, alipotafutwa Gavana Luoga kujua kama malipo hayo yamefanyika na kupata taarifa za ziada alisema bodi ya nafaka itakuwa inafahamu zaidi kuliko yeye.

“Wasiliana nao,” alisema kwa kifupi kupitia kwa msaidizi wake.

Alipoulizwa Dk Mansoor hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema, “kuna mambo yanaendelea hivyo siwezi kusema lolote kwa sasa mpaka yatakapokamilika, naomba uwe na subira.”

Alipoulizwa kama mambo yote muhimu yalizingatiwa kabla ya kuingia mkataba na kampuni hiyo, alisema: “Wizara ya Viwanda ndio iliyoufanikisha. Wao ndio wataalamu, hata kama sisi tunasaini wao wanatuwezesha.”

Advertisement