Spika Job Ndugai: Nilitumwa Misri na Rais Magufuli

Tuesday June 25 2019
pic ndugaii

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema hakwenda Misri yeye kama yeye, bali alitumwa na Rais John Magufuli kwenda kuiwakilisha nchi.

Spika Ndugai ameyasema hayo leo Jumanne Juni 25, 2019 alipokuwa akifafanua kauli ya aliyemuita kiongozi mmoja mmoja wa Serikali kuwatuhumu baadhi ya wabunge kuwa wamewalaumu wachezaji na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).

Amesema: “Mimi nimetumwa Misri na Rais, halafu anakuja mkuu wa mkoa mmoja ananisumbua, siwezi kusumbuliwa na mkuu wa mkoa mmoja.”

Amesema kiongozi huyo wa Serikali amezungumza maneno yasiyofaa kuhusu Bunge la Tanzania na wabunge na kumdanganya hadharani Rais Magufuli, kuwa wawakilishi hao wa wananchi wamewadhihaki wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Spika huyo amesema hawezi kusumbuliwa na mkuu wa mkoa mmoja, kwa kuwa anatambua nini anakifanya.

Amesema kati ya wabunge waliokwenda Misri ambako timu ya Taifa inashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), hakuna aliyemlaumu mchezaji yeyote wala kuisema vibaya timu hiyo.

Advertisement

 “Hayo ni mawazo ya mtu ambaye kidogo ndiyo hivyo. Ni bahati mbaya sana tuna viongozi wa Serikali wanadiriki kumdanganya Rais hadharani, kiongozi wa Serikali unapoongea mbele ya rais jipange uongea ukweli mtupu wa mwenyezi Mungu, usisingizie wala kumuonea mtu hatufanyi hivyo.”

Mapema leo asubuhi, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza katika ufunguzi wa Mradi wa Gesi, Kigamboni jijini humo, alisema ameshangaa wadau mbalimbali ambao wameizungumzia vibaya timu hiyo baada ya kupoteza mbele ya Senegal.

“Nimeumizwa na matokeo ya Taifa Stars, lakini nimeumizwa zaidi kwa watu kuwabeza wachezaji wetu ambao wametubeba Watanzania ambao ndani ya miaka 30, haikuwezekana lakini wao wamepambana mpaka tupo Afcon leo hii," alisema Makonda

Makonda alisema alizungumza na wachezaji hao pamoja na nahodha Mbwana Samatta na wamemuhakikishia kwamba watafanya vizuri katika mchezo wao dhidi ya Kenya.

"Sisi Afrika Mashariki tunajuana vizuri kwahiyo Mhesimiwa Rais wala usiwe na wasiwasi tutafanya vizuri katika mchezo huu ambao tunahitaji ushindi na wachezaji wapo vizuri," alisema Makonda.

Aliongeza iwapo Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli aweze kutoa neno lolote la kuwapa moyo kuelekea katika mchezo ujao.

Tanzania itacheza na Kenya Alhamisi mchezo utakaopigwa saa kumi na moja jioni.

Advertisement