Takukuru watakiwa kuwakamata wagombea CCM

Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally (katikati) akimsikiliza mzee wa kimila wa jamii ya wamasai Laigwanan John Lesiria, baada ya kukabidhiwa ng'ombe, mbuzi na mafuta ya alizeti Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, leo.Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amewaagiza watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata wagombea wa chama hicho tawala watakaojihusisha na vitendo vya kutoa rushwa

Kiteto. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amewaagiza watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata wagombea wa chama hicho tawala watakaojihusisha na vitendo vya kutoa rushwa.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 12, 2019 wakati akizungumza na wanachama na viongozi wa chama hicho kwenye kikao kilichofanyika katika mji mdogo wa Kibaya wilayani Kiteto.

Dk Bashiru aliyepo mkoani Manyara kwa ziara ya siku mbili amebainisha kuwa Takukuru wanatakiwa kuwakamata wagombea wote watakaonunua uongozi kwa kutoa rushwa bila kujali chama anachotoka hata kama ni wa CCM.

Amesema wanataka viongozi watakaochaguliwa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019  waibuke na ushindi kutokana na uadilifu wao, si kununua uongozi.

"Hatutaki kuona viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji wanapatikana kwa kutoa rushwa, Takukuru wakamateni wote,” amesema Dk Bashiru.

Amesema wanaotoa rushwa kwenye uchaguzi ni viongozi wasiojiamini, wanapaswa kubadilika na kufuata taratibu na kanuni.