Vita ya CAG, Bunge iko hapa

Spika wa Bunge, Job Ndugai 

Muktasari:

Taasisi hizo mbili zimeingia katika mgogoro baada ya Spika Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu kauli yake kuwa chombo hicho cha kutunga sheria ni dhaifu katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kasoro zinazobainishwa kwenye ripoti za ukaguzi.

 


Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikishuhudia mzozo kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Profesa Mussa Assad, majukumu ya kikatiba ya taasisi hizo mbili yanaweza kuwa tatizo wakati wa kumuhoji Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Mwananchi inakuchambulia.

Ndugai amemtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge Januari 21, 2019 kujieleza kuhusu kauli yake aliyoitoa wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa jijini New York kuwa chombo hicho cha kutunga sheria hakitekelezi wajibu wake ipasavyo na kwamba anaamini udhaifu huo utarekebishwa karibuni.

 

Ndugai anahisi kauli hiyo inadhalilisha Bunge na hivyo kumtaka Profesa Assad kwenda kwa hiari yake mbele ya kamati hiyo kujieleza na asipofanya hivyo, atapelekwa akiwa amefungwa pingu.

 

Wito huo unaweza kuibua ushindani mkali wa kisheria hasa kutokana na jinsi Katiba inavyotoa mamlaka kwa taasisi hizo mbili na majukumu yao. Tafsiri ya mamlaka na majukumu hayo inaweza kuibua ushindani mkali wa hoja.

Ibara ya 143 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza nafasi ya CAG na kazi zake, wakati kifungu kidogo cha pili kinaeleza majukumu ya CAG kuwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba matumizi ya fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali lazima yaidhinishwe na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya Katiba.

“Iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe,” inasema Katiba.

Kazi nyingine ni kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa, zitokane na fedha zilizomo katika mfuko mkuu wa hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, na ambazo zimetumika, zimetumiwa kwa ajili ya shughuli zilizokusudiwa.

“Angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na katibu wa Bunge,” inaeleza.

Kifungu kidogo cha (4) kinaeleza mchakato wa CAG kupeleka taarifa yake kwa Rais kila taarifa atakayotoa.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho,” inaeleza.

Kifungu kidogo cha tano kinaeleza madaraka zaidi ya CAG kuwa ni pamoja na kutekeleza kazi na shughuli nyingine kwa mujibu wa sheria kuhusu hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Kifungu kidogo cha sita kinasema: “Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya 2, 3 na 4 ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali. 

“Lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.”

Suala hilo linaweza kuibua utata, lakini shauri litajikita katika hoja kama kauli aliyoitoa CAG ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake.

Katiba pia inaeleza majukumu ya Bunge katika ibara ya 63(2), ikisema kuwa ndicho chombo kikuu kitakachokuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hapa ndipo Bunge linapopata madaraka ya kumhoji yeyote na hivyo kujitungia kanuni ambazo zinamlazimisha yeyote kufika mbele ya kamati hiyo ya maadili, ambayo inafanya kazi kama mahakama.

Katika muhtasari wa kila ripoti anayotoa, CAG huwa anaeleze utekelezaji wa mapendekezo aliyotoa katika ripoti iliyopita na mara kadhaa ameonyesha kuwepo kwa udhaifu katika utekelezaji wake.

Hivi karibuni alipohojiwa kuhusu nakisi ya Sh1.5 trilioni ambayo alieleza katika ripoti yake kuwa haikukaguliwa, CAG alisema hilo si jukumu lake na kutaka Bunge la Jamhuri ya Muungano lihoji suala hilo.

Jitihada za Serikali kumtuma bungeni naibu Waziri wa Fedha kutoa maelezo kuhusu fedha hizo, hazikufanikiwa kutokana na wabunge wengi kutoridhishwa na maelezo hayo.