Wachambua hukumu iliyowaachia huru Mbowe, Matiko

Muktasari:

  • Katika hukumu aliyoitoa Jaji Rumanyika aliamuru waachiwe huru na dhamana yao iendelee wakati wakiendelea na kesi yao ya msingi baada ya kujiridhisha kuwa Mahakama ya Kisutu haikuzingatia matakwa ya sheria kuwafutia dhamana huku akisisitiza umuhimu wa dhamana kwa mshtakiwa.

Dar es Salaam. Hukumu ya rufaa ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Esther Matiko imewaibua mawakili mbalimbali wakimpongeza Jaji Sam Rumanyika aliyeitoa.

Baadhi ya mawakili waliohojiwa na Mwananchi wameielezea hukumu hiyo kuwa ni ya kihistoria na imeweka mwongozo kwa Mahakama za chini katika kushughulikia masuala ya dhamana za washtakiwa.

Pia, wamemwelezea Rumanyika kuwa ni mmoja wa majaji wanaotanguliza haki kwa misingi ya sheria, huku wakikumbuka kazi zake nyingine za nyuma kama ya uamuzi wa kuzifuta kesi nyingi za mauaji kwa pamoja kutokana na kukaa mahakamani muda mrefu bila upelelezi kukamilika.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na Matiko ambaye pia ni mbunge wa Tarime Mjini, walikuwa mahabusu katika Gereza la Segerea walikokaa kwa siku 104 baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Hata hivyo, juzi Jaji Rumanyika katika hukumu yake aliyotoa kutokana na rufaa ya Mbowe na Matiko kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu, alitengua uamuzi wa kuwafutia dhamana.

Jaji Rumanyika katika hukumu hiyo aliamuru waachiwe huru na dhamana yao iendelee wakati wakiendelea na kesi yao ya msingi baada ya kujiridhisha kuwa Mahakama ya Kisutu haikuzingatia matakwa ya sheria kuwafutia dhamana huku akisisitiza umuhimu wa dhamana kwa mshtakiwa.

Pia, aliainisha mambo tisa ambayo mahakimu na majaji wanapaswa kuyazingatia wanaposhughulikia dhamana, iwe ni kumpa, kumnyima au kumfutia mshtakiwa.

Akizungumzia hukumu hiyo, Wakili wa kujitegemea, Abdon Rwegasira alisema ni ya kihistoria na imeweka mwongozo wa msingi kwa mahakama za chini kuhusu dhamana.

Wakili Rwegasira alisema ingawa hajawahi kufanya kazi na Jaji Rumanyika, lakini anamfahamu kupitia kazi zake anazozifanya kila siku.

“Kwa hukumu hii, ametoa uamuzi ambao ninadhani ni wa haki na utakuwa mwongozo kwa mahakama za chini,” alisema Rwegasira.

Wakili Juma Nassoro pamoja na Wakili Daimu Halfani walikumbuka wakati Jaji Rumanyika akiwa Jaji Mfawidhi Tabora alivyokusanya kesi nyingi za mauaji katika mahakama za chini zilizokuwa zimekaa miaka mingi zikiahirishwa kwa sababu ya upelelezi kutokukamilika, akazipitia na kuzifuta zote na washtakiwa wakaachiwa.

“Japo DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) alikata rufaa Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Rufani ikaufuta uamuzi wake huo, lakini yeye kama Jaji wa Mahakama Kuu alikuwa amefanya kazi yake.

Wakili Flaviana Charles alisisitiza hukumu hiyo imeweka msingi wa Katiba kuwa mtu hatachukuliwa kama mhalifu hadi kosa lake litakapothibitika na Mahakama ikamtia hatiani.

Wakili Nyaronyo Kicheere alisema hukumu hiyo inatakiwa ifuatwe na Mahakama Kuu yenyewe pamoja na mahakama zote za chini

“Sisi mawakili tunaifurahia sana kwa sababu imeweka msimamo ambao hautakiukwa na Mahakama za chini. Sababu alizozitoa ziko kama tisa hivi, zitawaongoza mahakimu katika kutoa au kunyima dhamana,” alisema Kicheere.

Mwenyekiti Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mkoa wa Kilimanjaro, David Shilatu alisema hukumu hiyo ya haina jipya kwa kuwa huo ndiyo msimamo wa sheria na Katiba.

“Kilichofurahisha katika hukumu hii ni hizo kanuni ambazo Jaji Rumanyika amezi ‘drive’, ambazo ni wazi kwamba sasa hivi zinakuwa sheria kwa Mahakama zote za chini kwenda mbele juu ya namna gani suala la dhamana linapaswa kushughulikiwa kwa makosa yote yenye kudhaminika,” alisema.

Nyongeza na Daniel Mjema na Elias Msuya