Wapinzani Tanzania waja na bajeti ya Sh 29 trilioni, vipaumbele vitano

Mbunge wa Momba, David Silinde akiwasilisha bungeni maoni ya kambi ya upinzani kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2019/20 pamoja na mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewasilisha bajeti yake mbadala mwaka 2019/2020 ya Sh29 trilioni yenye vipaumbele vitano ambavyo ni elimu, kilimo, viwanda, maji na afya

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania imewasilisha bajeti yake mbadala mwaka 2019/2020 ya mapato na matumizi ya Sh 29 trilioni yenye vipaumbele vitano.

Bajeti hiyo imewasilishwa leo Jumatatu Juni 17, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri kivuli wa Fedha, David Silinde ambaye kabla ya kuanza kusoma hotuba hiyo, alitakiwa na naibu Spika, Dk Tulia Ackson kutosoma baadhi ya maneno  kwa maelezo kuwa yameondolewa.

Alhamisi iliyopita Juni 13, 2019 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwasilisha  bajeti kuu ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni, huku Sh12. 2 trilioni zikiwa kwa ajili ya maendeleo.

Silinde ambaye pia ni Mbunge wa Momba (Chadema) amesema katika bajeti hiyo mbadala, Sh7 trilioni ni kwa ajili ya deni la Taifa, Sh6.6 trilioni sawa na asilimia 23 ya bajeti yote kwa ajili ya mishahara.

“Matumizi mengineyo ni  Sh2 trilioni, matumizi ya kawaida Sh15.7 trilioni. Matumizi ya maendeleo ni Sh13 trilioni ambazo ni fedha za ndani na nje pia,” amesema Silinde.

Ametaja vipaumbele na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya utekelezaji ni elimu (Sh4.3 trilioni), kilimo (Sh5.8 trilioni), viwanda (Sh4.3 trilioni), maji (Sh2.9 trilioni) na afya (Sh2.9 trilioni).

Silinde amesema Sh8.7 trilioni zitakuwa kwa ajili ya utekelezaji wa mambo mengineyo.