Wapinzani watema nyongo Lowassa kuhama wamchambua

Dar/Moshi. Wabunge na makada wa vyama vya upinzani wamekosoa hatua ya Edward Lowassa kujitoa Chadema na kurudi CCM alikokuita “nyumbani”.

Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, alitangaza uamuzi huo juzi mbele ya viongozi mbalimbali wa CCM waliokusanyika ofisi ndogo za chama hicho zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam.

Karibu viongozi wote wa juu, wakiongozwa na mwenyekiti wao, John Magufuli walikuwepo kwenye ofisi hizo na Lowassa alipelekwa na Rostam Aziz, mbunge wa zamani wa Igunga aliyetangaza kustaafu siasa wakati CCM ikiendesha mkakati wa “kujivua gamba”.

“Bwana Yesu asifiwe, salaam alleikum. Sina mengi ya kusema; nimerudi nyumbani,” yalikuwa maneno machache ya Lowassa aliyotoa mbele ya umati wa wanachama nje ya ofisi hizo.

Lowassa alipambana vikali na Rais Magufuli kuwania urais mwaka 2015 akiwakilisha Chadema na vyama vilivyounda Ukawa, katika uchaguzi uliokuwa na msisimko na ushindani mkali. Aliviwezesha vyama vya upinzani kuongeza idadi ya madiwani na wabunge.

Lakini baadhi ya wabunge na makada wa vyama vya upinzani waliozungumza na Mwananchi wameponda uamuzi wake wa kurejea CCM.

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema kuondoka kwake hakuna athari yoyote kwenye chama kwa sababu Chadema ni chama imara na hata Lowassa anajua.

Mzigo wa kumuepusha Lowassa na kashfa za ufisadi, hasa mradi tata wa umeme wa Richmond, sasa umehamia CCM.

“Viongozi waandamizi wa CCM walikuwa wakipita kumnadi (Lowassa kuwa) ni fisadi, wakitumia majukwaa ya kisiasa. Itawalazimu kutumia majukwaa hayohayo kumsafisha,” alisema Meya Jacob, ambaye ni diwani wa Ubungo.

“Hawatakuwa tena na ajenda ya (kwamba) ‘Chadema wana mafisadi’, kwa sababu ilikuwa ndiyo ajenda yao kuu. Sasa itabadilika na kuiimarisha zaidi Chadema na wao watabadili msemo.”

Jacob pia alisema Lowasa hajaondoka kipindi sahihi. Alisema alipaswa asubiri kwanza viongozi wa chama, akiwamo mwenyekiti Freeman Mbowe, ambaye yuko mahabusu, atoke na Tundu Lissu anayejiuguza nchini Ubelgiji, arejee kwa sababu walimpokea kwa heshima.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alikwenda mbali akidai kuondoka kwa Lowassa na familia yake kunatokana na kesi inayomkabili mkwewe, kukomboa shamba lake linaloshikiliwa Tanga na shamba lake la mifugo la Dodoma.

Kwa kusema mkwewe, alikuwa akimaanisha Sioi Sumari, ambaye pamoja na mfanyakazi mwenzake wa Stanbic, Shose Sinare, na kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya walifikishwa mahakamani na Takukuru Aprili 1, 2016 wakituhumiwa kwa kula njama na kujipatia fedha kwa udanganyifu, kughushi na utakatishaji wa fedha.

Wote wako mahabusu kwa kuwa mashtaka yao hayana dhamana.

Mbali na hilo, Lema amemfananisha Lowassa na kiongozi anayeweza kukubaliana na ukandamizaji kwa maslahi yake binafsi.

“Mtu huyu alitaka kuwa Rais, hali ya kisiasa ilivyo sasa watu wapo magerezani, wanapata misukosuko ya kibiashara, hawana cha kuipa CCM ili wapate ahueni, lakini yeye kwa sababu anacho cha kuwapa CCM ili apate amani. Hajaona gharama ya kufanya hivyo,” alisema mbunge huyo.

“Chadema imepata baraka kuondokewa na mtu kama huyu. Alikuja kwa ajili ya kutaka urais na si mabadiliko aliyokuwa akiyanadi. Nchi inataka demokrasia, katiba mpya, sheria mpya na inakabiliwa na ubanwaji wa vyombo vya habari.

“Mwanasiasa yeyote makini hawezi kuungana na CCM bali atapingana nayo kwa maslahi mapana ya nchi.”

Alisema hawamshangai kwa kuwa walimuona hivyo baada ya kumalizika kwa kampeni za uchaguzi mkuu. Alisema mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipigwa risasi na mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alifungwa lakini Lowassa hakuandika wala kusema chochote kulaani.

“Utakumbuka mwenyekiti Freeman Mbowe wakati yupo ndani, Lowassa alikwenda kwenye mdahalo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako mgeni rasmi alikuwa Rais Magufuli,” alisema.

“Huyu hakuwa mwenzetu, alikuja kwa ajili ya maslahi yake. Ukiwa na kiongozi kama huyu tena kwenye nafasi ya juu, akiondoka ni kuvuja kwa pakacha, (hivyo inakuwa) nafuu ya mchukuzi.”

Kuhusu mwelekeo wa siasa za Lowassa, Lema alisema amefika mwisho atakachopewa na CCM ni kijana wake Fred kupewa ubunge na binti yake kurudishwa kazini kwenye taasisi moja kubwa ya kifedha.

“Ninawajua vizuri hawa. Nikiamua nimuanike huyu mzee atakuwa hapiti mitaani watu watamuona wa ajabu sana. Mbinafsi, ana roho mbaya na yupo radhi kufanya lolote hata kama lina madhara kwa wengine,”alisema.

Afadhali ameondoka

Mwingine aliyeona ahueni Lowassa kuondoka ni mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe ambaye alisema sasa “roho yake imetulia”.

Alisema Lowassa alikuwa na hali ngumu mbele ya familia kutokana na mali zake zinavyobanwa.

“Kila mwanasiasa ana vitu anavyoona vya maana kwake. (Kwa) Lowassa mali ni kipaumbele na si misukosuko. Aondoke atuachie wenyewe,” alisema Rugwe.

“Lowassa alikuja kwa ajili ya urais, ameukosa. Akae kusubiri nini” Acha aende huko kwao. Kwanza hata alivyo hawezi mapambano nyinyi wenyewe mnamuona.”

Alisema amejipambanua vema sasa kuliko wakati ule alipokuwa akihubiri mabadiliko ilhali siyo asili yake.

Kwa upande wa mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema wamekubaliana kuacha kumjadili kiongozi huyo na kuacha wananchi waamue.

“Tumeamua kuwa low profile (kutulia). Alichoandika katibu mkuu kinatosha. Tunawaachia wananchi waamue,” alisema Mchungaji Msigwa.

Mchungaji Msigwa anaungana na mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche aliyesema “kwa sasa tuko busy kujenga chama kuanzia ngazi za chini”.

Akijibu swali la Mwananchi kuwa kuondoka kwake kunaweza kuwa pigo, Heche ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti alisema: “Haiwezekani, Chadema ni kubwa kuliko mtu, ndio maana alikuja Chadema na hakwenda chama kingine.”

Haturudi nyuma

Naye mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, akizungumza kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikokuwa amelazwa, alisema japo ameondoka, “wataendelea na harakati za siasa mpaka kieleweke”, ingawa aliheshimu mchango wake.

“Lowassa alikuja kwetu baada ya kudharauliwa, kubezwa na kukataliwa na chama ambacho alikitumikia kwa muda mrefu,” alisema Selasini.

“Tulimchukua tukijua alikuwa na mchango katika kukuza demokrasia ya nchi yetu. Ni dhahiri upo mchango wake ambao aliongeza katika chama chetu na hatuwezi kuudharau,” alisema Selasini.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyesema: “Lowassa ni mtu mzima anajua anachokifanya. Lakini wakati anajiunga Chadema ilikuwa imara na huku Kaskazini ilikuwa ya upinzani. Hatuumii ila inahuzunisha.”

Wakati Lowassa akitimkia Chadema, alifuatana na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Dk Makongoro Mahanga akiwa naibu waziri wa kazi na ajira ambao wote walisema alichokifanya ni uamuzi wake binafsi.