Kutekwa Mo Dewji kulivyobadili upepo nchini

Muktasari:

  • Baada ya mfanyabiashara Mo Dewji kutekwa alfajiri ya Oktoba 11, uzito wa tukio hilo ulifunika matukio mengine ya kijamii ikiwamo uchaguzi mdogo wa Liwale, hamahama ya wabunge wa upinzani, ziara mbalimbali za viongozi nchini pamoja na mambo mengine.


 

Dar es Salaam. Hazikuwa siku tisa za hofu kwa familia tu, tukio la kutekwa hadi kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ lilifanya matukio mengine yafunikwe kwa namna moja au nyingine nchini.

Mo alitekwa saa 11: 30 alfajiri ya Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi, lakini akapatikana saa 7:30 usiku wa Oktoba 20, baada ya kutelekezwa na watekaji hao katika viwanja vya klabu ya Gymkhana.

Siku hizo tisa za kutekwa kwa bilionea huyo kijana barani Afrika kulileta hekaheka kiasi cha kufunika matukio mengine yaliyokuwa yanatokea kutokana na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ndani na nje kujadili suala hilo kwa muda mwingi zaidi.

Vyombo vingi vya habari vya kimataifa kama CNN, BBC, Al Jazeera na vinginevyo viliripoti tukio hilo huku mikutano ya waandishi wa habari na polisi ikifanyika mara kwa mara nchini.

Si tu vyombo vya habari, tukio hilo liliwaibua vigogo kadhaa serikalini kuanzia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), viongozi wa dini na taasisi mbalimbali ambao kwa nyakati tofauti ama walizungumzia jitihada zinazofanywa kumtafuta au kutoa wito wa kutaka apatikane.

Kutokana na uzito wa suala hilo la kutekwa kwa bilionea huyo mwenye utajiri wa Sh3.5 trilioni, matukio mengine nchini ‘yalifunikwa’ kwa sababu mjadala mkubwa katika jamii na vyombo vya habari ulikuwa ni Mo Dewji.

Baadhi ya matukio yaliyojikuta yamekumbwa au kufunikwa na kutekwa kwa Mo ni uchaguzi mdogo wa ubunge wa Liwale, hamahama ya wabunge, makongamano ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na ziara za viongozi mbalimbali nchini.

Ziara mbalimbali za viongozi hasa mawaziri zilijikuta zimefunikwa na hata matukio waliyoyafanya kutofahamika kwa sababu ya tukio hilo la Mo Dewji.

Hata siasa ziliathirika kwani ziara na mikutano ya viongozi wa chama tawala na vyama vya upinzani ilijikuta ‘ikififishwa’ na tukio hilo la kutekwa kwa mwekezaji huyo wa klabu ya Simba.

Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana kuwajadili wabunge wake, Anthony Komu (Moshi Vijijini) na Saed Kubenea (Ubungo) juu ya tuhuma za kutaka ‘kumdhuru’ Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kwa namna mmoja au nyingine, mjadala wake ulifunikwa na suala la Mo, ambaye kwa mara ya kwanza alionekana hadharani Ijumaa iliyopita aliposhiriki Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Shia Ithnasheri.

Matukio mengine kama ajali za magari, madhara ya hali ya hewa na mvua na matukio mengine ya aina hiyo kwa namna mmoja au nyingine yalikosa mvuto kwa muda.

Mitazamo ya wachambuzi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana na mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa walizungumzia kwa mitazamo tofauti juu ya suala la Mo kufunika mengine.

“Mo ni mtu mkubwa katika siasa za nchi hii na kwenye medani za michezo, hivyo kujadiliwa zaidi na kuandikwa kwenye vyombo vya habari ni sahihi,” alisema Dk Bana.

“(Mfanyabiashara huyo) ni zaidi ya wabunge kumi na Mo ni zaidi ya vyama vitano vya siasa vya upinzani. Tukio lake la kutekwa eneo ambalo kuna walinzi na kupatikana kwake ni sahihi kujadiliwa zaidi,” alisema Dk Bana.

Aliongeza, “Ingawa sote ni binadamu lakini maisha ya Mo kila mtu anayajua. Mo Dewji ni zaidi ya jina, ni mtu mwenye kauli na matendo yake hakuna ubishi kuwa anastahili kuzua mjadala.”

Ole Ngurumwa alisema vyombo vya habari ndivyo vinavyoweza kuendesha mijadala, iwe kwenye jamii au makundi ya mitandao na ndicho kilichotokea kwa matukio mengine.

“Watanzania huwa hatuna utamaduni wa kufuatilia mambo yanayotuhusu na ndiyo maana viongozi utakuta wanatuanzishia mambo mapya,” alisema Ngurumwa

“Tatizo hatuna wasemaji, wanaopaswa kusemea mambo mbalimbali. Wasemaji wamekuwa wachache, si vyombo vya habari, wanaharakati, wanasiasa, wasomi, wote hawaongei kama zamani na hii inaweza kuwa sababu.”

Uchaguzi mdogo wa ubunge wa Liwale uliofanyika Oktoba 13 na Zuberi Kuchauka wa CCM kuibuka mshindi ulionekana kutokuwa na hamasa kwani wananchi waliendelea kujadili kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

Oktoba 12, siku moja baada ya Mo kutekwa, ulifanyika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Nyerere uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mdahalo huo uliohudhuriwa viongozi mbalimbali wa Serikali, kisiasa na wasomi, ulishuhudia katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ‘wakitoana jasho.’

Wakati Lowassa akisema wananchi wanajengewa hofu na chuki nyakati za uchaguzi ili wawachague wasiowataka, Dk Bashiru alisema wezi wa mali za umma ndiyo wenye hofu.

Dk Bashiru, akiwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere alizungumzia kuwachukulia hatua wanachama ambao wanakichafua chama hicho mitandaoni.

Tofauti na huko nyuma, kilichosemwa na Dk Bashiru na Lowassa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema mwaka 2015, hakikuzima mjadala wa kutekwa kwa Mo, ni jambo lililopita kama upepo.

Pamoja na mengine, Chadema ilikutana kuwajadili Kubenea na Komu ambao sauti yao ilisikika wakipanga mipango dhidi ya Meya wa Ubungo, Jacob. Sakata hilo lilimalizika kwa wabunge hao kukiri kuwa sauti ni zao na kuomba radhi hadharani.

Wimbi la hamahama ya madiwani na wabunge wa upinzani ilishuhudiwa mbunge wa kwanza mwanamke wa jimbo, Pauline Gekul wa Babati Mjini akijiuzulu lakini kama ilivyokuwa kwenye matukio mengine nalo lilipita pasi na kishindo.

Kama ilivyo kwa matukio hayo, mawaziri mbalimbali wa Serikali walifanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini, lakini matukio yao ni kama yalifunikwa na suala hilo la kutekwa kwa Mo.