HEKAYA ZA MLEVI: “Lekebisheni ruga zenu”!!!???

Rubani mmoja alipata ajali ya ndege ndogo na kuangukia kwenye kijiji asichokielewa. Alipoteza fahamu kwa dakika kadhaa, alipozinduka hakujua alizimia muda gani na wakati ule yalikuwa majira gani.

Alimwuliza mmoja wa wawindaji: “Hapa wapi?” akajibiwa “Sisi wageni”. Akatazama saa yake iliyoharibika vibaya na kuuliza tena: “Ni saa ngapi hivi sasa?” Wakamjibu “Hatujui”.

Akatazama jua angani na kugundua miale yake ilikuwa finyu. Lakini kwa kuwa hakujua wapi Magharibi, wapi Mashariki, hakuelewa yalikuwa mawio au machweo. Akauliza: “Kwani jua linaelekea wapi?” akajibiwa “Tushakwambia sisi wageni, hatujui safari zake eneo hili!”

Kwa haraka unaweza kuona hawa wote walikuwa machizi. Ni mtu gani asiyejua alipo? Hata kama hajui jina la nchi ile, ndio asijue kuwa yupo jangwani au nyikani? Yaani walishindwa hata kujua kuwa walikuwa ardhini?

Jambo lingine eti unauliza jua linaelekea wapi! Tangu lini jua likatembea? Inawezekana wawindaji walitoa jibu sahihi la kutojua kumbe sehemu zingine jua linasafiri. Kwao dunia ndiyo inayosafiri kulizunguka jua.

Ingekuwa jua linatoka lilipo kwenda kwingine kusingekuwa na ulimwengu. Maana lenyewe lipo katikati ya sayari zote ikiwamo dunia. Ingelikuwa kinyume chake basi kusingekuwa na sayari iliyosalia sehemu yake. Zile ambazo lingezisogelea zingeungua, na ambazo zingeachwa mbali zingeporomoka kwa ukosefu wa nguvu ya uvutano.

Maswali yasiyojibika yapo kila mahala. Tatizo si uelewa, bali matumizi mabovu ya lugha. Utamsikia mtu akimwuliza mwenzie “Eti leo lini?” Mtu makini lazima ujiulize huyu anauliza nini. Kwa sababu ni lazima iwe leo. Haiwezi asilani kuwa jana au kesho.

Nikiamua kuainisha utumbo unaoongeleka mtaani, hakika magazeti hayatatosha kuubeba. Nitakumbusha machache ambayo huwa naona hata aibu kumrekebisha mkoseaji.

Wakati mwingine nikisoma maandiko ya mtandaoni au kusikiliza nyimbo za kileo sioni tofauti na maandiko ya kitabu cha “Aliyeonja pepo”. Tofauti ni kwamba mwandishi wa kitabu hicho aliandika Kiswahili kwa ufasaha, ila alibadilisha lugha na kuiita “Lugha ya peponi”.

Aliandika: “Petum lachaku, laaki kiataba laasipoku etumwachi” akimaanisha “Tumpe chakula, akila atabaki asipokula tumwachie”. Neno la mwisho aliliweka mwanzo makusudi. Yule aliyeonja pepo akaishtukia dili, alipopewa chakula akagoma na kuachiliwa arudi duniani.

Nimekumbuka wimbo wa zamani unaoimbwa “Umetoroka bila kuniaga.” Nikamfikiria mtu anayetoroka baada ya kuaga ni yupi? Sawa na kusema “Umeniibia bila ridhaa yangu? Kutoroka ni kuondoka bila ruhusa, kuiba ni kutwaa mali bila ruhusa.

Nani hajawahi kumsikia mtu akimwambia mtoto aliye ndani “Toka nje!” Aende wapi sasa? Kinyume cha kutoka ni kuingia, hivyo angeimalizia sentensi angesema “Toka nje uingie ndani”.

Mwingine anayefanana na huyo hajui tofauti ya kwenda na kuondoka. Utamkuta kituo cha basi Buza na kumwuliza “Vipi tena?”Atakujibu “Naondoka Mbagala” badala ya kusema “Naenda Mbagala”. Unaondokaje mahala usipokuwepo?

Madudu twayakuta hata katika sentensi rahisi. Wapo mabingwa wa SwaEng au Kiswa-Kinge wanaoongea sentensi za mseto wa Kiswahili na Kingereza, hupachika neno juu ya neno hilo hilo na kusababisha sentensi mbili kupandiana au kugeuka hewa. Upande huu waheshimiwa huenda wanaongoza kuboronga. Kawashindisha kutwa ukumbini, MC wake ataziba mapengo ya muda akirudia kusoma ratiba mara ya nne: “Mheshimiwa atapitia barabara ya Kilwa Road.”

Ebo! Kwani Barabara ya Kilwa si ndio Kilwa Road? Au alitaka kusema “Service Road ya Kilwa Road”? Halafu kama haitoshi, mheshimiwa ataanza hotuba kwa kusema: “Kwa niaba yangu na kwa niaba ya uongozi…”

Huyu naye amekula nini asubuhi? Unawezaje kusema kwa niaba yako wakati wewe mwenyewe tunakuona unaongea? Niaba ni uwakilishi wa asiyekuwepo. Utafanya tuamini kuwa kimwili upo nasi pale lakini kiroho upo sehemu nyingine kabisa.

Vinginevyo utatufanya tujiandae kushindwa kukuelewa hasa pale ulipochapia: “Tunawaletea bidhaa zenye standard za ubora wa juu” .Ungejua… neno likijirudia linaweza kuharibu maana. Mfano ukisema “Nampenda huyu msichana wa kike” unamaanisha yupo wa kiume. Nani sasa? Shoga?

Hali hii imefanya watu kuamini kuwa hivi ndivyo ilivyo. Tangu anakua anawasikia wazee wake wakisema Hosiptali badala ya Hospitali, Briskefu mahala pa Brifkesi, Inshu badala ya Ishu, Ballposition badala ya ballpossession na mengine mengi.

Mungu bariki siku hizi Mzee Kifimbocheza hagawi dozi mitaani. Vinginevyo jirani yangu anayejiita mwalimu wa twisheni asingekuwa na jeuri ya kuandika bango, ati: “Lean Engrish/Swahiri Glamour” (Learn English & Swahili Grammar).

Kifimbocheza angeanza kumtandika yeye, kisha angetinga mjengoni, mahakamani mpaka kwenye nyumba za ibada!