Bahati nasibu sekta inayokua kwa kasi lakini inahitaji tahadhari

Meneja wa uhakiki mapato Zantel, Anne Killindu (kushoto) Nadhifa Kassim Juma funguo za pikipiki baada ya kuibuka mshindi wa promosheni ya jero yako hivi karibuni.

What you need to know:

Historia ya michezo ya kubahatisha nchini, inaonyesha mpaka mwaka 1985, kulikuwa na Bahati Nasibu ya Taifa pekee.

Wananchi wengi waliokuwapo miaka ya 1980 wanashuhudia ongezeko la kampuni za bahati nasibu zinazopewa nafasi kwenye vyombo vya habari.

Historia ya michezo ya kubahatisha nchini, inaonyesha mpaka mwaka 1985, kulikuwa na Bahati Nasibu ya Taifa pekee.

Lakini, kutokana na mabadiliko ya sera za uchumi yaliyofanywa katikati ya miaka ya 1980, sheria iliruhusu sekta hiyo kujiendesha kibiashara.

Kufanikisha hilo, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania ilianzishwa Julai 2003 ili kuratibu, kusimamia na kuongoza masuala ya bahati nasibu nchini.

Mabadiliko hayo yamechangia kuwapo kwa kampuni nyingi zenye leseni ya kuendesha biashara hiyo. Zipo za michezo kama vile soka, ujumbe mfupi wa maneno, kasino, mashine za kubahatisha na mashine za slots (Slot machines).

Ongezeko hilo la kampuni za bahati nasibu linejidhihirisha kwenye mapato ya Serikali hata wananchi wanaoshiriki kutokana na usimamizi makini unaofanywa na GBT na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Mapato

Taarifa za GBT zinaonyesha kumekuwa na ongezeko la mapato kutoka sekta hiyo kwa miaka mitano mfululizo hata kuishawishi Serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya fedha mwaka jana.

Kumbukumbu zinaonyesha mapato hayo yamepanda kutoka Sh11.4 bilioni katika mwaka wa fedha 2012/13 mpaka Sh36.8 bilioni mwaka 2016/17.

Mchango wa kodi ya sekta hiyo kwa miaka mitatu iliyopita umekuwa wa kuvutia. Inaelezwa, mwaka 2014/15 Serikali ilikusanya Sh15.3 bilioni kiasi ambacho kiliongezeka mpaka Sh24.4 bilioni mwaka 2015/16 na Sh36.8 bilioni mwaka uliopita wa fedha.

Ufanisi huo, pamoja na mambo mengine unatokana na matumizi ya teknolojia kusimamia uendeshaji wa michezo yote ya kubahatisha.

GBT inatumia mfumo wa kidijitali kuratibu miamala yote inayofanywa na kampuni zinazochezesha bahati nasibu nchini. Kila kampuni, kanuni zinaelekeza, kuiruhusu bodi hiyo kufahamu mapato yanayokusanywa kila siku hivyo kuirahisishia kufahamu kinachoendele ana kudhibiti ukwepaji kodi.

Kutokana na maendeleo yaliyoshuhudiwa Mabadiliko yaliyomo kwenye Sheria ya Fedha mwaka 2017 yanaipa TRA jukumu la kukusanya mapato ya sekta hiyo kuanzia mwaka huu wa fedha.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa GBT, James Mbalwe kampuni za bahati nasibu zimeongezeka kutoka tano miaka mitatu iliyopita 26 mwaka huu. Kutokana na hilo, anasema: “Mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha yanatarajia kuongezeka hadi Sh39 bilioni mwaka huu wa fedha.”

Zantel

Kutokana na urahisi wa kushiriki, wananchi wengi; wazee kwa vijana wanaweza kubahatisha. Matumizi ya simu za mkononi pamoja na intaneti ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kukua kwa sekta hiyo.

Pamoja na mambo mengine, bahati nasibu huibua matumaini na kurejesha furaha kwa watu wengi hasa wenye kipato cha chini kutokana na mabadiliko ya ghafla ya kipato katika maisha yao.

Nadhifa Juma (30), mkazi wa Mburahati jijini Dar es salaam hivi karibuni alijishindia pikipiki katika promosheni ya jero yako inayochezeshwa na kampuni ya mawasiliano ya Zantel ambaye anaeleza furaha yake na jinsi zawadi hiyo itakavyomsaidia kiuchumi.

“Nilipopigiwa simu kuambiwa nimeshinda sikuamini, kiukweli sikudhani kama kuna siku nitakuja kumiliki kitu bila ya kutumia fedha nyingi,” anasema Nadhifa.

Mteja huyo wa siku nyingi wa Zantel anasema hakuwahi kufikiria kuibuka mshindi kwenye bahati nasibu kutokana na uvumi kuwa zawadi huwa zinapangwa.

Kutokana na zawadi aliyoshinda, Nadhifa anasema ataifanya bodaboda ili imuingizie kipato kitakachomuwezesha kuihudumia familia yake yenye watoto wanne na ikiwezekana, kuhama nyumbani kwao na kujitegemea na familia hiyo ambayo ilishampoteza baba.

“Natafuta kijana atakayekuwa anaiendesha hii pikipiki kwani mwenyewe siwezi kufanya hivyo. Ikikaa nyumbani haitakuwa,” anasema Nadhifa.

Ofisa mtendaji mkuu wa Zantel, Sherif El-Barbary alizindua kampeni ya jero yako itakayoendeshwa kwa miezi mitatu mfululizo Janauri 15, mjini Zanzibar. Mpaka itakapokamilika, alisema washindi 235 watazawadiwa.

Katika droo zinazochezeshwa kila mwezi, mshindi mmoja hujinyakulia gari aina ya Suzuki Carry maarufu kama kirikuu huku kila wiki washindi wakiondoka na pikipiki moja na baiskeli nne. Kila siku, simu za kisasa na Sh50,000.

Kushiriki kampeni hiyo, mteja anatakiwa kuweka Sh500 kwenye simu yake na kadri anavyoongeza salio mara nyingi zaidi ndivyo anavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda.

“Zantel tunathamini mchango wa wateja wetu waliotuonyesha kwa miaka mingi. Tunaamini wanastahili kuzawadiwa kwa kutufanya kuwa mtandao bora wa simu visiwani Zanzibar pamoja na kuongoza katika utoaji data nchini,” alisema El-Barbarry.

Twaha Abdallah Seif (40) mkazi wa Mwananyamala A ni miongoni mwa wateja wa kampuni hiyo walioshinda gari anasema itamsaidia katika biashara zake.

“Nilikuwa na ndoto ya kumiliki gari ya biashara itakayoniongezea kipato licha ya kibanda changu cha kuuza simu,” anasema.

Wataalamu

Mhadhiri mwanadamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Deogratius Mahangira anasema kuna mambo mengi yamebadilika siku za hivi karibuni hivyo kuongeza umaruufu wa bahati nasibu.

Kuimarika kwa utandawazi na kushamiri kwa mawasiliano ambayo takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) zinaonyesha kuna zaidi ya watumiaji milioni 40 wa simu nchini, ni chachu ya fursa nyingi zaidi kuonekana kwenye sekta hiyo.

“Kampuni zinafanya ubunifu mkubwa. Zinajua watu wanapenda michezo hivyo zimejielekeza huko. Wadau wa michezo ni wengi, kushiriki kwao kwenye bahati nasibu hizi ni sehemu ya kuunga mkono michezo husika,” anasema Dk Mahangira.

Anasema kuanzia Sh500 au chini ya hapo, wananchi wanapewa nafasi inayoweza kuwapa mtaji wa ama kuanzisha au kuendeleza miradi waliyonayo huku taarifa zikipatikana kwenye simu na vyombo tofauti vya habari.

Kudhibiti ushiriki unaoweza kuleta athari kwa jamii, anasema: “Mamlaka husika ziweke kanuni za udhibiti zitakazosimamiwa na kufuatiliwa kwa ukaribu.”

Mwanasaikolojia wa kujitegemea, Josephine Tesha anasema bahati nasibu limekuwa kimbilio la baadhi ya watu wasio na ajira rasmi ambao huamini mkaa bure si mtembea bure.

“Kutokana na kukosa ajira baadhi ya wananchi hucheza bahati nasibu kama mbadala. Kutokana na mazoea ya kushiriki huo hujiongezea uwezekano wa kuwa na uraibu (gambling addiction) unaoweza kuwaletea madhara,” anasema Josephine.

Kukabiliana na hali hiyo, anasema jamii inahitaji elimu ambayo ni vizuri ikaanzia ngazi ya familia kwa kuwapa taarifa sahihi watoto ambao ni rahisi kuvutika.

Mtafiti mwandamizi wa masuala ya uchumi na jamii, Profesa Samwel Wange bahati nasibu ni uwekezaji wa kucheza na saikolojia za wananchi kwa kuwatamanisha kupata fedha nyingi bila kufanya kazi wala kutekeleza mipango waliyonayo.

“Endapo wananchi wengi zaidi wataendelea kushiriki bahati nasibu hizi, ni mbaya kwa uchumi kwani wanaondolewa kwenye kufikiri na kuweka mipango ya maendeleo na kutegemea fedha za bure,” anasema Profesa Wangwe.