Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI: Bunge halijaitendea haki ripoti ya CAG kuhusu Sh1.5 trilioni

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2016-2017 ilipotoka Aprili mwaka jana mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alikuwa wa kwanza kueleza kuwa kiasi cha fedha, Sh1.5 trilioni hakikujulikana matumizi yake.

Ubishi ulianzia hapo, kwamba Zitto ni mwongo. Upande wa pili ukisisitiza kuwa Serikali lazima iseme ni wapi ilizipeleka Sh1.5 trilioni. CAG Profesa Mussa Assad alipata kuulizwa akajibu Bunge ndilo linapaswa kuibana Serikali iseme hizo fedha zilitumikaje.

Alhamisi ya wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Zitto ni mwongo. Akasema CAG aliulizwa na Rais John Magufuli kama Sh1.5 trilioni ziliibiwa akakataa.

Ndugai akiwa kiongozi wa Bunge, aliyasema hayo akitambua kuwa siku inayofuata (Ijumaa), ndiyo ambayo PAC walipaswa kuwasilisha bungeni uchambuzi wao wa ripoti ya CAG na juu ya ukaguzi maalumu wa Sh1.5 trilioni.

Je, hoja ya Sh1.5 trilioni ni uongo? Jawabu ni kwamba tofauti ya Sh1.5 trilioni ilionekana katika fedha zilizokusanywa na kuingia Mfuko Mkuu wa Hazina. Sh25.3 trilioni zilikusanywa na kuingia hazina lakini Sh23.8 trilioni ndizo zilizotoka, lakini Juni 30, 2017 wakati wa kufunga hesabu ilikuwa inasoma sifuri. Hivyo, hoja ya Sh1.5 trilioni ilikuwa iulizwe, fedha zilienda wapi?

Kitendo cha CAG kurudi kufanya ukaguzi wa namna ambavyo Sh1.5 trilioni zilitumika ni kipimo kingine kuwa hoja hiyo ilikuwepo. Na kumbe sasa, haikutakiwa wabunge wagawanyike, bali wangeshikamana kuibana Serikali ili ieleze fedha hizo zilipokwenda na zilivyotumika.

Ukipitia mjadala wa ndani ya Bunge na hitimisho la taarifa ya PAC, utaona kuwa ripoti nzima haikutendewa haki. Na mwanzo wa kutotendewa haki ni kauli ya uongozi wa bunge kujielekeza kwenye uongo au ukweli kuhusu sakata la Sh1.5 trilioni badala ya kuweka nguvu kuutafuta.

Mathalan, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema kuwa ripoti imeonyesha hakuna wizi wala upotevu wa Sh1.5 trilioni. Akafafanua kwamba kamati yake hufanya kazi yake kwa weledi na hufanya uchunguzi wa kina.

Alisema, baada ya Serikali kufanya marekebisho ya kimahesabu, hakuna tofauti yoyote, kwa hiyo mapato na matumizi yalipata uwiano. Hapa pia inaleta hoja kwamba Serikali ilifanya marekebisho ya hesabu, ndiyo maana tofauti ya Sh1.5 trilioni imeondoka. Hapohapo kuna hoja ya mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Catherine Ruge kuwa hoja ya Sh1.5 trilioni imeshahama na sasa fedha ambazo hazijulikani matumizi yake zimefikia Sh2.4 trilioni.

Nilitamani Catherine afafanue hiyo tofauti ya Sh2.4 trilioni imefika vipi, kwani naye alikuwa anafanya marejeo ya ripoti ya ukaguzi maalumu ya CAG. Tatizo hakukuwa na kujikita kwenye masuala ya msingi, badala yake siasa zilionekana kuteka mjadala. Pande mbili zikizomeana.

Mbunge wa Wete (CUF), Mbarouk Ali alichangia na kueleza kuwa matatizo mengi ya kimahesabu yapo kimfumo, kutokana na Hazina kutokuwa na utaratibu mzuri wa kuweka rekodi za kifedha.

Zitto alisimama kumpa taarifa Ali kuhusu ripoti ya CAG kuhusu suala la kubadilisha matumizi ya fedha. Kwamba kwenye ripoti ya CAG, inaelezwa Sh976.97 bilioni zilibadilishwa matumizi kinyume na sheria. Zitto akasisitiza ni maneno ya CAG siyo yake.

Ali alipoulizwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuhusu kupokea taarifa ya Zitto, alijibu anaipokea, kisha akaongeza kuwa katika Sh976.97 trilioni, ni Sh1.25 trilioni ndizo zilipata ufafanuzi wa Wizara ya Fedha na Sh975.71 trilioni zikiwa hazijapata maelezo.

Hiyo danadana ya Zitto na Ali iliyotufikisha kwenye fedha nyingi Sh975.71 trilioni, kwamba zilibadilishwa matumizi yake bila kufuata utaratibu, kwangu naona ilipaswa kupata mjadala mpana. Mapema kabla ya mjadala, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, aliomba ripoti ya CAG ya ukaguzi Maalum wa Sh1.5 trilioni iwepo bungeni ili ijadiliwe pamoja na taarifa ya PAC. Tulia alimjibu kuwa kazi ya kupitia ripoti ya CAG imeshafanywa na PAC, kwa hiyo wabunge walitakiwa kujadili taarifa ya kamati.Bunge halijaitendea haki ripoti nzima ya ukaguzi wa Sh1.5 trilioni.

Kwa nini mbunge anaomba ripoti ya CAG iwekwe bungeni anakataliwa? Kweli mbunge anafungwa kujadili taarifa ya PAC peke yake bila kuangalia hoja mahsusi za CAG? Kimsingi naona kuna mambo mengi yamekosa msisimko kwa sababu ya siasa.

Bunge halijaitendea haki ripoti nzima ya ukaguzi wa Sh1.5 trilioni.