Seguco yaonyesha njia kuwawezesha wahitimu vijana

Mkulima Elifuraha Semdolo akihifadhi maembe ofisini kwake mkoani Morogoro baada ya kuyakausha. Picha na Veneranda Sumila.

Muktasari:

  • Lakini  ni kazi ngumu kwa nchi kama Tanzania kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia ardhi kutokana na kukitelekeza kilimo pamoja na kwamba ndio sekta inayoajiri Watanzania wengi.

 “Tanzania  itanufaika sana na mpango wa kuboresha uchumi wake kama itaamua kwa makusudi kuwekeza katika kilimo,” anasema mjasiriamali kijana, Elifuraha Semdolo (26), huku akifafanua kwamba nchi yoyote itakayowekeza katika kilimo ikiwa na hali ya hewa njema na ardhi yenye rutuba lazima itaendelea.

Lakini  ni kazi ngumu kwa nchi kama Tanzania kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia ardhi kutokana na kukitelekeza kilimo pamoja na kwamba ndio sekta inayoajiri Watanzania wengi.

Mhitimu huyo wa chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) ni mkulima na mfanyabiashara ambaye anakausha matunda, mboga, viungo na kuviuza.

Semdolo  anategemea zaidi soko la ndani kwa biashara zake kutokana na kukosa fedha za kuifanya biashara hiyo kuvuka mipaka na kuingia katika masoko ya kimataifa.

Mashati magumu kupata mikopo

 Anasema taasisi za kifedha zilizopo nchini zina masharti magumu na kwamba zinatoza riba kubwa na kusababisha wajasiriamali vijana kukwama kupata huduma za kifedha kutoka katika taasisi hizo.

“Kama serikali itazipatia benki fedha za dhamana, ni wazi benki zitapunguza riba na kuwawezesha wajasirimali vijana kukopa kuboresdha shughuli zao na kuuimarisha uchumi,” anasema.

Semdolo anasema kinyume na hali ilivyoTanzania ,vijana wenzao wa Kenya wana nafasi ya kupata mikopo yenye riba ndogo na kupanua biashara zao na  kumudu ushindani wa kibiashara.

Anasema mwaka  2011, aliomba mkopo wa Sh 290  milioni kutoka Benki ya CRDB, lakini alimbulia Sh20 milioni alizopata mwaka jana huku riba yake ikiwa asilimia 20.

Kabla ya kupewa mkopo mjasirimali huyo alikuwa anauza juisi ya matunda ili kupata kipato.

 “Nikiwa na fedha kidogo nilizotunza wakati nasoma Sua, nilinunua mashine ya kusaga matunda na kuanza kutengeneza juisi ambayo nilikuwa naiuza chuoni, biashara yangu ilifanikiwa sana,” anasema Semdolo.

Anasema baada ya kupata mkopo mwaka jana alitumia nusu ya fedha hizo kutanua biashara yake.

Semdolo baada ya kupata mkopo alinunua mbegu na kuanza kilimo cha mboga na rosella chini ya uongozi wa Ushirika wa Wajasirimali Wahitimu wa Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO).
“Sasa natengeneza fedha, nimeajiri wafanyakazi wa kudumu sita na vibarua 60, kila siku nawalipa vibarua Sh2500,” anasema. Hata hivyo anasema kukosekana kwa ardhi ni changamoto kubwa kwake, kwani anahofia hali hiyo itamzuia kujitanua.

“Ardhi ninayotumia ni ya SUGECO ambayo mwakani nitalazimika kuirejesha kwa wanaushirika kwa kuwa muda wangu wa kukaa hapa utakuwa umekwisha,” anasema Semdolo.

“Kwa miaka mingi serikali imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuwavutia wawekezaji wa kigeni, ikiwamo kuwapatia ardhi na kutoa ushirikiano wote muhimu ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora,” anabainisha.

Lakini anasema kwa upande wa wawekezaji wa ndani hali ni tofauti kwani wamekuwa hawapewi kipaumbele. Kwanini serikali isiwawezeshe wawekezaji wazalendo ili nao wapate nafasi ya kuendesha  biashara?

Mchumi wa kilimo wa SUA, Anna Temu ameitaka serikali kutenga ardhi ili wajasiriamali vijana wapate ardhi yenye rutuba bure au kwa fedha kidogo.

“Kwa kuwapa ardhi yenye rutuba watachochea uchumi kukua na kuwa njia ya kukabiliana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na kuzuia vijana kukukimbia vijijini kwenda mijini,” anasema Dk Temu.

Anasema serikali inawasikiliza zaidi wawekezaji wageni ambao hutumia fursa za kuwekeza nchini kupeleka faida kwao na kuiacha Tanzania ikiwa maskini.

 “Wajariamali wetu wanatengeneza fursa nyingi za ajira na kila senti wanayoipata inabaki hapa nchini kwa shughuli za kiuchumi na kijamii,” anasema Dk Temu.

Anasema kama kweli serikali inataka kuondoa umaskini miongoni mwa watu wake ni vyema ikatoa ruzuku za kununua pembejeo kama matrekta ili wazawa watumie kubadilisha kilimo chao.

“Inasikitisha kuona kwamba taifa bado linategemea jembe la mkono kuendesha kilimo, kama kweli serikali ipo makini katika kuinua kilimo inunue matrekta ambayo wananchi watamudu kununua na pia kuwakodisha wengine,” anabainisha.

Wawekezaji wa nje wanapendelewa

Dk Temu ametaka wakala na mashirika mbalimbali ya serikali kama Shirika la Viwango nchini (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kutekeleza wajibu wake badala ya wananchi kuwaogopa.

Anaweka wazi kwamba serikali ifikirie kuwasamehe kodi wawekezaji wazalendo kama inavyofanya kwa wawekezaji wa kigeni.

 “Haingii akilini mkulima maskini analazimika kulipia kodi zote zikiwamo za tozo za mazao wakati mwekezaji wa kigeni ambaye ni tajiri anapewa likizo ya kodi. Hali hiyo inawanyonya Watanzania kwa manufaa ya taifa lao,” anasema Semdolo.

Kutokana  na matatizo hayo yote Semdolo anajipanga kupanua biashara yake ili angalau apate Sh100 milioni  kwa mwezi katika miaka kumi ijayo.

Ushirika wa wajasirimali wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO)  unasaidiwa na BEST AC kuendesha mradi unaojulikana kama ‘Incentives for Agriculture Business Start-ups.’

Habari zaidi:

Rais Jakaya Kikwete alipongeza mradi wa Sugeco katika hotuba yake ya  siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika Mbeya mwaka huu. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo:
Ndugu Wananchi; Tunakamilisha  taratibu za kuwekeza fedha zaidi katika Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi (maarufu kwa mabilioni ya bwana fulani).  Tutaweka utaratibu mzuri zaidi utakaofanya mfuko kuwa endelevu na kunufaisha zaidi walengwa.  

Katika miaka mitano ya uhai wa mfuko huu, tumejifunza kasoro mbili ambazo zitarekebishwa katika utaratibu mpya.  Kwanza waliofaidika na mpango huo hawakuandaliwa ipasavyo.  Na, pili,
hapakuwapo na utaratibu mzuri wa kufuatilia na kupima matokeo yake.

Kasoro hizo zitaepukwa safari hii. Bahati nzuri programu inayotekelezwa na Wizara ya Kazi na Ajira SUA, na CRDB kwa vijana waliohitimu vyuo vya elimu ya juu nchini ili waweze kujiajiri katika sekta ya kilimo na ufugaji, inatoa mwongozo mzuri wa namna bora ya kuboresha Mfuko huo.  

Katika programu hii, vijana wanaopewa mikopo, hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na baadaye kupatiwa mikopo.
Utaratibu huo umeonyesha mafanikio makubwa.