Fahamu sheria na utaratibu wa mirathi kisheria

Muktasari:

  • Kifo cha wazazi au ndugu hutokea bila kutarajia na kinachofuata huwa ni urithi wa mali. Kuna sheria zinazoongoza na kusimamia mirathi ambazo ni vyema ukazifahamu ili kupunguza usumbufu unaoweza kujitokeza.

Urithi wa mali iliyoachwa na marehemu una sheria na utaratibu wake. Sheria na kanuni hizo zinaongoza ukusanyaji, uangalizi, usimamizi, ugawaji na umiliki wa mali husika.

Lengo kuu la sheria za mirathi ni kuepusha mali zilizoachwa kuharibika au kupotea bure. Vilevile zinasimamia haki ya warithi halali hata wanaomdai au wanaodaiwa na marehemu.

Zipo sheria kadhaa zinazoongoza utaratibu wa ugawaji na usimamizi wa mali za marehemu nchini nazo ni Sheria ya Serikali, Sheria ya Mila na Sheria ya Dini ya Kiislam.

Sheria ya Serikali inaongoza na kusimamia mgawanyo wa mali za marehemu ambaye alikuwa hafuati Sheria za Kiislam wala za kimila au kwa waislamu wasiotaka itumike katika mgawanyo wa mali zao.

Kulingana na sheria hii, mjane anapata theluthi moja na watoto theluthi mbili ya mali iliyoachwa. Kama marehemu hakuacha watoto, basi mjane atapata nusu ya mali na zilizobaki zitaenda kwa wazazi na ndugu wa marehemu. Sheria hii haiwatambui watoto wa nje ya ndoa isipokuwa kwa wosia.

Serikali ilizitambua sheria za kimila za urithi tangu mwaka 1963. Ikibainika na kuiridhisha mahakama kwamba marehemu aliishi kwa kufuata mila na desturi za kabila lake, basi sheria za kimila zitatumika.

Mirathi kwa mujibu wa sheria za kimila; mtoto wa kwanza wa kiume anapewa daraja la kwanza akifuatiwa na wadogo zake wa kiume kisha dada zake ambao hupata sehemu ndogo ya mali husika.

Mgawanyo wa mirathi kwa Sheria ya Kiislamu huzingatia uwepo wa warithi halali na mali halisi na halali za marehemu.

Bila kujali unafuata sheria ipi, kuna utaratibu unaopaswa kuufuata unapofuatilia mirathi. Unatakiwa kuwasilisha barua ya maombi Rita au kwa katibu tawala wa wilaya (Das) ambayo marehemu ana mali. Yeye atakujazia atajaza fomu na kuwasilisha Rita. Ikiyaona yanafaa, itaiomba mahakama imteue msimamizi.

Mwombaji wa mirathi anatakiwa kulipa ada ya mwanzo ya kusimamia kulingana na ukubwa wa mali. Mtu yeyote wa karibu na mrehemu anaweza kuomba mahakama imteue kuwa msimamizi wa mirathi. Mahakama itafanya uteuzi kama itavyoona inafaa.