Namna ya kupanga bajeti yenye uhalisia kulingana na uchumi

Thursday April 4 2019

 

By Honest Ngowi

Katika msimu wa kujadili bajeti ni wakati wa kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Wiki hii Bunge la Tanzania linajadili bajeti za wizara mbalimbali hadi Juni.

Kwanza, bajeti za wizara zitajadiliwa kabla ya mjadala wa bajeti kuu itakayowasilishwa na Waziri wa Fedha. Mambo mengi yanajadiliwa katika bajeti za kisekta na ile kuu.

Lengo ni kuipata bajeti yenye uhalisia, inayotekelezeka kwa kuzingatia mapato na matumizi. Dhana ya bajeti ina sehemu kuu mbili. Moja ni upande wa mapato na nyingine ni ile ya matumizi. Bajeti ya nchi huonyesha kiasi cha fedha kinachopangwa kukusanywa na kutumika katika mwaka wa fedha.

Kwa Tanzania, pamoja na mambo mengine, bajeti ni chombo cha kutekeleza dira ya maendeleo ya mwaka 2025 kiujumla na mpango wa pili wa maendeleo uliovunjwa katika mipango mitano ya mwaka mmojammoja kimahususi.

Ni muhimu kuwa na bajeti yenye uhalisia kila mwaka kwa sababu rasilimali nyingi zinatumika kuandaa mapendekezo ya bajeti. Hivyo, ni muhimu kupata thamani ya fedha katika mchakato huu.

Uhalisia wa bajeti

Advertisement

Bajeti yenye uhalisia ni ile inayoakisi uchumi wa nchi katika mambo kadhaa ya msingi. Ni bajeti inayolenga kukusanya mapato yanayoendana na uchumi. Mapato haya ni yale ya kikodi na yasiyo ya kikodi.

Hii ni bajeti inayolenga kutumia fedha zinazokusanywa katika nchi kwa uhalisia wake. Ili kuwa na uhalisia katika matumizi, kwanza ni lazima kuwa na uhalisia katika mapato.

Uhalisia wa bajeti kwa upande wa mapato unamaanisha kukusanya kiasi kinachoweza kukusanywa. Kitaalamu, kabla ya Serikali haijapanga bajeti ya mwaka husika itakuwa na ukubwa gani kifedha hutizama hali halisi ya uchumi.

Hali hii huwezesha kupatikana kwa mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi kutoka vyanzo vyote. Hali halisi kimapato ni pamoja na kujua kama yanayotarajiwa yatapatikana ama laa.

Kwa upande wa mapato ya kodi kwa mfano, uhalisia wake hutegemea shughuli za uchumi zitakazotozwa kodi mbalimbali. Ndiyo maana mchanganuo wa mapato ya kikodi unapaswa kuonyesha kiasi kitakachopatikana kutoka na aina za kodi.

Kiuhalisia mapato ya kodi pekee hayatoshi kugharamia bajeti ya nchi ndiyo maana Serikali hupanga pia mapato yasiyo ya kikodi. Haya ni pamoja na fedha za mikopo na misaada kutoka sehemu mbalimbali.

Mikopo ya ndani na nje hutegemea uhalisia wa kuipata. Hii ni kweli pia kwa mapato ya misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo. Hivyo kabla ya kukopa na kutegemea misaada ni muhimu kufanya uchambuzi wa kina wa uwezekano wa kupata mikopo na misaada husika kwa wakati.

Uhalisia wa matumizi

Ni muhimu kupanga matumizi ya bajeti kwa kuzingatia uhalisia uliopo. Katika matumizi, bajeti huwa na upande wa maendeleo na matumizi ya kawaida. Matumizi ya maendeleo ni uwekezaji katika maeneo ambayo yatachochea uchumi katika muda mfupi, wa kati na mrefu.

Huu ni uwekezaji katika miradi kama miundombinu kwa ujumla wake. Hii ni pamoja na barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari na kadhalika. Matumizi ya kawaida ni pamoja na uendeshaji wa Serikali wa kila siku.

Hii ni pamoja na kulipa mishahara, gharama za mikutano, safari na kadhalika. Katika kutafuta uwiano wa matumizi ya maedeleo na ya kawaida ni lazima kuzingatia uhalisia.

Mizania isipokaa sawa katika hili, bajeti inaweza kuathirika. Kwa mfano, fedha za matumizi ya kawaida lazima ziwe za kutosha kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Ili kupata bajeti yenye uhalisia ni muhimu kuzingatia mambo ya msingi katika mapato na matumizi. Kwa upande wa mapato, bajeti yenye uhalisia ni ile ambayo inazingatia kukusanya kinachoweza kukusanyika na sio vinginevyo.

Hii ni kweli kwa mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi pia. Inabidi kufanya makadirio ya mapato yenye usahihi mkubwa ili kupata bajeti yenye uhalisia.

Advertisement