UBUNIFU: Msichana anayetumia teknolojia kubuni programu

Wakati idadi ya Watanzania wanaopata intaneti ikiongezeka huku wengi wakiwa watumiaji wazuri wa mitandao ya kijamii, Modesta Msabila anatamani wasichana wengi wangekuwa wanajua kutengeneza programu za kompyuta kama yeye.

Modesta ni miongoni mwa zaidi ya wasichana 1,000 waliopikwa kibunifu na Taasisi ya Apps and Girls ya jijini Dar es Salaam.

Mbunifu huyu anayeishi Kiwalani jijini Dar es Salaam, kama walivyo watoto wengine, alikuwa mdadisi tangu akiwa mdogo na mpaka anaanzishwa Shule ya Msingi Kigilagila kabla ya kujiunga na Sekondari ya Kisutu, aliendelea kuwa hivyo.

Akiwa shule ya msingi hakuwa anasafiri mpaka alipojiunga kidato cha kwanza; ndipo alipoanza kupata uzoefu mwingine ikiwamo kushikwa vibaya au kuzuiwa kupanda daladala. “Watu wazima waliomo (ndani ya daladala) hunyamaza. Wanaona ni kawaida kwa kila kinachofanyika,” anasema Modesta ambaye ni mbunifu wa kiteknolojia.

Aliwahi kulalamika kwa wazazi wake lakini hawakuwa na majibu ya kero hiyo zaidi ya kumtaka awe anawaambia askari trafiki waliopo kwenye barabara anazopita. Hakuridhika.

Hakuwa na cha kufanya lakini akawa anaendelea kujiuliza anachoweza kufanya kupata muafaka wa hali hiyo mpaka pale alipojiunga na klabu ya utengenezaji wa programu za kompyuta (coding club).

Mafunzo ya utengenezaji wa programu hiyo walifundishwa na Taasisi ya Apps and Girls ambayo imejikita kuwajengea uwezo wasichana wadogo kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.

“Nikiwa kidato cha pili ndipo ilikuja taasisi hiyo. Nilijiunga na klabu ya mafunzo hayo. Tulipoanza mafunzo nilianza kuyapenda kwa kuona ukiiambia kompyuta ikupe rangi fulani unaipata. Kila Jumamosi nikawa naenda Mzambarauni walikokuwa wanatufundishia,” anasema.

Kadri walivyoendelea kusoma wakaambiwa wafikirie tatizo wanalotaka kulitatua katika jamii. Anasema alishuhudia wengi wakiacha shule kwa sababu tofauti wengine wakifariki dunia kwa kukosa matibabu hivyo ikawa changamoto kwake kuchagua lakini baada ya kutafakari akawa na mawazo mawili.

“Kwanza ilikuwa kuwa na chanzo cha habari za uhakika, niliona mitandao mingi hutoa habari za uongo ili kuvutia watu kuzifungua.

Ya pili ilikuwa kutengeneza mfumo utakaowaruhusu wanafunzi kuripoti manyanyaso wanayofanyiwa wakiwa kwenye daladala,” anasema.

Kutokana na mawazo hayo, Modesta anasema mshauri wake alimwambia atekeleze wazo la pili.

Anasema kadri mafunzo yalivyokuwa yanaendelea, baba yake alianza kuwa na wasiwasi hivyo ili kumtoa hofu akamuomba kompyuta. “Niliporudi nikamuonyesha tovuti niliyoitengeneza, akashangaa na kufurahi. Akasema endelea kufanya hivyo na umfundishe ndugu yako. Basi nikaendelea nikiwa na baraka zote,” anasema Modesta.

Tovuti

Akiwa kidato cha tatu mwaka 2015, alitengeneza tovuti aliyoiita ‘Kilio Chetu’ ambayo sasa hivi ameibadilisha na anaiita ‘Our Cries.’

Baada ya kuikamilisha, anasema alihitaji Sh10 milioni mwaka huo, hivyo alishiriki shindano la TanzICT lililokuwa linaendeshwa na Tume ya Taifa ya Sayansi (Costech).

Katika shindano hilo lililokuwa na wabunifu 200, alishinda. Anasema baada ya kupata fedha alizitumia kuuimarisha mradi wake kwa kuutangaza.

Modesta anasema mwaka huo pia alipata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania nchini Finland kwenye mashindano ya wajasiriamali wabunifu yajulikanayo kama Slush.

“Tulikuwa wengi. Kwa kuwa nilikuwa mdogo nilikabidhiwa kwa Faraja Nyalandu. Huko nilipata wabia na washauri wa biashara,” anasema.

Baada ya mafunzo aliyopata Apps and Girls akafuzu kuwa mwezeshaji na akapangiwa kufundisha wanafunzi katika shule 19 za Dar es Salaam.

Baada ya kupata ujuzi kwenye mifumo ya kompyuta, anasema mwaka 2017 alianza kujifunza masuala ya roboti na akaomba kushiriki mashindano ya dunia yaliyokuwa yanafanyika Washington, Marekani.

Mwaka huo pia alikutana na mkurugenzi mkuu wa Sumatra na kuuelezea mradi wake. Waliupenda na kuufurahi lakini ili washirikiane walimuambia anatakiwa kuwa na kampuni.

“Wakati huo nilikuwa sijatimiza miaka 18 hivyo nilisubiri nitimize umri huo ili nisajili kampuni,” anasema.

Anasema alishirikiana nao kwa muda katika vikosi kazi kadhaa vilivyowajumuisha trafiki pia. Walikuwa wanatoa elimu kwa wanafunzi na kuwajuza kuhusu tovuti yake. Mafunzo hayo yalikuwa yanafanyika mwaka 2017 alipokuwa amemaliza kidato cha nne.

Alipohitimu sekondari akawa anawaza atafanya nini kuendelea na masuala ya kompyuta huku akisoma;jibu likawa kuomba ufadhili nje ya nchi. Akaenda Afrika Kusini.

“Nilipata nafasi shule inayoitwa African Leadership Academy (ALA) ambayo wanafundisha masomo ya darasani pamoja na ujasiriamali. Katika shule hiyo, wanafunzi huwa na miradi yao hata kabla hawajahitimu,” anasema. Akiwa shuleni hapo alijiunga na programu ya Launch X Enterpreneurship iliyompa fursa ya kwenda kushiriki mafunzo ya uundaji wa roboti katika Taasisi ya Teknolojia Massachusetts (MIT) ya Marekani kwa mwezi mmoja. Aliporudi shule akachaguliwa kuwa makamu wa rais wa klabu ya Launch X.

Fursa zaidi

Alipokuwa anakaribia kumaliza kidato cha sita akawa anawaza kuhusu chuo kikuu ila akauona ugumu wa kusoma nchini. Alijua hawezi kupata mkopo baada ya kusoma nje ya nchi hivyo ikabidi atafute mbadala.

Akiwa ALA akaona fursa ya ufadhili kutoka Kampuni ya Mastercard inayotoa nafasi kwa wanafunzi 30 kwa shule 19 Afrika nzima. “Haya ni mashindano magumu kupata nafasi,shule kubwa mfano IST ya nchini zinashiriki pia. Huwaandaa watu wanaofanya mambo makubwa yanayoleta manufaa kwa jamii zao,” anasema.

Hata hivyo, amepata ufadhili huo na atajiunga Chuo Kikuu African Leadership University kilichopo nchini Rwanda.

Anasema alipotimiza miaka 18 mwaka juzi, alianza mkakati wa kusajili kampuni yake. Kwa sasa anakamilisha mahitaji muhimu kabla ya kuwarudia Sumatra.

Modesta ni mbunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambaye anapenda kuona wasichana wanazitumia fursa zilizopo eneo hilo kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo.

Kwa sasa Apps and Girls inatoa mafunzo pia kwa wasichana walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali yajulikanayo kama Jovia.