Kishika uchumba: Mbinu mpya ya shule kuvuna

Kuna wakati ambao wazazi wengi hujikuta wakikuna vichwa. Ni kipindi cha mwanzo wa mwaka wanapohaha kulipa karo za watoto wao.

Ni kipindi anbacho wazazi hulazimika kutoboa mifuko yao ili kuwaandalia watoto wao maisha bora baadaye

Wakati wazazi kipindi hiki wakijua kiasi wanachopaswa kulipa kama karo, kipo kipindi kingine cha wazazi kuwatafutia shule watoto wao wanaotarajia kuanza kidato cha kwanza hasa katika shule binafsi

Ni kama vile wanacheza kamari, kwa kuwa wanalazimika kutoa fedha kununua fomu kutoka shule zaidi ya moja, kote huko ni kwa ajili ya kutafuta nafasi ya usaili.

Hata hivyo, wasichokijua baadhi ya watu ni kuwa sasa wamiliki wa shule wamekuja na utaratibu wa kuvuna fedha kutoka kwa wazazi ujulikanao kama ‘kishika nafasi’.

Shule na utaratibu wa kishika nafasi

Midraj Ibrahimu ambaye ni mzazi anayeishi jijini Dar es Salaam, anasema kishika nafasi hufanyika baada ya mtoto kumaliza kufanyiwa usaili ambapo hupigiwa simu atoe fedha la sivyo mwanawe atapoteza nafasi baada ya kushinda ufaulu.

‘’Unalipa kiasi hicho ili mtoto asije kwenda shule nyingine au akichaguliwa kwenda shule nyingine, asiweze kwenda kwa sababu mzazi wake atakuwa ameshalipia tayari,’’ anasema na kuongeza kuwa ikitokea mzazi amelipa na mtoto akapata shule nyingine, fedha hiyo hairudishwi.

Kuhusu kiasi cha fedha wanachotoa wazazi kama kishika nafasi, Ibrahimu anasema: ‘’Hapo inategemea na shule kwa mfano mimi nafahamu tu kwa shule ya Marian ambapo mzazi anatoa anatoa Sh500,000 shule nyingine sijui kiwango kikoje.’’

Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Marian Girls, Lighness Massawe anasema kinachotolewa ni sehemu ya ada na sio malipo mengine.

‘‘Ukishalipia fomu mtoto anafanya mtihani kama walivyofanya, analipa tu sehemu ya ada ya mwanaye ya mwakani kuthibitisha kwamba anakuja mwakani, lakini siyo kwamba analipa malipo mengine ili tumchague.

Anaongeza: ‘‘ Ni kwa wale wanaofaulu tu, ili kumwambia kwamba mwanao anakuja mwakani 2020, kwa hiyo lipa tu ki-portion (sehemu) hiki ili kuthibitisha kuwa mwanao ni mwanafunzi wetu mwakani.’’

Pamoja na kukiri kuwa shule binafsi zina lengo la kufanya biashara kupitia wanafunzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo anasema wizara yake haitambui wala

kuukubali utaratibu huo na kuwa watalifuatilia.

“Hiyo gharama ya kishika nafasi inalenga kumfanya mzazi asimwondoe mwanawe, kwa sababu wanajua kuwa wazazi hupeleka wanafunzi kufanya mitihani shule nyingi na anaweza kupata zote, baadaye anachagua aipendayo,”anasem

Anaongeza: “Kama wizara hatuungi mkono, tutalifanyia kazi na tutatoa taarifa.’’

Uuzaji wa fomu

Kutoka kufanya mtihani hadi mwishoni mwa mwaka, ni kipindi kingine ambacho wazazi wanalazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kununua fomu, ambazo baadhi ya watu wana fikra fomu hizo ni mbinu mojawapo ya shule kujipatia kipato.

Mkuu wa shule ya sekondari ya Educare ya mkoani Morogoro Staphord Msite, anakiri kuwa mauzo ya fomu yanawasaidia wamiliki wa shule kupata fedha za kuendesha shule.

Kwake fedha za fomu zina uhakika wa kupatikana tofauti na zile za ada anazosema kuna changamoto katika kuzipata.

“Shule yetu imejiwekea lengo la kuuza fomu 80 za kufanya mchujo wa kuwapata wanafunzi wapya watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani na mpaka sasa fomu 28 ndio zimechukuliwa na Oktoba 7 mwezi ujao ndio tutawafanyia usaili, alieleza.

Hivi karibuni, shule za Marian Boys Girls na Boys zilizopo wilayani Bagamoyo ziliendesha usaili wa karibu wanafunzi 2000 waliokuwa wakiwania nafasi 400 za wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani. Kila fomu iliuzwa kwa Sh25,000.

Fedha za fomu hazitoshi

Meneja wa shule ya sekondari ya Ahmes, Sem Mjema ambaye ambaye shule yake ilitoza ada ya Sh10,000 kwa kila fomu huku ada kwa mwaka ikiwa Sh milioni tatu, anasema licha ya wingi wa watahiniwa fedha hizo hazitoshi.

“Fomu inauzwa Sh10,000 ambayo ni gharama ya kutunga mtihani, kusahihisha na kutoa matokeo. Kuna karatasi, bado kuchapisha na hao watu wana huduma watakazopata, kwa hiyo ukiangalia hata hizo fedha hazitoshi,” alisema alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni.

Shule hiyo ilifanya usaili wake Septemba ikiwa na watahiniwa 900 waliokuwa wakitafuta nafasi 90 za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza

Naye Mkuu wa Shule ya Marian Girls, Lightness Massawe anasema licha ya kutoza Sh 25,000 kwa kila fomu, fedha hizo hazikidhi mahitaji

“Hii selection (uchaguzi) siyo kwa ajili ya ku-raise fund (kukusanya fedha), na huwa hatudhibiti idadi fulani, huwa tunataka kila mtu ajaribu apate,” alisema Massawe hivi karibuni.

Alisema gharama hizo zinahusisha uratibu wa mitihani inayofanyika katika vituo vya Bagamoyo, Dodoma, Kahama na Moshi.

“Kuna uandaaji wa hiyo mitihani, kuitunza mpaka ije kufanyike, isafirishwe ije isahihshwe, wazazi waje wapate matokeo ni gharama kubwa,” anasema.

Shule hiyo na shule mwenza ya Marian Boys zilikuwa na jumla ya watoto wapatao 2000 waliokuwa wakipigania nafasi 400 za kidato cha kwanza katika usaili uliofanyika hivi karibuni.

Pre form one

Umegundua kitu? Ni hivi; leo kila kona ni mabango, kwenye vyombo vya habari ni matangazo. Mabango na matangazo haya yana ujumbe mmoja. Ni ujumbe wa kuhamasisha wazazi na walezi kuandikisha watoto wao kujiunga na masomo ya maandalizi ya kidato cha kwanza, maarufu Kiingereza kwa jina la ‘Pre form one courses’.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini wanafunzi wamekuwa wakilipa kati ya Sh10,000 hadi 100,000 kusomea masomo hayo kwa kila mwezi. Zipo shule zinazotoza karo ya miezi mitatu kwa mkupuo.

Uchunguzi unaonyesha masomo yanayofundishwa ni pamoja na Hisabati, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza , Uraia na masomo ya sayansi.

Mwalimu wa kituo cha The choice Academy kilichopo Temeke Luciana Emanuel anasema dhana ya kuwa vituo hivyo lengo lao ni kupiga pesa siyo ya kweli

Anasema inawezekana dhana hiyo ikawa imechangiwa na wingi wa vituo vinavyoendesha masomo hayo katika maeneo mbalimbali nchini.

”Sisi kwanza tukishampokea mwanafunzi tunahakikisha kuwa tunakuwa na namba za mawasiliano za mzazi wake ili kuweza kuwasiliana naye mara kwa mara kujua maendeleo ya mtoto wake, lakini pia hata ufundishaji wetu ni kama ule wa shuleni ambapo kila jumamosi wanafunzi wanafanya mitihani ili kupima uelewa wao,” anasema.

Mkazi wa jijini Dodoma, Ainea Lukas ambaye watoto wake pacha wamehitimu darasa la saba mwaka huu, anakiri kutoona faida ya watoto kusoma twisheni kabla ya kuanza elimu ya sekondari, akisema inawapotezea muda na fedha hivyo kwake siyo kipaumbele.

Kila mzazi anapenda mtoto wake apate nafasi katika shule yenye sifa. Ni kutokana na hilo baadhi ya wazazi hulazimika kulipa fedha shuleni kupitia kile kinachojulikana kama ‘kishika nafasi’

Hiki ni kitendo cha mzazi kulipa kiasi cha fedha shuleni ili kuuhakikishia uongozi wa shule kuwa mtoto wake hatokwenada shule nyingine.