Kitendawili cha ajira Tanzania

Kwa zaidi ya miaka saba sasa Dawamu Mlay amekuwa akitafuta ajira. Macho na masikio ameviweka tayari kuona ama kusikia lolote kuhusu ajira ya fani aliyosomea ya sayansi za bahari.

Awali alijua fani hiyo ni adimu na tena kama angesomea nje ya nchi, angezidi kujiweka katika mazingira mazuri ya kupata ajira.

Haikuwa hivyo, safari ya miaka kadhaa ya kusoma nchini India imekuwa ni majonzi kwake. Anawakumbuka watu waliowahi kumshauri asomee ualimu. Pengine leo angekuwa katika moja ya shule nchini akishika chaki!

Mlay anamkumbuka rafiki yake aliyemuacha nchini ambaye baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka minne bila ya ajira, aliamua liwalo na liwe. Mhitimu wa shahada ya ya soshioljia tena kutoka chuo chenye heshima nchini --(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam--, akaishia kuwa mfagiaji katika moja ya viwanda vilivyopo kando ya barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Yeye hataki kufagia, bado anaamini ipo siku majaliwa yake yatatimia na kupata ajira ya ndoto yake.

Hali si nzuri

Wakati matarajio ya Mlay na wahitimu wengi wa elimu ya juu yakiwa ni kupata ajira yenye staha, hasa kutoka katika vyombo mbalimbali vilivyo chini ya Serikali, hali ya ajira serikalini na sekta binafsi inakatisha tamaa. Wahitimu wanalazimika kunyang’anyana fursa chache zilizopo.

Desemba 17, 2018 , Sekretarieti ya Ajira ilitoa taarifa inayoonyesha kuwa kati ya Novemba 2015 na Desemba 2018 maombi ya kazi serikalini yalikuwa 594,300, lakini waliopata ajira ni watu 6,554

Hali pia sio shwari upande wa sekta binafsi ambapo kiwango cha ajira kinatajwa kupungua kutoka ajira 239,017 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054 mwaka 2017/18. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya Agosti 14, 2019.

Si kwa elimu ya juu pekee, hata madaraja mengine ya chini maelfu ya vijana wanaoshindwa kuendelea na masomo hawajulikani wanapoishia. Kwa mfano mwaka 2016, waliomaliza kidato cha nne walikuwa 408,372, lakini waliofanikiwa kuingia kidato cha tano na kumaliza masomo miaka miwili baadaye ni 90,001, sawa na asilimia 22. Wanafunzi hao wanapotelea wapi na walipo wanafanya nini?

Wanafunzi walio shuleni na vyuoni wanaunda kundi kubwa la vijana duniani ambao hawana ajira. Ripoti ya soko la ajira kwa vijana kutoka Shirika la Kazi Duniani, (ILO) ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa takriban vijana milioni 71 duniani hawana ajira.

Kiwango cha ajira chaongezeka

Hata hivyo, wakati kwa wengi uhaba wa ajira kwa wahitimu ukionekana kuwa bomu linaloitesa nchi na kitendawili kilichokosa mteguzi, NBS inasema kwa jumla idadi ya watu wanaoajiriwa imeongezeka.

Taarifa iliyotolewa Agosti 14 na NBS kuhusu maoteo ya mwenendo wa hali ya soko la ajira nchini ambayo yanabainisha mabadiliko yaliyotokea katika soko la ajira tangu mwaka 2014 hadi mwaka 2018, inaonyesha kuwa idadi ya watu walio na ajira imeongezeka kutoka milioni 20.0 mwaka 2014 hadi milioni 22.0 mwaka 2018.

“Mwaka 2017/18 kulikuwa na jumla ya ajira 552,063 zilizozalishwa nchini ikilinganishwa na ajira 453,466 kwa mwaka 2016/17. Hili ni ongezeko la ajira 98,597 sawa na asilimia 21.7 kati ya mwaka 2016/17 na mwaka 2017/18,’’ inasema taarifa hiyo na kuongeza kuwa kati ya ajira hizo 552,063 zilizozalishwa ajira 415,009 sawa na asilimia 75.0 zilikuwa ni ajira kutoka serikalini.

Hata hivyo, taarifa inakiri kupungua kwa ajira upande wa sekta binafsi kutoka ajira 239,017 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054.

Wahitimu kukosa sifa

Ukiondoa ukweli kuwa uchache wa ajira hasa rasmi ni moja ya sababu kubwa, uwezo mdogo wa waajiriwa wenyewe kimaarifa na utendaji kazini ni sababu nyingine inayotajwa na wadau wa masuala ya ajira kama sababu kubwa ya kuwakosesha wahitimu wa Tanzania fursa za kielimu.

Kwa mujibu wa utafiti wa elimu katika nchi za Afrika Mashariki uliofanywa mwaka 2018 na Chama cha Waajiri cha Afrika Mashariki (EAEO), nusu ya wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za ukanda huo hawana sifa na ujuzi wa kuajiriwa.

Utafiti huo unaonyesha kuwa vyuo vikuu na vya kati katika nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania, vinatoa elimu isiyowasaidia vijana hao kuajiriwa.

Kwa wahitimu wa Tanzania, mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk Aggrey Mlimuka anasema wana changamoto ya kushindwa kuonyesha nia kubwa ya kujiendeleza katika mafunzo na aina mpya za ujuzi wasizokuwa nazo.

“Pia, wanapungukiwa aina za ujuzi lakini kama uongozi, kufanya kazi katika timu na akili ya kudhibiti hisia,” alisema Mlimuka katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni.

Wakitaka kufanya vema katika soko la ajira, anawashauri kutambua aina mbalimbali za ujuzi zitakazowawezesha kuwa na uwezo wa kuajirika sambamba na kuwa na shauku ya kujifunza mahitaji ya soko kwa maana ya aina mbalimbali za ujuzi zinazohitajika katika soko tangu wakiwa vyuoni.

“Wajenge mitandao ya kitaalamu na wadau wa ajira walioko ndani ya soko. Pia, wawe na utayari wa kufanya programu za mafunzo ya maandalizi kwa ajili ya kazi kama uanagenzi (apprenticeship) na mafunzo tarajali (internship),’’ anasema.

Wanakosa ujuzi wa kazi

Katika andiko lake la “Higher Education System and Jobless Graduates in Tanzania” la 2016, Lyata Ndyali anasema mfumo wa elimu hauzalishi wahitimu wenye stadi na ujuzi wa kazi.

“Hali ya soko la ajira kwa vijana Tanzania inakatisha tamaa kwa sababu wengi wanashindwa kupata ajira na kuishia kufanya kazi katika mazingira hafifu katika sekta ya uchumi usio rasmi,” anasema.

Ndyali anasema vyuo vikuu nchini ni lazima vifuatilie mabadiliko na mahitaji ya soko la ajira ili viweze kufikiri upya na kuja na mbinu mpya.

Ujasiriamali vyuoni

Japo inatia moyo kusikia baadhi ya vyuo vikifundisha masomo ya ujasiriamali, kwa mwalimu mstaafu, Bakari Kheri, ufundishaji huo bado una kasoro kadhaa kama kukosekana kwa ulinganifu kati ya ujasiriamali na kozi husika vyuoni.

“Kuna dhana kuwa ujasiriamali unahusu ufanyaji wa biashara kama vile mtu kugeuka kuwa machinga mtaani. Tunakosea ujasirimali katika muktadha wa elimu vyuoni ni kuwafundisha wanafunzi namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo katika jamii katika kozi wanazosomea,’’ anaeleza na kuongeza:

“Mathalani, wale wanaosomea kozi za lugha au fasihi waelezwe ni kwa namna gani wanapomaliza wanaweza kutumia elimu zao kujiajiri kama vile kuwa wakalimani, kufanya kazi za uhariri. Huu ndio ujasiriamali tunaousema na sio ule wa kutaka kila mtu akauze kitu fulani au abuni kitu kinachoonekana.’’

Sekta ya ajira na elimu lazima zishirikiane

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus anasema kwa muda mrefu sasa sekta binafsi imekuwa ikipaza sauti kuwa vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini haviwaandai wahitimu wazuri au wahitimu wenyewe hawajiandai vizuri kwa soko la ajira. Anasema kwa sehemu kubwa wanafunzi vyuoni wanafundishwa mambo mengi kwa nadharia zaidi.

“Ipo haja sasa kwa sekta ya ajira na sekta ya elimu kukaa pamoja kubainisha mahitaji ya mafunzo vyuoni na kushirikiana bega kwa bega na taasisi za elimu katika kuandaa programu za pamoja za mafunzo. Lengo la kuwa na programu za ushirikiano huo ni kuhakikisha kuwa mafunzo ya nadharia yaende sambamba na mafunzo kwa vitendo,’’ anasema.

“Faida ya kuwa na programu hiyo ni kuwa sekta ya ajira itapata nguvu kazi kutoka kwa wanafunzi wa vyuoni na wakati huo huo kuwaandaa kama waajiriwa wa baadaye na hivyo kupunguza gharama za mafunzo kazini kwakuwa watakuwa tayari wamepata uzoefu wakati wa kuendesha mafunzo kwa vitendo.

Ofisa wa utafiti na uchambuzi wa sera wa HakiElimu, Florige Lyeru anasema ili kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana, Taifa halina budi kuandaa mipango ya kuwafundisha vijana kulingana na mazingira na fursa zilipo.

“Yatupasa kuandaa mitalaa inayoendana na soko la ajira na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kilimo, ufugaji na biashara ambavyo vina fursa nyingi nchini,’’ anasema.