Sababu za mkoa wa Kilimanjaro kushuka umaarufu wa elimu

Zama za wazazi kukimbilia kupeleka watoto kusoma shule mkoani Kilimanjaro hazipo Tena.

Japokuwa ufaulu wa mkoa kitaifa katika mitihani ya kitaifa bado unaridhisha, Kilimanjaro ya sasa sio ile ya miaka ya 1980, 1990. Je, wajua sababu?

Mdau wa elimu, Profesa Honest Ngowi anasema sababu kubwa ni kuanzishwa kwa shule katika maeneo mbalimbali nchini, tofauti na ilivyokuwa zamani, ambapo Mkoa wa Kilimanjaro ndiyo uliosifika kwa kuwa na shule nyingi na nzuri kitaaluma.

“Shule zimeanzishwa sehemu mbalimbali nchini na hii inaweza kuwa sababu ya watu wengi kutoleta watoto kusoma Kilimanjaro kama ilivyokuwa zamani. Ilikuwa ukitaka shule nzuri zilikuwa Kilimanjaro lakini siku hizi zimefunguliwa shule kila mahali, shule za kata, na shule nyingine binafsi, hivyo hamna haja tena ya kuwaleta watoto huku”alisema.

Akizungumzia ubora wa elimu, Profesa Ngowi alieleza kuwa,kwa sasa umeshuka ikilinganishwa na miaka ya nyuma jambo ambalo limechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi.

“Wakati tunasoma sisi,darasa moja lilikuwa na wanafunzi 25 hadi 30, lakini leo unaambiwa darasa moja lina mikondo mingi na wanafunzi ni zaidi ya 100. Suala hili limechangia kupunguza ubora wa elimu, kwani tumeongeza idadi bila kuongeza rasilimali kama walimu na miundombinu mingine kama madarasa”alisema.

Padri Dk Aidan Msafiri anasema mkoa huo sasa haukimbiliwi tena kwa sababu ya shule zilizoanzishwa mikoa mingine kutumia mbinu zilizokuwa zikitumiwa Kilimanjaro zamani ikiwamo udhibiti wa maadili na wadau kujali elimu.

“Nafikiri Kilimanjaro tulijipanga vizuri, turudi pale tulipokuwa kimaadili, kimaono na kiuchumi, na kubwa turudi kwenye mbinu zetu ambazo ni kupenda elimu,kupenda maadili,kuwa na maono ya muda mrefu na vipaombele vya mkoa wetu viwe ni elimu iliyojikita kwenye maadili”anasema.