Bobi Wine anavyotikisa miaka 30 ya utawala wa rais Museveni

Saturday May 11 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Miaka 10 iliyopita mwanamuziki Bobi Wine alitambulika kwa mwonekano wake wa rasta kichwani, tambo za kimuziki akichuana na mahasimu wake kama Bebe Cool na Jose Chameleone.

Kofia nyekundu aina ya barret yenye maneno People’s Power, Our Power ndio utambulisho wake katika ulingo wa kisiasa nchini Uganda na mwiba katika utawala wa nchi hiyo kwa sasa.

“Viongozi wanapogeuka wapotoshaji na watesaji upinzani hubaki kuwa suluhu yetu”. Hiyo ni sehemu ya wimbo Situka ukiwa na mashairi kama: “When our leaders have become misleaders and mentors have become tormentors. When freedom of expression becomes the target of oppression, opposition becomes our position.”

Huu ni moja kati ya nyimbo nyingi za kuhamasisha mageuzi alizoimba Bobi Wine wakati wa uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika mwaka 2016.

Wakati akiimba hivi, wasanii maarufu nchini humo karibu wote walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Rais Yoweri Museveni ili achaguliwe kwa awamu nyingine.

Ni wakati huu ndipo alipoona haja ya kubadili upepo kuwa badala ya kubaki kuimba tu, aliomba ridhaa kwenda bungeni kupaza sauti.

Advertisement

Alianza kama utani tu. Jina la Rais wa Ghetto lilimsukuma kuingia kwenye siasa. Itikadi zake ziliwavutia vijana hasa waliokuwa mashabiki wa muziki wake.

Kabla ya kuingia katika siasa alijigamba kuwa muziki wake unalenga kuburudisha na kuburudisha. Moja kati ya nyimbo zake za mwanzo kabisa, Kadigo ulihusu usafi wa mwili.

Juni 27, mwaka juzi safari yake ya kisiasa ilianza rasmi baada ya kutangazwa mshindi katika Jimbo la Kyadondo Mashariki. Aliibuka na ushindi wa asilimia 77 ya kura zote na kuwabwaga wapinzani wake zaidi ya watatu.

Tofauti na wabunge wengi, wakati wa kuapishwa kwake alibeba bendera ya Taifa kwa kuwa hakugombea kupitia chama chochote...alikuwa mgombea binafsi.

Tangu mwaka jana, Bobi Wine ameonekana si tu mwanamuziki aliyejiingiza kwenye siasa bali mpinzani anayeweka ufa katika ukuta wa Urais wa Yoweri Museveni uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.

Tayari ameonekana kuwa sauti ya upinzani nchini humo.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 37 ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, anaonekana kuvaa viatu vya aliyekuwa mpinzani mkuu wa Rais wa nchi hiyo, Kiiza Besigye.

Wimbi la mabadiliko

Mwanzoni mwa mwezi hii Bobi Wine aliwekwa ndani kwa makosa aliyofanya mwaka jana ya kuandaa maandamano kinyume cha sheria.

Linapokuja suala linalomhusu Bobi Wine, wananchi na wapinzani huungana kumtetea. Kwa mfano alipokamatwa mapema mwezi huu, Jenerali Mugisha Muntu aliyewahi mkuu wa majeshi ya nchi hiyo kati ya mwaka 1989 – 1998 alikemea kitendo hicho akisema hakikubaliki.

Umaarufu wa Bobi Wine ndani na nje ya nchi hiyo unaonekana kuikereketa serikali ya Museveni.

Misukosuko anayoipata imempeleka katika majukwaa makubwa ya kimataifa na kumuongezea umaarufu kiasi cha kutangaza kuwa anataka kumrithi Museveni.

Katika mahojiano yake na DW mwezi uliopita alisema anakusudia kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2021.

Katika uchaguzi huo, Museveni, 74, anaweza kugombea baada ya Bunge la nchi hiyo kubadilisha katiba inayomruhusu kugombea tena.

Kilichompa umaarufu

Sababu moja iliyomuingiza katika uadui na Museveni ni pale alipotamka kuwa utawala wake umetosha.

Hata hivyo, kukamatwa mara kwa ma kumemfanya awe maarufu mara dufu kutokana na matukio ya aina hiyo kuvutia vyombo vya habari hasa vya kimataifa.

Hata hivyo, mwanaharakati na haki za binadamu na mwanasheria maarufu nchini humo, Ladislaus Rwakafuzi anamuonya Bobi Wine kuwa Museveni hajawahi kushindwa vita na wapinzani wake.

Anasema Kizza Besigye aliwania urais 2001, 2006, 2011 na 2016 na zote alianguka vibaya.

Alitolea mfano pia swahiba wa Museveni, Amama Mbabazi aliyewahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kati ya mwaka 2011-2014 naye alikiona cha moto baada ya kugombea Urais mwaka 2016.

Advertisement