HOJA ZA KARUGENDO: Kwa nini tupoteze muda na fedha nyingi kujadili ‘ndiyo’?

“Ukisema ‘ndiyo’ na iwe hivyo, hali kadhalika ukisema ‘siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule mwovu,” Biblia inamnukuu Yesu akizungumzia mtu kuwa na msimamo, uadilifu na uaminifu. Kwamba mtu ukiamua kuisimamia kweli, basi uisimamie bila kutetereka.

Kwa maneno mengine, mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu hawezi kujiwekea kikao cha kujadili kuwa “ndiyo” anayoijua ni “siyo”. Mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu daima anakuwa mbali na unafiki na uovu.

Hoja ninayoijenga leo kwenye makala hii ni kule kupoteza muda mwingi na fedha nyingi kuijadili “ndiyo” ambayo hata kama watu wengi wanajua na kuamini kwamba ni “siyo”, lakini watawala na mfumo uliopo wanaamua kwamba ni “ndiyo”.

Tunahitaji muda kuyashughulikia mambo mengine mengi maana taifa bado ni masikini. Tunahitaji fedha kutekeleza mipango mingi ya maendeleo. Kwa nini basi muda huu unaohitajika hivyo na fedha hizi za maendeleo vitumike kujadili jambo ambalo si lenyewe?

Bajeti yetu inayojadiliwa kila baada ya mwaka mmoja kwa utawala na mfumo uliopo sasa ni “ndiyo”. Ijadiliwe isijadiliwe ni lazima ipitishwe. Hata pale inapoonekana waziwazi kuna ulazima wa kubadilisha, bado inapitishwa hivyohivyo, maana wabunge wa chama tawala ni wengi kuliko wa upinzani.

Wakati mwingine inasikitisha zaidi bajeti inapopitishwa hata bila kujadili vifungu vyote kwa kisingizio cha kukimbizana na muda. Hoja ni kwamba kwa nini wabunge wakae Dodoma miezi miwili wakijadili “ndiyo”?.

Ni busara gani inayotumika wabunge kutumia muda wote huo na fedha nyingi hivyo wakijadili “ndiyo?” Kama lengo ni wabunge kuibariki bajeti, kwa nini bajeti isisomwe kwa siku mbili au tatu na kupitishwa ili kuokoa muda na fedha?

Sina ugomvi na spika na wasaidizi wake kuhusu “ndiyo”, maana huu pia ni mjadala mkubwa. Mfumo wetu wa utawala unamlazimisha spika kuyatanguliza maslahi ya chama chake kabla ya kitu kingine.

Spika wetu, ambaye anatoka CCM, hawezi kwenda kinyume na matakwa ya chama chake ambacho kinatawala nchi na kinataka bajeti ipite jinsi ilivyo, hata kama busara za spika binafsi zinamwelekeza kuunga mkono hoja mbadala zenye kujenga. Ni lazima aangukie upande wa chama chake. Kwa maneno mengine, spika anakuwa mlinzi na msimamizi wa masilahi ya chama ndani ya Serikali.

Kwa kupendekeza muda wa Bunge la Bajeti kupunguzwa kutoka miezi miwili ya sasa hadi siku tatu, sina lengo la kubeza na kutoutambua mchango wa wale wanaotoa hoja nzito za kuonyesha kwamba ndiyo inaweza kugeuka na kuwa siyo. Ninaheshimu sana mchango wa wabunge wa upinzani.

Wanafanya kazi nzuri. Wanaonyesha msimamo, uadilifu na uaminifu kwa wapigakura wao. Lakini ukweli unabaki palepale, kwamba “ndiyo” inaendelea kuwa “ndiyo”, hata wakisema nini.

Ni lazima kushirikiana sote-- vyama vya upinzani, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, mashirika ya dini na watu wengine wenye nia njema-- kupinga Bunge kupoteza muda mwingi kujadili “ndiyo”.