MAKALA ZA MALOTO: Mfumo wa siasa za vyama unajiua au unauawa?

Wednesday November 20 2019Luqman Maloto

Luqman Maloto 

By Luqman Maloto

Walatini wana maneno mawili, ‘de jure’ na ‘de facto’. La kwanza, de jure (by law) humaanisha jambo ambalo lipo kisheria. De facto (in fact), yaani si kisheria lakini uwepo wake ni hali halisi.

Mfumo wa siasa za vyama kwa Tanzania upo kisheria. Kipindi hiki ambacho vyama vinajitoa kwenye uchaguzi, inamaanisha nini?

Je, taifa linakwenda kwenye mfumo wa bila vyama vya siasa? Au tayari kwa hali halisi (de facto) nchi imeshafika huko?

Vema kuuliza maswali hayo kwa sababu tayari kuna mbiu zinatolewa na wanasiasa kuhusu nchi kutangazwa kuwa ya chama kimoja au vyama vifutwe. Kwa nini tunafika huko?

Tanzania haitakuwa ya kwanza kufutwa kwa siasa za vyama, nchi za Ghuba ya Uajemi, Oman na Kuwait, vilevile dola ndogo za Niue, Tuvalu na Palau, hazina vyama vya siasa na maisha yanakwenda.

Mabunge kwenye mataifa hayo, si vyombo vya kitunga sheria na kuisimamia Serikali, bali yanakuwa mabaraza ya ushauri. Na kama inavyofahamika, kupokea ushauri ni hiyari. Watawala huchagua kufanyia kazi ushauri wa Bunge au kuupuuza na maisha yanakwenda.

Advertisement

Wanaosema vyama vifutwe ni kwa sababu wameona siasa za vyama zimekufa kutokana na hali halisi au wanatafuta visingizio?

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, upinzani ulipata nguvu kadiri uchaguzi ulivyofanyika. Mwaka 2010 na 2015, kilikuwa kilele cha kukua kwa vyama vya upinzani na ongezeko la wabunge na madiwani.

Kipindi ambacho nchi imekuwa na wabunge wengi wa upinzani kuliko wakati mwingine wowote, ndio vilio vya wapinzani ni vingi na upinzani unaonekana dhaifu kuwahi kutokea.

Swali, upinzanini dhaifu au unalazimishwa kuonekana dhoofu? Kama vyama vya upinzani ni dhaifu na vinashindwa kwenda na kasi iliyopo, si viombe kujitoa kuliko kujaza idadi isiyo na faida kwao na kwa wapigakura?

Ikiwa vyama vya upinzani vinalazimishwa kuonekana dhaifu, wanaofanya hivyo wanawaza nini kwa sheria za nchi? Katiba na sheria nyingine zinazosema Tanzania ni nchi ya demokrasia ya vyama vingi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alitaka vyama vifutwekisha kiundwe kingine chenye kuitwa Magufuli Ruling Party, lakini Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alimkemea.

Ferdinand Marcos wa Ufilipino mwaka 1972, alitoa Tamko Na. 1081 la kuifanya nchi hiyo kuwa taifa lianloongozwa na sheria ya jeshi, na alipoona uchaguzi hauna maana kwake, alipitisha mpango wa kura za wazi kwa sauti.

Sheria ya kijeshi, utekelezaji wake ni kusimika maofisa wa juu wa jeshi katika nafasi muhimu za Serikali. Hivyo, Serikali ya Marcos baada ya tamko hilo, ilipambwa na mabosi wa jeshi.

Katika kura za kupaza sauti, wananchi walipanga mistari, katikati yao walipangwa wanajeshi, waliotazama wale ambao wangesema hapana kwa mabadiliko ya Katiba. Mwisho kabisa maisha yalisonga mbele.

China leo ina chama kimoja kinachotawala na Rais wao, Xi Jinping, ni wa maisha. Vyama vingine vidogo haviruhusiwi kuwania madaraka. Ni utaratibu wao. Wanaopaswa kuupinga ni Wachina wenyewe ambao wapo kimya na maisha yanakwenda.

Hata Ufilipino walipotangaziwa nchi ni ya sheria ya jeshi, waliyaishi na mabadiliko ya Katiba waliyafanya wenyewe ingawa kwa mfumo batili wa upigaji kura. Walipoona wamechoka, ndipo mwaka 1986 walimpindua Marcos.

Kilichopo kwa Tanzania sasa hivi ni nidhamu mbaya kwa Katiba na kutokuheshimu wananchi. Nchi ya vyama vingi halafu vyama havishiriki uchaguzi, ni kuwafanya wananchi wabaki njia panda, hawajui walipo. Je, nchi inakwenda kwenye chama kimoja au kutokuwa na vyama kabisa?

Kwa namna yoyote ile, kama wapinzani madai yao ya kujitoa katika uchaguzi ni uongo, maana vyama vinajiua. Ikiwa wananchi ndio hawapendi vyama, basi vyama vinakufa. Kama watawala hawataki ustawi wa vyama, dhahiri vyama vinauawa.

Swali gumu ni mahali ambako nchi ipo. Wananchi watabaki njia panda na mambo kwenda kama yalivyo mpaka lini? Je, wananchi watasema ndio hali halisi na kuizoea, au utafika wakati hayo mambo yataingizwa kwenye Katiba, ili iwe kisheria, yaani de jure? Ukweli kipindi hiki Watanzania wapo njiapanda.

Advertisement