MAKALA YA MALOTO: Sirro amehuisha mjadala wa Lissu, Azory Gwanda

Shambulizi la risasi alilofanyiwa mbunge wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, limeacha doa kubwa kwa Jeshi la Polisi, ikiwamo tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari, Azory Gwanda.

Ongeza matukio mengine ya kupotea kwa mwenyekiti wa halmashauri Kibondo (CCM), Simon Kanguye na Ben Saanane, ambaye alikuwa msaidizi wa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema.

Lissu ana miaka miwili na miezi miwili tangu aliposhambuliwa, Azory ametimiza miaka miwili tangu apotee, Kanguye miaka miwili na miezi minne, Saanane amefunga miaka mitatu kamili. Wote hao kesi zao hazijapata ufumbuzi.

Inapaswa kufahamika kuwa tiba ya jeraha la uhalifu ni wahalifu kupatikana na kutendewa haki. Kwa vile suala la Akwilina Akwilini lilifungwa ndani ya muda mfupi, maana yake jeraha la uhalifu halijapata tiba.

Hivi karibuni, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, alizungumza na chombo kimoja cha habari na kueleza kuhusu kesi za Lissu na Azory.

Sirro alisema, shauri la Azory limeshafunguliwa jalada la uchunguzi na kutaka mwenye taarifa za kusaidia kutoa mwanga wa kupotea Azory, aende polisi.

Kuhusu Lissu, alisema polisi wamekosa ushirikiano wa kuanzisha upelelezi, akasema kuwa wanamngoja Lissu na dereva wake warejee nchini.

Sirro amefanya vizuri kuwazungumzia Lissu na Azory, maana kwa kufanya hivyo amesaidia kuuweka hai mjadala wa uhalifu ambao ulitendeka dhidi yao.

Ni kwa sababu bila kuwazungumzia, ukimya unaendelea mpaka Watanzania na familia zao, wataona ni mambo yaliyokufa. Sirro amerejesha uhai na kuchagiza mijadala iendelee. Matukio ya uhalifu hayapaswi kufa kabla ufumbuzi kupatikana.

Pamoja na kufurahia Sirro kuufanya uhalifu dhidi ya Lissu na Azory kuwa mjadala hai, yapo mambo ya kugusia kila upande. Kuhusu Lissu ni swali; polisi wameshafanya nini mpaka sasa na wamekwama wapi kiasi kwamba wanashindwa kuendelea, hivyo kuona Lissu au dereva wake ndio wenye majibu?

Polisi wasiseme wanamsubiri Lissu au dereva wake ndio waanze upelelezi. Walipaswa kuanza upelelezi siku Lissu aliposhambuliwa. Kauli ya Sirro inatonesha kidonda ambacho hakijapata nafuu.

Kuna tofauti kubwa kati ya sentensi mbili; “tumeshafanya upelelezi lakini kuna mahali tunakwama, Lissu na dereva wake watatusaidia” na “tunashindwa kufanya upelelezi kwa sababu Lissu na dereva wake hawatupi ushirikiano”.

Miaka miwili na miezi miwili kuzungumzia kuanza upelelezi ni ukakasi. Lissu na dereva wake waliishi Nairobi Hospital miezi minne. Polisi walishindwa nini kutuma watu kwenda kuwahoji?

Shambulizi dhidi ya Lissu sio madai kusema kama mwenyewe hataki kufungua malalamiko, Jamhuri haina cha kumsaidia. Ni kesi ya jinai. Mlalamikaji ni Jamhuri, Lissu na dereva wake ni mashahidi. Hatuoni ukakasi mlalamikaji kuwategea mashahidi?

Kuhusu Azory, miaka miwili, kauli ya polisi haipaswi kuwa “tumefungua jalada”, badala yake ingeelezwa jalada lililofunguliwa miaka miwili iliyopita linaendeleaje.

Kusema “tumefungua jalada” Novemba 2019, kuna mtu atauliza, “siku zote polisi walikuwa wapi kufungua jalada tangu Novemba 2017?” Tunayo kumbukumbu ya kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, aliyesema Azory alijipoteza kwa sababu za kimaisha na polisi hawawezi kumtafuta.

Utaona kuwa Sirro ameweka hai mjadala wa uhalifu dhidi ya Lissu na Azory, lakini ametonesha kidonda badala kuleta nafuu. Na hapa ndio mahali pazuri kumkumbusha Sirro kauli ya Rais John Magufuli kuwa “polisi wasidhani Watanzania ni wajinga.” Rais Magufuli alisema hayo kufuatia hali isiyoeleweka ya kutekwa na kupatikana mfanyabiashara Mohamed Dewji.

Vizuri pia Sirro akaja na maelezo ya kuuweka hai mjadala wa kupotea Saanane na Kanguye, vilevile kupigwa risasi na kuuawa Akwilina.

Akisema upelelezi umeanza au haujaanza ni kutonesha vidonda, akitamka polisi walipofikia, angalau itatoa matumaini na kuleta nafuu kwenye jeraha. Kila jeraha la uhalifu linahitaji tiba au nafuu.