Mo Dewji aonekana hadharani, atoa sadaka

Muktasari:

Leo Oktoba 26,2018 bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’ ameswali swala ya Ijumaa katika msikiti wa Shia uliopo Mtaa wa Idhira Gandhi katikati ya jiji la Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu kutekwa na kutelekezwa na watu wasiojulikana 

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohamed Dewji ‘Mo’ leo Ijumaa Oktoba 26,2018 ameswali swala ya Ijumaa katika msikiti wa Shia uliopo Mtaa wa Idhira Gandhi katikati ya jiji la Dar es Salaam.

‘Mo’ amehudhuria swala hiyo saa 7 mchana ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana hadharani tangu alipotelekezwa na watekaji Jumamosi iliyopita ya Oktoba 20, 2018 katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Bilionea huyo kijana, alitekwa na watu wasiojulikana alfajili ya Oktoba 11,2018 katika  Hoteli ya Collesium jijini Dar es Salaam alikokuwa amekwenda kufanya mazoezi ‘Gmy.’

Kuonekana kwa ‘Mo’ hadharani kuliamsha hali ya waumini waliokuwa wakiswali na wale wa nje wakitaka kumwona ‘live’ baada ya gari lale jeusi lenye jina la ‘Mo 1’ kuwa limeengeshwa nje ya msikiti huo.

Baada ya swala hiyo, ‘Mo’ amekuwa mtu wa mwisho kutoka msikitini na wakati huo waumini na wananchi walikuwa wamejazana nje karibu na gari hilo wakisubiri kumwona.

Siyo waliotaka kumwona tu ‘Mo’ bali baadhi ya wananchi ambao hukaa milangoni na karibu na msikitini wakisubiri kupewa sadaka, walikuwa kando ya gari la mwekezaji huyo wa Klabu ya Simba.

Mara ‘Mo’ akatoka ndani, akiwa amevalia shati jeusi na suruali vyote vya rangi nyeusi pamoja na miwani huku akisindikizwa na mlinzi wake ambao alimfungulia mlango na kupanda.

Baada ya kupanda kwenye gari, wale waliokuwa wakiomba sadaka walilisogelea hali iliyosababisha ‘Mo’ kushusha kioo na kutoa sadaka kwa baadhi yao.