VIDEO: Polisi: Tunaendelea kuwatafuta waliomteka Mo Dewji

Muktasari:

Leo Jumanne Novemba 6,2018, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea na msakako wa watuhumiwa waliomteka mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’


Dar es Salaam. Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas amesema wanaendelea kuwasaka wahusika waliomteka Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohamed Dewji ‘Mo’ na wakibainika watafikishwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Novemba 6, 2018 Kamanda Sabas amesema hakuna kisichowezekana ikiwa Mo mwenyewe kapatikana basi hata hao waliomteka watakamatwa na watafikishwa mahakamani.

“Polisi hatujalala, tutahakikisha tunawakamata tu na tunawasaka kila siku usiku na mchana na tena tunaendelea vizuri tu na uchunguzi wetu,’’ amesema.

Amesema kazi ya polisi ni kufanya uchunguzi hivyo kwa sasa hakuna cha kusema zaidi ya kwamba wanaendelea na uchunguzi kwa wahusika.

Amesema anatoa wito kwa wahusika wasifikirie wameshaokoka na hili tukio polisi bado wapo kazini na wakibainika watafikishwa sehemu husika ili kujibu mashtaka.

Mo alitekwa alfajiri ya Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi na Oktoba 20, 2018 alipatikana baada ya kutelekezwa  katika viwanja vya  Gymkhana.

Soma zaidi: