Uchaguzi wa mitaa ajenda kubwa ndani, nje ya Bunge

Sunday November 17 2019

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Salome

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Salome Makamba akichangia mjadala wa Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais John Magufuli kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wake bungeni Dodoma juzi. Picha na Anthony Siame  

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao utafanyika Novemba 24 mwaka huu ni miongoni mwa hoja ambazo ziliuteka mkutano wa 17 Bunge uliomalizika juzi Ijumaa.

Uchaguzi huo utafanyika huku vyama kadhaa vya upinzani – Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, Chauma, CUF na NLD, UPDP vikiwa vimejitoa katika uchaguzi huo.

Hoja ya uchaguzi imekuwa agenda kubwa bungeni hasa kwa wabunge wa upinzani ambao wamekuwa wakiizungumzia kila walipopata nafasi ya kuchangia katika mkutano huo uliomalizika Ijumaa.

Baadhi ya hoja zilipata ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa Serikali huku nyingine zikigoga mwamba au kuishia kujibiwa kwa vijembe na wabunge wa CCM wakati wakichangia.

Hoja hiyo ilichagizwa zaidi baada ya shughuli ya kuteua wagombea wa uchaguzi huo kukamilika na vyama vya siasa kujitoa kwa madai ya wagombea wao wengi kuenguliwa.

Wabunge hao wametumia fursa hiyo bungeni, kubainisha baadhi ya mambo yaliyoyaita figisufigisu za uchaguzi huo ambazo ni ofisi za watendaji kufungwa ama ili wasitoe au kupokea fomu za wagombea wao, fomu kutogongwa mihuri, kukataliwa kupewa au kurejesha fomu za kuomba kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Advertisement

Fursa zilizotumiwa na wabunge hao kupenyeza hoja hiyo ni katika kuomba miongozo, kipindi cha maswali na majibu, maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu, Mjadala wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo na maazimio ya Bunge.

Akitumia fursa ya miongozo kwa spika bungeni, Maftaha Nachuma, mbunge wa Mtwara Mjini (CUF) alitaka Bunge litoe dakika 30 ili wabunge wajadili kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao iligubikwa na malalamiko katika maeneo mengi kutokana na wapinzani kuzuiwa kuchukua fomu au kuzirudisha baada ya watendaji kufungua ofisi ama kuziacha wazi.

Pamoja na hoja na hiyo, Seleman Jafo, waziri wa mchi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anaishia kujibu kwamba hana maoni yoyote anapopewa nafasi na Spika Job Ndugai kufafanua suala hilo.

Mbunge mwingine aliyejaribu kupenyeza hoja hiyo na kugonga mwamba baada ya swali lake kutojibiwa ni Devotha Minja, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema).

Devota, wakati akiuliza swali la papo kwa papo kwa waziri mkuu, hata kabla hajamaliza swali, alipigwa ‘stop’ na Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa madai kuwa aliandikiwa.

Mbunge huyo anasema hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na

Waziri wa Tamisemi na Naibu wake kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa uko palepale Novemba 24 licha ya vyama vya upinzani kujitoa...

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Akiwa anaendelea kujenga msingi wa swali lake, alikatishwa na Ndugai akimweleza kuwa kanuni zao zinakataza mbunge kuandikiwa swali huko (nje) na kuja bungeni kuwasomea.

“Swali hilo linaonekana kwamba sio la kwako bali umeandikiwa na watu waliokutuma,” akasema Ndugai na kumwita mbunge mwingine aulize swali.

Hata baada ya Devota kujitetea kuwa hakuandikiwa, fursa hiyo ilikuwa imeshamponyoka.

Mbunge mwingine wa Viti Maalumu pia kupitia Chadema, Salome Makamba yeye akaibuka na hoja hiyo wakati wa kujadili Azimio la Bunge la “kumpongeza Rais John Magufuli kwa utendaji uliotukuka katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake”.

Salome katika mchango wake akawaomba mawaziri wamshauri Rais Magufuli atoe kauli yake kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Naomba nilikumbushe Bunge lako (Spika), kwamba mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye waziri mwenye dhamana ya Tamisemi. Lakini pamoja na joto kali na matatizo yaliyojitokeza mpaka leo waziri wetu Dk John Magufuli hatujasikia kauli yake,” anasema.

Anawaomba mawaziri kumshauri Rais Magufuli kwa sababu mwisho wa siku wizara zao zinakwenda vizuri lakini wizara yake inasuasua na kuna doa kubwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hoja ya mbunge huyo inajibiwa na Jenista, mnadhimu wa Bunge na waziri wa nchi katika Ofisi ya waziri mkuu kuwa Katiba inampa mamlaka Rais kukasimu madaraka yake kwa Baraza la Mawaziri na watendaji wengine ambao watamsaidia kutekeleza majukumu mbalimbali.

“Na jukumu hilo limefanywa vizuri na waziri aliyekasimiwa madaraka Selemani Jafo na hivi tunavyoongea Watanzania ni mashahidi kwamba ameshafanya kazi yake vizuri ya kutoa maelekezo kwa kila kinachojiri katika uchaguzi huu, kinachotakiwa kufuatwa na maamuzi ya Serikali katika uchaguzi huu,” anasema Mhagama ambaye anashughulikia sera, bunge, vijana, ajira, kazi na watu wenye ulemavu.

Lakini Salome anabaki na dukuduku, anasema vyama vya upinzani havijaridhishwa na uchaguzi huo na hivyo wanahitaji waziri mwenye dhamana (Rais Magufuli) atoke mwenyewe atoe kauli juu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, Pamoja na msisitizo huo, mbunge huyo hakupata majibu ya kutuliza kiu yake.

Kwa upande wa wabunge wa CCM nao walipenyeza hoja hiyo ya uchaguzi kwa staili zilizotofautiana na wenzao, ikiwemo ya kuwapiga vijembe wapinzani.

Akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2020/2021, Ally Keissy, mbunge machachari wa Nkasi Kaskazini, bila kumung’unya maneno alisema wapinzani hawana hoja na kuwa wamebakia wachache kwa sababu ya kazi nzuri zinazofanywa na Rais Magufuli.

Mbunge mwingine alikuwa ni wa Allan Kiula wa Mkalama wa CCM ambaye anasema kumekuwa na hofu kwa baadhi ya Watanzania juu ya haki ya kupiga na kupigiwa kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhoji kauli ya Serikali.

Wasiwasi wake ulijibiwa na Waziri mkuu Majaliwa akisema kwa utaratibu ambao unaoongozwa kwa kanuni na sheria, anaamini kuwa kila Mtanzania atapata haki yake na kwamba muhimu ni kuzingatia hizo kanuni, sheria na taratibu.

Lakini aliposimama Godluck Mlinga, mbunge wa Ulanga akahusisha kujitoa kwa vyama katika uchaguzi na vurugu zinazotokea, akikitaka Chadema kuwa kujitoa kwake katika uchaguzi ni moja ya sababu za vurugu zinazojitokeza.

Mbunge huyo akahoji Serikali inasemaje kuhusu matukio ya watu kufyeka shamba la msimamizi wa uchaguzi mkoani Songwe na kauli ya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda kuhusu kumtimua mpangaji kwenye nyumba yake kwa sababu haoni umuhimu wa kushirikiana naye.

Maswali ya Mlinga hayakuwa tofauti sana na ya Richard Ndassa, mbunge wa Sumve, aliyehoji Serikali inasemaje kuhusu Chadema iliyoamua kutoheshimu Katiba kwa haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Akijibu maswali hayo, waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola anasema Serikali haitanyamaza wala kutochukua hatua kwa vitendo vyote vya kuhatarisha usalama na mali za wananchi.

Anasema Jeshi la Polisi limejipanga kuchukua hatua kwa mtu yoyote, vikundi au vyama vitakavyofanya fujo wakati wote wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Pamoja na majibu hayo ya hatua za kuchukua, Mwita Waitara, naibu waziri Tamisemi akaongeza uzito kuhusu madai ya viongozi wa mitaa kuwakimbia wagombea akisema hayana ukweli.

Na ili kuepuka baadhi ya migogoro, Nape Nauye, mbunge wa Mtama na Munde Tambwe (Viti Maalum-CCM, kwa nyakati tofauti waligusia hoja ambayo inajadiliwa pia nje ya Bunge kuwa Serikali iunganishe uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu na kuufanya kwa pamoja, kuliko kuutenganisha.

Munde anasema kwa kufanya siku moja uchaguzi wa Serikali za Mitaa, madiwani, wabunge na Rais kutapunguza gharama.

Advertisement