Tume yawarejesha wagombea tisa wa udiwani

Muktasari:
NEC imesema taarifa rasmi za uamuzi zimetumwa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili wawapatie wahusika.
Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewarejesha wagombea tisa wa udiwani katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26,2017.
Kati ya rufaa 15 zilizowasilishwa NEC, tisa ziliwasilishwa na wagombea ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi waliowaengua kutoka katika orodha ya wagombea wa udiwani katika kata mbalimbali.
Tume imesema kuanzia Novemba 3 hadi 4,2017 kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015, ilipokea, ilijadili na kufanya uamuzi wa rufaa hizo.
NEC ikizungumzia rufaa hizo tisa, imesema imezikubali na kuwarejesha kugombea udiwani katika kata husika kuanzia Novemba 4, 2017.
Rufaa sita kati ya hizo 15, Tume imesema ziliwasilishwa na wagombea ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi wa kuwaruhusu wagombea wenzao kuendelea kugombea udiwani katika halmashauri mbalimbali.
Kuhusu rufaa hizo sita Tume imezikataa na imekubaliana na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi, hivyo waendelee kuwa wagombea.
NEC imesema taarifa rasmi za uamuzi zimetumwa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili wawapatie wahusika.