Utata wazingira tukio la mimba ya mwanafunzi kutoka

Geita. Utata umeibuka kuhusu tukio la mwanafunzi wa darasa la tano (13) katika Shule ya Msingi Ibondo iliyopo Kata ya Ludete wilayani Geita anayedaiwa kutoa mimba kwenye choo cha shule.

Katika tukio hilo, mwanafunzi huyo akiwa chooni kiumbe kilianguka kwenye shimo baadaye kondo kutoka akiwa nyuma ya darasa.

Mkunga wa Zahanati ya Ibondo, Aloyce Emmanuel alisema, “Alipofikishwa hapa tumempima na tumebaini alikua na malaria kali, tumempa huduma na dawa,” alisema.

Alisema juzi saa 7:30 mchana walipata taarifa ya mwanafunzi kutoa mimba na walipomchukua na kumchunguza walibaini kuwa hakutoa mimba, bali ilitoka kutokana na kuwa na malaria,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Dk Christopher Peterson wa Dar es Salaam alisema ni vigumu kuthibitisha malaria kusababisha mimba kutoka na kwamba tukio hilo linahitaji uchunguzi zaidi.

Alisema kinachoweza kusababisha mimba kutoka kinaweza kuwa kifafa cha mimba ambacho aghalabu husababishwa na malaria kupanda kwenye ubongo.

Akizungumzia tukio hilo, akiwa katika zahanati hiyo alikolazwa, mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa kutokana umri wake) alisema kwa miezi minne hajapata hedhi na aligundua kuwa ana ujauzito lakini hakuthubutu kusema kwa wazazi wala walimu wake akihofia kuchapwa na kufukuzwa.

Alisema juzi walitakiwa kwenda kulima shamba la shule lakini alishindwa kutokana na kuumwa tumbo na mwalimu alimruhusu kupumzika darasani.

“Niliporudi darasani tumbo lilizidi kuuma nikahisi haja kubwa nilipokwenda chooni nilijisaidia halafu akatoka mtoto.

Nilipokuwa nikirudi darasani kabla sijaingia ikatoka nyama nikaamua kwenda nyumbani hadi walimu walipokuja kunichukua na kunileta zahanati,” alisema.

Mwanafunzi huyo alisema aliyempa ujauzito ni mkazi wa kijiji aliyemtaja kwa jina ambalo linahifadhiwa kwa sasa.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Alsacus Karuna alisema walihisi mwanafunzi huyo kuwa mjamzito Ijumaa iliyopita mchana na walimwita na kumuuliza sababu za yeye kuwa mkimya na aliwajibu kuwa anaumwa.

“Ijumaa baada ya wanafunzi kutoka nyumbani kula chakula cha mchana alipita mbele ya walimu ambao walimwita, mmoja alimuuliza mbona tumbo kubwa naye akadai amekula ugali akashiba,” alisema mwalimu mkuu huyo.

Alisema walikubaliana wanafunzi wa kike wa darasa la tano na la sita wakapimwe ujauzito Jumatatu lakini ilishindikana baada ya mwalimu anayehusika kupata matatizo na hivyo kazi hiyo kuahirishwa.

Baba mzazi wa mtoto huyo, William Kwimba alisema hakuwa akijua kwamba mwanae ni mjamzito na siku ya tukio alikwenda shamba na mkewe na walimweleza mtoto wao aende shule.

“Nilipotoka shambani niliambiwa nahitajika shule, nimefika naambiwa mtoto wangu amejifungua nimeshangaa sana maana hakuonyesha dalili zozote za ujauzito,” alisema.

Diwani wa Kata ya Ludete, Sebastian Benedicto alisema suala hilo halipaswi kufumbiwa macho na kutaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinamkamata aliyempa ujauzito.