Wanafunzi 14 wa shule ya msingi, sekondari Bwisya wafa Mv Nyerere

Sehemu ya kivuko cha Mv Nyerere ikionekana kutokana na juhudi za kukinyanyua kivuko hicho zinazoendelea kufanywa chini ya usimamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Picha na Jovother Kaijage.

Muktasari:

  • Wanafunzi 14 wa shule za msingi na sekondari Bwisya wilayani Ukerewe, watatu wakiwa wa msingi na 11 wa sekondari wamekufa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Alhamisi Septemba 20, 2018.

Ukerewe. Wanafunzi 14 wa shule za msingi na sekondari Bwisya wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza wamekufa katika ajali ya kupinduka kwa kivuko cha Mv Nyerere.

Kati yao, watatu ni wa shule ya msingi na 11 wa sekondari.

Akizungumza na Mwananchi jana, kaimu mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Bwisya, Emmanuel Minja alisema wanafunzi 11 wa sekondari walikufa na kati yao, watatu walikuwa wa kidato cha nne huku wengine wakiwa wa vidato vingine.

Alisema kati ya wanafunzi hao wa sekondari, watano walikuwa wa kiume huku sita wakiwa wa kike.

Kivuko hicho kilizama Septemba 20, mita 50 kabla ya kutia nanga katika gati la Kijiji cha Bwisya katika Kisiwa cha Ukara, huku watu zaidi ya 228 wakiripotiwa kufa.

Minja alisema idadi hiyo imetokana na kuwa siku kivuko kinazama wakati kikitokea Bugolora, wengi wa abiria walikuwa wanafunzi waliokuwa wakitokea kwenye gulio.

“Mwanzoni wakati tunapokea miili, wawili walikutwa na soksi mifukoni. Hii inadhihirissha kwamba walikuwa wameenda Bugolora,” alisema Minja.

Alibainisha kuwa shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 900 kabla ya ajali hiyo na kwamba wamehakiki idadi ya wanafunzi waliokufa kupitia rajisi ya darasani na maelezo ya familia zao.

Minja alisema shule hiyo ina walimu 21 na maofisa wengine wakiwamo walinzi na mafundi seremala.

“Kwetu hili ni pigo kubwa kwani wanafunzi hawa, hususan hawa wa kidato cha nne, walikuwa tegemeo kubwa kwenye ufaulu wa mtihani wa kitaifa,” alisema Minja.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bwisya, Sabuni Yohana alisema wanafunzi watatu walikufa katika ajali hiyo na kubainisha kuwa watafuatilia baada ya wanafunzi kuanza kurejea shuleni. “Wote walikuwa wa kiume. Licha ya kwamba shule tayari zimefunguliwa, mwamko bado ni mdogo na kutokana na ajali hii, kumekuwa na kuyumba kwa masomo,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bwisya, Oru Magero alisema, “Nimetembelea baadhi ya familia hapa katika kijiji hiki na vya jirani. Pengine miili mingine ipatikane ila kwa sasa waliozikwa 11 ni wa hapahapa Bwisya.”

Mhandisi aliyenusurika

Katika hatua nyingine, hali ya mhandisi wa Mv Nyerere aliyenusurika katika ajali hiyo baada ya kuokolewa saa 48 tangu kilipozama, inaendelea vizuri.

Mmoja kati ya madaktari katika hospitali ya rufaa Bugando akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini alisema hali ya mhandisi huyo, Agustine Charahani inazidi kuimarika.

Alisema kila anapoingia chumbani alipolazwa mhandisi huyo huanza kumsimulia namna safari ilivyoanza Bugolora hadi Ukara na sehemu aliyokuwa amekaa wakati kivuko hicho kikizama.

“Mgonjwa wetu anaongea sana. Yaani kila daktari akiingia tu anazungumza mwanzo hadi mwisho,” alisema.

Hata hivyo, alisema mhandisi huyo hayupo chini ya ulinzi mkali kama inavyoripotiwa.

Ofisa habari na Uhusiano wa hospitali hiyo, Lucy Mogele alisema hali ya mhandisi huyo inaimarika siku hadi siku.

Charahani ni mmoja kati ya watu 41 waliookolewa wakiwa hai.

Soma zaidi: