Wafanyakazi 3,000 kiwanda cha vigae hatarini kupoteza ajira

Chalinze. Wafanyakazi zaidi ya 3,000 wa kiwanda cha vigae cha Keda (T) Ceramics Company limited, wapo hatarini kupoteza vibarua vyao au kusitishiwa kwa miezi minne kutokana na kiwanda kutaka kufungwa kupisha uuzaji wa bidhaa zilizopo.

Kiwanda hicho ambacho awali kilijulikana kama Tyford, kinatarajia kusitisha uzalishaji kutokana na kupungua kwa mauzo kulikosababishwa na kujaa bidhaa kwenye maghala.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Tony Wu alisema wana vigae zaidi ya mita za mraba milioni 4 kwenye maghala.

“Kutokana na mwenendo wa biashara tukisimamisha uzalishaji kwa miezi minne tunaweza kuuza angalau nusu ya bidhaa na kama ni miezi nane pengine tunaweza kumaliza” alisema.

Wu alieleza kuwa kama kiwanda kingekua kinafanya kazi kwa asilimia mia moja wana uwezo wa kutengeneza mpaka mita za mraba 50,000 za vigae, lakini hawafanyi hivyo kutokana na hali halisi na kwa sasa wanatengeneza wastani wa mita za mraba 42,000 kwa siku.

Akizungumzia sababu ya tatizo hilo, msaidizi wa Wu, Bruce Ni alisema kuna kiwango kikubwa cha vigae kinachoingizwa nchini kutoka China na India na kupungua kwa usafirishaji nje ya nchi kunatokana na vikwazo vya kibiashara na tozo.

Kwa mujibu wa viongozi hao kiwanda hicho kinaweza kuzalisha mita za mraba milioni 12 kwa mwaka, sawa na asilimia zaidi ya 85 ya mahitaji ya ndani ambayo ni mita za mraba milioni 14.

Nani wataathirika

Keda Ceramics imeunda mchoro wa uzalishaji kuanzia kwa wachimbaji wa udongo mpaka wauzaji wa jumla na rejareja.

Miongoni mwa wadau hao ni wasambazaji wa udongo, wasafirishaji, Serikili, vibarua na watoa huduma (Tanesco, Tancoal, mamlaka ya maji na wengine), wafanyabiashara wa jumla na rejareja.

Kwa mujibu wa Ni, mfumo wa uzalishaji utaathirika ikiwamo mapato ya Serikali na ajira zitapungua.

“Kiwanda kimeajiri watu zaidi ya 1,000 kwa ajira za moja kwa moja na wengine 2,000 ajira za nje,” alisema na kueleza kuwa asilimia 95 ya maligafi wanaipata nchini na inayobaki ni kimekali ambazo hazipatikani nchini, hivyo wanaagiza nje ya nchi, huku asilimia 100 ya nishati wanayotumia wanaipata nchini.

Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Saidi Msangi anasema kama kiwanda kitasitisha uzalishaji itamuathiri kwa kiasi kikubwa kwani mahitaji yake na familia yake hutegemea kiwanda hicho.

“Nimeajiriwa hapa tangu Novemba 2017, na kwa kipindi chote nitajipatia ruziki yangu na familia kwa shughuli hii… kusitishwa kwa shughuli za kiwanda kutaniathiri sana,” alieleza Msangi ambaye ni mkazi wa Chalinze.

Akieleza jinsi wadau wengine watakavyoathirika, Ni alisema: “Kwa siku kiwanda kinatumia tani 900 za udongo na tani 200 za makaa ya mawe, tunalipa tozo za bidhaa kila siku… tunalipa TRA, Tanesco na Tancoal, Wizara ya Madini na Serikali ya kijiji.”

Pia usafirishaji wa bidhaa kwa nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Msumbuji na Zambia kunaiingizia Serikali dola 10 milioni (Sh2.3 bilioni) kwa mwaka. Kiwango hicho kwa sasa kitapungua.

Wizara yazungumza

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya alisema kuna viwanda viwili vya vigae nchini vyenye uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa ambazo zitatosheleza mahitaji ya nchi.

Alisema kutokana na hali hiyo, hakuna sababu ya kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.

“Tunahitaji kuwa na ushindani wa haki, lakini vilevile tuhakikishe vile viwanda ambavyo vimeanzishwa hapa nchini vimeendelea kukuwa na kudumu, kwa hiyo tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha viwanda hivi vinalindwa,” alisema Manyanya alipofanya ziara katika kiwanda hicho.

Changamoto

Kiwanda cha Keda Ceramics kipo katika kijiji cha Pingo, Chalinze mkoani Pwani. Ukubwa wa eneo la lradi ni heka 140 za ardhi wakati gharama za mraid huo zikiwa ni dola 70 milioni. Kiwanda kilianza uzalishaji Novemba 2017, mwaka mmoja baada ya ujenzi wake.

Mkurugenzi mtendaji, Wo alisema licha ya kufanya uzalishaji kwa takribani miaka miwili sasa, bado wana changamoto za muda mrefu ikiwemo vikwazo katika kupata wafanyakazi wenye ujuzi na uzoefu unaohitajika.

“Kazi za viwanda zinatokana na uhalisia wa kazi sio vigezi vya kielimu… na wataalamu tunaoingiza wanapata shida ya kuingia nchini kwa kuwa inachukua muda au serikali inasita kuwapa vibali, kwani wanaona kama wataalamu hawa wapo ndani,” alisema na kueleza kuwa viwanda hivyo ni vigeni Tanzania, hivyo ni vigumu kupata wafanyakazi wa ndani wenye ujuzi wanaouhitaji.