Marekani yaionya Iran

Monday January 13 2020

 

Washington, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump ameionya Iran kwa kitendo cha kuwaua raia wake wanaoandamana kuipinga Serikali hiyo.

Raia hao wameanzisha maandamano muda mfupi baada ya Serikali ya Iran kukiri kwamba iliidungua ndege ya abiria ya Ukraine.

Matukio hayo yanajiri wakati ambako Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper alisema milango iko wazi kwa Iran kufanya mazungumzo na taifa hilo bila masharti yoyote.

Ujumbe huu wa Trump umekuja wakati ambako uongozi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu unakabiliwa na changamoto kutoka kwa waandamanaji walio na hasira baada ya nchi yao kunusurika kuingia katika vita na Marekani baada ya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Katika ujumbe wake wa Titter, Trump ameeleza kuwa ulimwengu na hasa Marekani inatazama yanayoendelea nchini humo kwa sasa.

Licha ya onyo la rais huyo wa Marekani, video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha polisi ya Iran na majeshi yakifyatua risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji karibu na eneo la Azadi.

Advertisement

Hata hivyo, mkuu wa polisi mjini Tehran, Hossein Rahimi alikanusha hayo akisema maafisa wake wamepewa masharti ya kutowakabili waandamanaji.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu nayo yamejitokeza na kuitaka Jamhuri hiyo ya Kiislamu kuwaacha raia kuandamana kwa amani kama inavyoruhusu katiba ya nchi hiyo.

Kufariki kwa watu wote 176 waliokuwa kwenye ndege iliyodunguliwa wiki iliyopita na kukiri kwa Iran baadae kwamba kikosi chake kiliilenga ndege hiyo kimakosa kwa kufikiri kuwa lilikuwa ni kombora ndicho chanzo cha maandamano hayo nchini humo.

Inaelezwa kuwa Canada ndiyo nchi pekee iliyokuwa na idadi kubwa ya watu katika ndege hiyo ambako Waziri Mkuu, Justin Trudeau aliahihidi haki kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao.

"Nataka kuzihakikishia familia zote na Wakanada wote, hatutapumzika hadi tutakapopata majibu. Hatutopumzika hadi kutakapokuwa na haki na uwajibikaji," alisema Waziri Mkuu Trudeau

Advertisement