Wajumbe wa Seneti waapishwa kesi ya kumng’oa Trump

Friday January 17 2020

 

Maseneta 100 wa Marekani wameapishwa kuunda Baraza la Mahakama litakaloshughulikia kesi ya kutaka kumng’oa Rais Donald Trump.

Jaji mkuu wa Mahakama ya Juu ya Marekani, John Roberts aliwaapisha maseneta kuhakikisha wanatenda haki bila upendeleo katika kesi ambayo imepangiwa kuanza Januari 21.

Wiki zijazo, maseneta hao wataamua iwapo Trump anastahili kuondolewa madarakani kwa makosa yaliyowasilishwa na Bunge la Wawakilishi – ya kutumia madaraka vibaya na kuzizuia baraza hili kufanya kazi yake.

Jaji Roberts aliwauliza maseneta, "Je mnaapa ya kwamba katika kesi inayomkabili Donald Trump, Rais wa Marekani, ambayo inangoja kusikilizwa, mtatenda haki bila upendeleo kulingana na Katiba, Mungu awasaidie?"

Wajumbe hao wakajibu "Ndio" kabla ya kila mmoja wao kusaini kitabu cha kiapo.

Kiongozi wa walio wengi wa Republican Mitch McConnell aliahidi kutoa ushirikiano na Trump, kisha akaahirisha kikao cha kutathmini iwapo Trump ana kesi ya kujibu na kutangaza kwanza kesi hiyo itaanza kusikilizwa Jumanne saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Advertisement

Trump anakanusha makosa hayo na kusema kwamba kesi dhidi yake ni madai ya uongo.

Vikao vya Seneti vilianza huku msimamizi wa Bunge hilo akihakikisha shughuli za ziko sawa na vifungu vya kumwondoa Trump madarakani vilisomwa na mbunge wa Congress na mwendesha mashtaka mkuu, Adam Schiff.

Schiff ni mmoja kati ya wajumbe saba ambao watakuwa wanafanya maamuzi ya kesi dhidi ya Rais. Alisema hakuna rais ambaye amewahi kuzuia mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye.

Chuck Schumer, kiongozi wa Democratic katika Seneti, alitoa wito kwa mashahidi wapya kujitokeza na vilevile ushahidi wa nyaraka uruhusiwe bungeni. ''Kesi hii inahitaji uthibitisho wa wazi.''

Seneta Susan Collins wa Republican alionekana akibubujikwa na machozi wakati mashtaka yanasomwa.

Wabunge waandamizi wa Democrats walimkosoa McConnell baada ya kuahidi kushirikiana na Trump na kuonekana kama anakwenda kinyume na kiapo walichoapa.

Akizungumza baada ya vikao hivyo, Schumer aliwaambia wanahabari: "McConnell amesema yeye atashirikiana na rais, sisi hatutashirikiana na yeyote."

Schumer amesema anatarajia kwamba wiki ijayo kutapigwa kura ya iwapo mashahidi wataitwa na kuongeza kuwa hajaona azimio la kiongozi wa wabunge wa Republican kuhusu sheria za kufuatwa wakati wa kesi hiyo.

McConnell hajaondoa uwezekano wa mashahidi kuitwa, lakini alipendekeza kwamba hilo litakuwa ni sawa na kuigiza kesi ya kutokuwa na imani ya Rais Bill Clinton 1999, wakati ambapo maseneta walipiga kura ya mashahidi watakaoitwa na kufuatiwa na majadiliano makali na kipindi cha maswali yaliyoandikwa.

Wakati kikao hicho kinaelekea kukamilika katika eneo la Capitol Hill, Trump aliwaambia wanahabari waliokuwa Ikulu kwamba kesi hiyo inastahili kumalizika haraka iwezekanavyo.

"Huu ni uongo mtupu," Rais amesema. "Madai ya udanganyifu yaliyotungwa na Democrats ili wapate kushinda katika uchaguzi.

" Alirejelelea kauli yake kwenye mtandao wa Twitter na kwamba amefunguliwa kesi ya kumuondoa madarakani kwa kupiga simu ya nia njema.

Democrats wanadai kwamba Rais alizuia msaada wa Dola 391 mlioni  ili kushinikiza Ukraine kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa, Joe Biden.

Thuluthi mbili ya maseneta inahitajika ili rais aweze kuondolewa madarakani, lakini kwa kuwa Bunge la Seneta linaongozwa na Republican, Trump anatarajiwa kuondolewa mashtaka hayo.

Timu yake ya utetezi bado haijatangazwa, lakini mawakili ya Ikulu ya Marekani, Pat Cipollone na Jay Sekulow wameombwa kuongoza.

Bunge la Wawakilishi lilipiga kura Jumatano kupeleka madai ya kumwondoa madarakani kwa bunge la Seneti, baada ya kupiga kura 228 dhidi ya 193 zilizokataa.

 

Advertisement