MAKALA ZA MALOTO: Kiongozi anapoona Katiba inamkwaza ajue uongozi umemshinda, ang’oke!

Thursday September 5 2019

 

By Luqman Maloto

Julai 25, 2016, saa 5 usiku, kijana wa Kifilipino, Restituto Castro, alipokea ujumbe wa simu kutoka kwa mtu asiyemfahamu, kumtaka aende sehemu inayoitwa MacArthur Highway, Manila.

Alipofika, akakuta kawekewa mtego. Akazungukwa na askari, jirani yake kukawa na kifurushi chenye dawa za kulevya. Castro ni mmoja wa watu wa mwanzo kabisa kuuawa kwa tuhuma za dawa za kulevya nchi Ufilipino.

Saa chache kabla ya Castro kutolewa nyumbani kwa ujumbe wa simu, Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte alikuwa ametangaza kiyama dhidi ya wauza unga. Alipitisha uamuzi kuwa wauawe mara moja.

Duterte alisema siku hiyo “hatutaacha mpaka muuza unga mkubwa wa mwisho na muuza unga mdogo wa mwisho, wajisalimishe ama tuwafunge jela au tuwazike kaburini.”

Kauli hiyo kali, imekuwa ikilaumiwa kwamba watu wasio na hatia wanatengenezewa ushahidi bandia kisha kuuawa, Castro anatajwa kuwa mmoja wa waliouawa bila hatia.

Castro alikuwa baba mwenye familia yake, akiwa na mke pamoja na watoto wanne. Rekodi za maisha yake zilikuwa safi, aliishi kwa kipato halali na hakuwa mwenye makundi maovu, ila alipowekewa mtego tu, akanasa na kuuawa.

Advertisement

Tatizo kubwa la Ufilipino ni kuwa Duterte amewapa maagizo mazito polisi. Aliwaambia: “Timiza wajibu wako, ikiwa utaua watu 1,000 nitakulinda. Kama unamjua mtumiaji nenda kamuue, ukiwaacha wazazi wake waifanye hiyo kazi wataumia.”

Kwa kauli hizo za Duterte, Ufilipino imefunguliwa awamu mpya ya mauaji. Polisi wanamtaja na kumuua wanayemtaka kisha ripoti zinatolewa kuwa aliyeuawa ni ama muuza unga au teja.

Lawama kubwa Ufilipino ya Duterte ni mauaji nje ya mfumo wa mahakama. Polisi wamepewa mamlaka ya kutuhumu, kuhukumu na kutekeleza hukumu.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa bahati mbaya alitoa kauli yenye kufanana na ya Duterte. Alisema, watu wenye kuua walemavu wa ngozi nao wauawe. Pinda alisema hivyo kwa kuguswa na ongezeko la mauaji hayo kipindi hicho.

Kauli ya Pinda iliibua mjadala mzito. Amri ya wanaoua wauawe sio ya kikatiba. Mahakama ndio chombo cha kutafsiri sheria na kutoa haki. Kiongozi anapaswa kuagiza watuhumiwa wasakwe na kupelekwa mahakamani.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 16, ibara ndogo ya 6 (b), inatamka: “Ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.” Ongeza kuwa Mahakama ndicho chombo cha kuthibitisha makosa.

Kutokana na kauli yake, Pinda aliandamwa na watetezi wa haki za binadamu. Aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Hamad Rashid, alimbana Pinda bungeni ikiwa ni mwanzo wa kutaka kuanzisha hoja ya kutokuwa na imani naye. Pinda aliomba radhi bungeni. Alitokwa na machozi akiwa amesimama kwenye mimbari ya Bunge.

Ipo video inasambaa mitandaoni, inamwonesha Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, akitangaza kuwa ametoa amri vibaka wote wapigwe, wavunjwe miguu na kupewa ulemavu kwa sababu wanapopelekwa mahakamani, wanapewa dhamana na kurejea mitaani kuiba tena.

Tofauti ya kauli ya Pinda na Sarah ipo kwenye amri walizotoa. Pinda alisema “wauawe”, Sarah ametaka “wavunjwe miguu, wapewe ulemavu”, ila kwenye Katiba, dhambi hiyo ni moja. Matamshi ya wote ni ya kuvunja Katiba.

Katiba inataka Mahakama iheshimiwe. Sarah haheshimu mahakama. Mpaka hapo sio tu kavunja Katiba, bali pia kakiuka kiapo chake.

Ni vizuri sauti isikike kuwa kiongozi akiona Katiba inamkwaza, ajue umeshindwa.Huwezi kutumikia kitabu usichokiamini. Kauli sampuli ya iliyotolewa na Sarah, inaonesha anakerwa na Katiba. Anabaki kuwa kiongozi wa nini? Bunge linafaa kumsaidia Sarah ili aachie ngazi.

Advertisement