Mkapa alivyopigishwa jembe Butiama alipomfuata Nyerere

Muktasari:

Baada ya makabidhiano ya ofisi, Mkapa akajikuta hana kazi ya kufanya katika ofisi yake mpya Ikulu wakati huo Mwalimu Nyerere hakuwepo Dar es Salaam; alikuwa amekwenda kijijini kwake Butiama mkoani Mara.

Ukisoma kitabu “My Life, My Purpose” - “Maisha Yangu, Kusudi Langu”, cha Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kina mengi kuhusu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa kutambua kuwa ametawala sana kitabu chake, Mkapa ameandika sababu ni maisha yake ya kisiasa na uongozi kuathiriwa zaidi na Waziri Mkuu huyo wa Kwanza wa Tanganyika, na wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukisoma “My Life, My Purpose”, utapata msamiati “Clinic” – “Kliniki”. Haina maana ya zahanati kama ujuavyo, bali nyumbani kwa Mwalimu Nyerere Msasani, Dar es Salaam. Mkapa ameandika kuwa enzi hizo mtumishi au kiongozi serikalini unaitwa Kliniki, lazima jasho likuchuruzike.

Hata hivyo, Mkapa hakueleza kinagaubaga kwa nini nyumbani kwa Mwalimu Nyerere paliitwa Kliniki.

Badala yake amesimulia jinsi jina hilo livyokuwa likitisha.

Kuhusu sababu ya Msasani kwa Mwalimu Nyerere kuitwa Kliniki, nilimuuliza mwanasiasa mkongwe nchini na Spika wa Bunge wa zamani, Pius Msekwa alisema, hakuwa akifahamu moja kwa moja kwa nini Msasani paliitwa Kliniki.

Msekwa, aliyefanya kazi kwa ukaribu na Mwalimu Nyerere hasa katika chama, alisema anadhani sababu ya Msasani kuitwa Kliniki ni kutokana na kupachukulia kama sehemu ya tiba na wengi waliokwenda walirudi wakiwa wamepona.

“Hii ni tafsiri yangu, ukiona inafaa ichukue. Kliniki ni mahali ambako watu huwa wanakwenda kupata tiba. Msasani kwa Mwalimu Nyerere palikuwa mahali ambapo watu wanakwenda kupata tiba. Mawaziri mbalimbali walikuwa wanakwenda. Hata mimi nilikuwa naitwa, nakwenda, napata tiba. Kwa Mwalimu palikuwa mahali pa kutibiwa hasa,” anasema Msekwa.

Mkapa, alifariki dunia Julai 24, na kwa sasa amelala usingizi wa dawamu, kaburini kijiji cha Lupaso wilayani Masasi, Mtwara. Hata hivyo, si vibaya kudurusu yale aliyotuachia kupitia kitabu chake. Hususan yenye kumhusu Mwalimu Nyerere, aliyefariki dunia, Oktoba 14, 1999. Yaani siku kama ya leo, miaka 21 iliyopita.

Ukiacha hilo la Msasani kuitwa Kliniki, kuna jingine lililoandikwa ukurasa wa 70, sura ya saba. “My First Steps on My Political Journey (Hatua Zangu za Mwanzo Katika Safari ya Kisiasa)”. Mkapa anasimulia uteuzi uliofanywa na Mwalimu Nyerere mwaka 1974.

Mwaka huo, Mwalimu alimteua Mkapa kuwa ofisa habari wake. Kabla ya hapo, Mkapo alikuwa mhariri mtendaji wa Daily News. Alifanya kazi magazeti ya Serikali akitokea ya chama cha Tanganyika African National Union (Tanu).

Ferdinand Ruhinda, aliyepata kuwa msaidizi wa Mkapa, ndiye aliteuliwa kuwa mhariri mtendaji wa Daily News. Hivyo, kwa Mkapa kuteuliwa kuwa ofisa habari wa rais, alimuachia Ruhinda ofisi.

Baada ya makabidhiano ya ofisi, Mkapa akajikuta hana kazi ya kufanya katika ofisi yake mpya Ikulu wakati huo Mwalimu Nyerere hakuwepo Dar es Salaam; alikuwa amekwenda kijijini kwake Butiama mkoani Mara.

Mkapa akawaza afanyeje? Kukaa na kusubiri si mtindo wake wa ufanyaji kazi. Akaona bora amfuate Mwalimu Butiama. Alipofika, alikuta Mwalimu Nyerere akiwa shamba analima kwa jembe la mkono.

“Ben, umekuja kuripoti kazini? Karibu,” Mkapa anamnukuu Nyerere katika kitabu chake. Baada ya hapo Mwalimu aliendelea kulima.

Jiulize, hata ungekuwa wewe, bosi wako ambaye ndiye Rais wa nchi, analima, utasimama pembeni kumtazama? Mkapa akawaza, akaomba jembe ili naye ashiriki kilimo.

Kilichofuata, Mkapa akajikuta analima kwa saa tatu mfululizo. Ameandika kuwa ilikuwa kazi ngumu kwake kwa sababu alizoea kukaa ofisini kwenye madawati ya uandishi na uhariri.

Ameandika kwamba haikuishia siku hiyo, bali kila siku asubuhi, kwa siku walizokuwepo Butiama na Mwalimu Nyerere, waliamkia shambani.

Kwa msisitizo, Mkapa anasema hivyo ndivyo alivyoanza kazi ya ofisa wa habari wa Rais; yaani shambani na msoto wa jembe la mkono.

Mkapa anasimulia kuwa mchana ndio alikuwa anaketi pembeni ya Mwalimu Nyerere akiwa na wageni ili kuchukua taarifa, kisha kuzisambaza katika vyombo vya habari.

Ni stori ya Baba wa Taifa na urais wake, lakini alitenga muda wa kwenda kijijini kulima.

Si kutuma, alilima mwenyewe. Na hiyo taarifa kuwa kama wewe ni mvivu au hujazoea shamba, ungesikia Mwalimu Nyerere yupo Butiama, bora usimfuate. Vinginevyo ungepata msoto wa shamba kwa saa nyingi bila kupenda.

Maana, usingeona sawa kukaa pembeni na kumuacha Mwalimu alime peke yake. Na hicho ndicho kilimpata Mkapa, Rais aliyeiongoza Tanzania kwa miaka 10 (1995- 2005).

Katika mambo mengi yaliyosimuliwa na Mkapa katika kitabu chake kuhusu Mwalimu Nyerere, lipo na hili; Mkapa alipokuwa mhariri mtendaji wa magazeti ya chama, Uhuru na The Nationalist alipitia nyakati za kusakamwa na wanasiasa, hasa mawaziri wake.

Alichukuliwa kuwa ni ‘mnoko’ sana, kiherehere, aliyeandika au kusimamia habari na makala za kumfanya Mwalimu amuone yeye ndiye ‘kichwa’.

Mpango wa mafunzo ya lazima ya Jeshi ya Kujenga Taifa (JKT) ulipoanzishwa mwaka 1964, magazeti ya Uhuru na The Nationalist yalihamasisha kuunga mkono juhudi za Mwalimu Nyerere.

Mwaka 1966, Mkapa alipokuwa anahamasisha ushiriki wa JKT, alipigwa madongo kuwa alihamasisha kitu ambacho yeye mwenyewe hakuwa amekipitia.

Akaenda kwa Mwalimu Nyerere. Akamuomba ruhusa ya kujiunga JKT; akaruhusiwa.

Akaripoti kambini, alikutana na mkufunzi ambaye alikuwa komando wa kike, mrembo sana, lakini hacheki. Hakuthubutu kumwambia chochote.

Kambini alishiriki mafunzo na watu kutoka kada tofauti. Wasomi wenye shahada walikuwa wachache. Wengi walikuwa wakulima na wafanyakazi waliojua kusoma na kuandika tu.

Msoto wa jeshi ulimfanya Mwalimu Nyerere ampotee Mkapa. Mwalimu alikwenda kukagua mafunzo. Wakati wa gwaride, alikagua mstari kwa mstari lakini hakumtambua kijana wake Mkapa.

Iliandaliwa risala ya kusoma mbele ya Rais Nyerere ambaye kicheo pia ni Amiri Jeshi Mkuu.

Mkapa ndiye alichaguliwa kusoma. Wakati anasoma risala, ndipo Mwalimu alimtambua.

Bila shaka ni kwa sauti yake maana alikuwa kakonda, kachakaa.

Mwalimu alivunjika mbavu, alicheka sana kuona Mkapa alivyobadilika mpaka akamsahau.