VIDEO: Wafanyabiashara Coco Beach wazungumzia kauli ya Magufuli

Muktasari:

Wafanyabiashara wa Coco Beach jijini Dar es Salaam wampongeza msimamo wa Rais Magufuli aliyezungumzia  mradi wa Ufukwe huo, wasema yupo sahihi.


Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa ufukwe wa Coco Dar es Salaam nchini Tanzania wamepongeza msimamo wa Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyezungumzia mwenendo wa mradi wa uboreshaji wa ufukwe huo.

Juzi Jumapili Septemba 22, 2019 wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu, Rais Magufuli aligusia suala hilo akisema mradi wa Coco Beach una maswali mengi ya kujiuliza na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo, alishindwa katika mradi wa soko la Mwanjelwa (Mbeya).

Mbali na hilo, Rais Magufuli alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, huwezi ukajenga muundo mkubwa ndani ya mita 60 kutoka au ziwani, lakini cha kushangazwa alipokabidhiwa  kuna mradi mwingine wa daraja la Salender.

Wakizungumza na Mwananchi jana Jumatatu Septemba 23, 2019 wafanyabiashara hao wamesema  Rais Magufuli yupo sahihi hasa  suala la mradi huo kuingiliana na ule wa ujenzi wa barabara zitakazounganisha daraja la Salender. Pia, unakinzana na sheria ya mazingira.

“Msimamo wa rais wa jana (juzi) kila mtu hapa ameufurahia maana kwa vyovyote wahusika watabadilisha taratibu zitakazotusaidia.”

“Jambo jingine Rais Magufuli alisema lazima uandae miundombinu mbadala watu wanaopisha mradi, lakini hapa Coco Beach haikufanyika hivyo bali tumeambiwa tunatakiwa kuondoka,” alisema  Yusuf Idd.

Idd alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo ni vyema ukafanyika kwa awamu ili kuwapa fursa wafanyabiashara wa eneo hilo kufanya shughuli zao badala ya kuamuru waondoke.

“Tumepewa mwezi mmoja na nusu, baada ya hapo tunatakiwa kuondoka. Tunawashauri wahusika waanze kujenga kwa awamu, badala ya kutuambia twende Kawe au Msasani,” alisema

Kobelo Munishi alisema suala  kutakiwa kuondoka katika eneo hilo limewaathiri kisaikolojia kwa namna wanavyofanya shughuli za kwenye ufukwe huo.

“Nilimsikiliza kwa makini Rais Magufuli, maelezo aliyoyatoa jana sioni dalili ya wafanyabiashara kuondoka bali tunatarajia kuwekewa utaratibu maalumu,” alisema Munishi.

Katika hatua nyingine, mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema maelekezo yote yaliyozungumzwa na Rais Magufuli yatafanyiwa kazi.