Waziri Jafo azungumzia waraka wa Jiji la Dodoma kuwataka watumishi kujiandikisha

Thursday October 17 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi, Selemani Jafo 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi, Selemani Jafo amesema waraka uliotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wa kuwatambua watumishi waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura una lengo la kuhamasisha watu kushiriki katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Akizungumza jana Jumatano Oktoba 16, 2019, Waziri Jafo amesema alimuuliza mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhusu waraka huo uliokuwa ukizunguka katika mitandao ya jamii akamjibu kuwa ulilenga kuhamasisha kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura.

"Sio kuwa watu wengine watawajibishwa ama kufukuzwa kazi no (hapana).nataka nitoe maelekezo kama ni kuhamasisha inawezekana maandishi hayakuwa vizuri," alisema.

Alisema lengo la waraka huo ni kuona jinsi gani watumishi husika  wanaweza kuwa kipaumbele katika kujiandikisha na kupiga kura kwenye uchaguzi huo.

Alisema isitokee kwamba watu wakatafsiri kuwa inatengenezwa adhabu ama mtu kufukuzwa kazi bali ni suala la kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha.

Pia, alisema ujumbe unaotishia watu wasiojiandikisha hawatapa huduma ambao unasambaa katika mitandao ya jamii hauna ukweli.

Advertisement

Waziri Jafo alisema hakuna atakayepelekwa katika chombo cha sheria wala kunyimwa huduma kwa kutojiandikisha katika orodha hiyo.

Barua anayoizungumzia Waziri Jafo iliandikwa Oktoba 14, 2019 na uongozi wa Jiji la Dodoma kwenda kwa Wakuu wa Idara ya na Vitengo, Watendaji Kata wote pamoja na Waratibu Elimu Kata wote wa Jiji la Dodoma.

Waraka huo ulikuwa na kichwa cha habari ‘Kuwatambua watumishi wa umma walioandikisha katika daftari la wapiga kura ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019.’

“Serikali inataka kutambua majina ya watumishi waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Utambuzi huu unatakiwa kufanyika na kukamilika kabla ya Oktoba 17, 2019 na kuwasilisha majina hayo kwa mkurugenzi wa jiji la Dodoma,” inasomeka sehemu ya waraka huo

“Ili kuweza kuwatambua watumishi waliojiandikisha, utaratibu ufuatao utatumika; kila msimamizi wa eneo la kazi ataorodhyesha majina yote ya watumishi waliopo katika eneo lake, mfano kituo cha afya, zahanati, kata nk,” iliongeza 

 

Advertisement