Tamasha la Mawazo la Kusi lafanyika Rwanda

Kigali. Tamasha la Mawazo la Kusi limeanza rasmi jana katika ukumbi wa mikutano wa Intare uliopo Kigali, Rwanda huku lengo likiwa ni mjadala wa kuangazia mustakabali wa Bara la Afrika.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG) na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), limewaleta pamoja wadau na viongozi walioongozwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, mjumbe wa miundombinu ya Jumuiya ya Afrika, Raila Odinga na Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Donald Kaberuka.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Bodi ya NMG, Dk Wilfred Kiboro alisema tamasha hilo limepelekwa Rwanda kwa sababu nchi hiyo ndiyo mahali pazuri pa kuzindulia sherehe hiyo muhimu na inawakilisha jamii tofauti barani Afrika, haswa zile zilizopitia historia mbaya, kwamba zinaweza kufikia mafanikio.

“Tunaadhimisha miaka 60 kama NMG na tukizingatia hili, tulidhani itakuwa vizuri kwa bara hili kuwa na mazungumzo juu ya mustakabali wake. Ndiyo maana tuko hapa leo,” alisema Dk Kiboro.

“Mkutano huu wa Mawazo ya Kusi ni kwa vijana kuzungumzia wanachopenda kukiona katika miaka 60 ijayo katika nyanja za miundombinu, siasa, elimu, afya, kilimo na teknolojia.”

NMG ilizindua sherehe hizo kama sehemu ya ajenda yake ya mabadiliko ya kijamii na kuanza ‘kujenga mawazo ya pamoja ya Waafrika wote’ ili kukuza fursa na uvumbuzi unaopatikana katika karne hii.

Mawazo ya Kusi yatatoa jukwaa la kimkakati la kuangalia nyuma Afrika katika miaka 60 iliyopita na kuweka kasi ya miaka 60 ijayo.

Mazungumzo katika tamasha hilo yatazingatia mada nne muhimu ambazo ni kulisha mabilioni ya Afrika; kuelekea Bara lisio na mipaka, mabadiliko ya tabianchi na usalama wa binadamu barani Afrika.

“Tamasha litafanyika katika miji mbalimbali ya Kiafrika kila mwaka ili tuweze kuruhusu uhusiano wa watu ambao wataunda mabara katika miaka 60 ijayo,” alisema Dk Kiboro.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Odinga alisema atashiriki kuzihamasisha Serikali za Afrika katika kutoa fursa zaidi kwa vijana ili wafanikiwe.

“Kama viongozi, tunahitaji kuangalia ni wapi tunaelekea na si kukaa nyuma. Tunapoanza hili, inamaanisha tutakuwa tunapanga kwa bara la baadaye na vijana wake. Wao wanataka, kweli wanataka kujua mengi juu ya mipaka ya mwili lakini ni usalama gani ambao tutawapatia. Ndiyo maana niko hapa,” alisema Odinga.

Wakati wa majadiliano ya jumla kuhusu mustakabali wa kilimo, washiriki walikubaliana matumizi ya teknolojia yanaweza kuisaidia Afrika kujilisha yenyewe.

“Bara linatumia zaidi ya Dola 35 bilioni za Marekani kwa uagizaji wa chakula, wakati uwekezaji ni Dola 11 bilioni za Marekani, tunaweza kubadilisha hili. Tunahitaji sasa kuanza kuona uwekezaji unaobadilisha fursa zetu wenyewe za kilimo,” alisema Dk Diane Karusisi, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Kigali.