ACT – Wazalendo: Wabunge wa CCM watawajibika lolote likimtokea Zitto

Kiongozi wa chama cha ACT Zitto Kabwe.

Muktasari:

Siku moja baada ya baadhi ya wabunge kumwita Zitto Kabwe msaliti, Naibu Kiongozi wa chama cha ACT - Wazalendo, Juma Duni Haji amesema chama hicho kimevichukulia vitisho hivyo vya baadhi ya wabunge kwa tahadhari kubwa na kwamba, watawajibika lolote litakapotokea.

Dar es Salaam. Naibu Kiongozi wa chama cha ACT - Wazalendo, Juma Duni Haji amesema chama hicho kimechukulia kwa uzito mkubwa vitisho vya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya kiongozi wa chama chao, Zitto Kabwe.

Duni ameyasema hayo leo Jumapili Februari 2, 2020 Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari akizungumzia barua ambayo Zitto aliwaandikia Benki Kuu (WB) kusitisha kutoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania.

Amesema tayari chama kimewaelekeza mawakili wake kuliangalia suala hilo huku wakitoa onyo kwamba chochote kitakachomtokea Zitto basi wabunge hao waliomtishia maisha watawajibika kikamilifu.

“Chama cha ACT Wazalendo kimevichukulia kwa uzito mkubwa vitisho vya wabunge wa CCM dhidi ya kiongozi wetu, Zitto Kabwe.

“Tunawaeleza kuwa lolote lile baya litakalomkuta, watawajibika kikamilifu. Chama chetu kimewaweka katika tahadhari wanachama wetu nchi nzima kumlinda kiongozi wao kwa lolote,” amesema Duni.

Kiongozi huyo amesema chama hicho kinampongeza Zitto kwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za watoto wa kike wanaopata mimba kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua.

Amefafanua kwamba barua ya Zitto haina nia yoyote ovu bali alitaka mkopo utolewe kwa Tanzania baada ya changamoto mbalimbali kama vile ukiukaji wa haki za binadamu ziwe zimetatuliwa.

“Tumesikitishwa na tumefadhaishwa na matumizi mabaya ya Bunge dhidi ya kiongozi wetu wa chama, tunachukulia kila neno lililotoka kwa tahadhari kubwa," amesema.